30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

kusafirisha mkaa kwa matumizi ya nyumbani mwisho Kg 50

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

KUANZIA sasa watakaosafirisha mkaa unaozidi kilo 50 kwa matumizi ya nyumbani, watapaswakupita katika njia na vituo vilivyoainishwa kwa ukaguzi wa bidhaa hiyo, huku wakibanwa sawa na wale wanaosafirisha nishati hiyo kwa biashara.

Hayo yamo katika kanuni za uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu ambazo zinatafsiri mkaa kwa matumizi ya nyumbani kuwa ni ule usiozidi kilo 50.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, mkaa unapaswa kusafirishwa kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni. 

“Mtu yeyote anayesafirisha magogo, mbao, miti, nguzo au mkaa, isipokuwa mkaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, atapaswa kupita katika njia na vituo vilivyowekwa kwa ajili ya ukaguzi,” inasomeka sehemu ya kanuni hizo.

Kanuni hizo zilizotangazwa Mei 24, mwaka huu kupitia Tangazo la Serikali namba 417, zimegawanyika katika vipengele 24 vikiwamo kamati za mavuno, kazi za kamati za wilaya, mikutano ya kamati, maombi ya uvunaji, aina za uvunaji, utunzaji kumbukumbu na uzalishaji wa mkaa.

Vipengele vingine vinahusu kusitisha kibali cha uvunaji misitu, uvunaji magogo, mbao, mkaa kwa matumizi ya biashara, uvunaji magogo, mbao, mkaa kwa matumizi ya nyumbani, muda wa usafirishaji, usafirishaji magogo, mbao, mkaa kwa matumizi ya nyumbani, kuuza katika maeneo yasiyosajiliwa na usafirishaji mkaa nje.

MAOMBI KWA AJILI YA MAVUNO

Kwa mujibu wa kanuni hizo, mwombaji leseni lazima awe raia wa Tanzania, ameandikishwa kama muuzaji wa mazao ya misitu kupitia kanuni za mwaka 2004, ana leseni halali ya biashara, ana Nambari ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na amelipa ada kama ilivyoelezwa katika Kanuni za mwaka 2004. 

Mtu anayeomba leseni ya kukata miti kwa ajili ya magogo, mbao au uzalishaji wa mkaa, atatakiwa kuwasilisha maombi kwa Meneja wa Misitu wa Wilaya ambaye atawasilisha maombi kwa Kamati ya Wilaya.

Mtu mwenye ruhusa ya kukata miti kwa madhumuni ya magogo, mbao, nguzo au uzalishaji wa mkaa, hataruhusiwa kukata aina nyingine ya miti isipokuwa ile iliyotajwa katika leseni aliyoomba.

Kamati ya Wilaya inaweza wakati wowote kabla ya kumalizika kwa leseni husika kuifuta iwapo uvunaji utakuwa umefanywa kinyume cha kanuni hizo.

Aidha mtu ambaye hakurudhishwa na maamuzi ya Kamati ya Wilaya, anaweza kukata rufaa kwa waziri ndani ya siku 30 tangu tarehe uamuzi ulipofanyika na kwamba uamuzi wa waziri utakuwa wa mwisho.

Hata hivyo, iwapo muhusika hataridhishwa na uamuzi wa waziri, anaweza kuwasilisha maombi Mahakama Kuu.

Adhabu kwa atakayezikiuka kanuni hizo ni faini kuanzia Sh 500,000 hadi Sh milioni 12 au kifungo kuanzia miezi mitatu hadi miaka saba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles