KUSHUHUDIA PAMBANO LA MAYWEATHER MIL 21/-

0
701

 LAS VEGAS, MAREKANI


PAMBANO la bingwa wa ngumi za uzito wa juu, Floyd Mayweather na mpinzani wake, Conor McGregor, linatarajiwa kufanyika Agosti 26 na waandaaji wa pambano hilo wametangaza kiingilio cha juu ni dola 10,000, zaidi ya Sh milioni 21.

Mbali na kuwawekea kiasi hicho cha juu, wametangaza kiasi cha chini kwamba kitakuwa cha dola 500 sawa na Sh 1,096,300. Kiingilio hicho cha chini kitawafanya watazamaji kukaa kwenye jukwaa la juu mbali kidogo na eneo la ngumi.

Bei hiyo ya tiketi inaonekana kuwa kubwa dhidi ya ile ya pambano la Mayweather na Manny Pacquiao lililofanyika Mei 2015, huku kiingilio cha juu kikiwa dola 7,500, zaidi ya milioni 16 na kiasi cha chini kikiwa dola 1,500, zaidi ya milioni 3,288,900.

Pambano hilo la kihistoria linatarajiwa kuteka hisia za mashabiki wengi kutokana na mpinzani wa Mayweather, McGregor kuwa na uwezo wa hali ya juu.

Pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa T-Mobile Arena, uliopo Las Vegas na tiketi hizo zimeanza kuuzwa jana nchini Uingereza.

Mayweather na McGregor wameanza kutambiana kuelekea pambano hilo, huku McGregor akisema kwamba atahakikisha kwenye raundi ya nne anamaliza pambano hilo kwa kumchapa KO.

“Sitakuwa na muda wa kupoteza, ninaujua uwezo wa mpinzani wangu, hivyo lengo langu ni kuhakikisha ninalimaliza katika raundi ya nne kwa kumpiga KO,” alisema McGregor.

Mwishoni mwa wiki iliyopita bingwa Anthony Joshua, alitembelea kwenye mazoezi ya Mayweather na kumpa mbinu za kumpiga mpinzani wake. Joshua ameweka wazi kuwa Mayweather ana nafasi kubwa ya kuwa bingwa kutokana na uwezo wake.

“Sina wasiwasi na Mayweather kutokana na uwezo wake, niweke wazi kuwa mimi ni shabiki wa timu ya Mayweather TMT, hauwezi kuongea lolote juu ya staa huyo, nina imani kubwa ubingwa lazima achukue, nimeanza kumjua Mayweather tangu nikiwa na umri mdogo na mara zote amefanya makubwa,” alisema Joshua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here