26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kupima homa ya dengue sasa bure

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

SERIKALI imesema mpaka sasa watu 4,320 wameugua dengue na wanne kufariki dunia, huku ikitangaza kuanza kutoa bure huduma ya vipimo vya ugonjwa huo kwenye vituo vya afya vya umma.

Akitoa bungeni kauli ya Serikali juu ya ugonjwa huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema licha ya Serikali kununua vipimo moja kwa moja na kuviuza kwa bei nafuu, bado hospitali binafsi zimekuwa zikitoza fedha nyingi kwa kipimo ha ugonjwa huo.

Katika baadhi ya hospitali binafsi jijini Dar es Salaam,  mgonjwa anatozwa zaidi ya Sh 50,000 kupima ugonjwa huo, huku bima za afya zikiwa hazitumiki kwa sababu ni ugonjwa wa mlipuko.

Ummy pia jana aliliambia Bunge kuwa, wamenunua mashine kubwa sita za kupulizia dawa za kuua mbu wanaoeneza ugonwa huo.

 Alisema pia Serikali imeishanunua lita 60,000 za viuavidudu kutoka kwenye kiwanda cha uzalishaji kilichopo Kibaha.

“Lita 11,400 zimesambazwa kwenye halmashauri 5 za Mkoa wa Dar es salaam, lita 48,600 zinazosambazwa kwenye halmashauri za Geita lita 8,092, Kagera lita 12,308, Kigoma lita 7,616, Lindi lita 9,048 na Mtwara lita 11,536,”alisema.

Alisema lita zingine 36,000 zimeagizwa ambapo zitasambazwa kwenye mikoa yanye mlipuko wa ugonjwa huo ikiwemo, Pwani, Morogoro, Tanga na Singida.

Ummu alisema Serikali imeagiza mashine kubwa sita kwa ajili ya kupulizia mbu wapevu na mashine hizo zinatarajiwa kufika mwishoni Julai 2019.

“Dawa za kunyunyuzia nje lita 2,000 kwa ajili ya kuua mbu wapevu pia zimeagizwa ambazo zitasambaza katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Tanga,”amesema.

Alisema mpango mwingine ni kuunda kikosi kazi cha wataalamu cha kushughulikia udhibiti wa mbu wanaoeneza ugonjwa huo na malaria nchini.

Alisema kikosi kazi hicho kitaimarisha jitihada za kudhibiti  ndani ya Mikoa na Halmashauri zote nchini.

“Katika kuimarisha uchambuzi na matibabu ya ugonjwa wa homa ya dengue, bohari ya dawa imeshanunua vipimo 30,000 vya kupimia homa hiyo na awali wizara ilielekeza vituo vya umma kutoa huduma ya vipimo kwa uchangiaji wa kawaida katika matibabu.

“Kutengeneza na kusambaza mwongozo wa matibabu ya ugonjwa huu kwa ajili ya watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma.

“Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na magonjwa mengine,” alisema.

MAAMBUKIZI MAPYA YAMEPUNGUA

Ummy alisema takwimu za hali ya maambukizi ya ugonjwa huo zinaonesha maambukizi mapya yamepungua kutoka wagonjwa 2494 Mei 2019 hadi 813 Juni 19.

Aidha alisema changamoto ambazo wamekutana nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo ni gharama za kupimia ugonjwa huo.

“Ingawa Serikali kupitia bohari ya dawa imenunua vipimo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na kuviuza kwa bei nafuu ukilinganishwa gharama inayotozwa kutoka kwenye baadhi ya hospitali binafsi, bado wananchi wanashindwa kumudu gharama za uchangiaji matibabu ya ugonjwa huo,”alisema.

Alisema changamoto zingine ni ushirikishwaji wa jamii, pamoja na matibabu ya ugonjwa huo katika vituo vya kutolea huduma.

“Watoa huduma za afya kutokufuata kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa wa homa ya dengue.

DAR KINARA VIFO, MAAMBUKIZI

Katika hatua nyingine, Ummy alisema jumla ya wagonjwa 4,320 na vifo 4 vimetolewa taarifa huku Mkoa wa Dar es salaam ndio ukiwa kinara kwa kuwa wagonjwa wengi.

Alisema Mkoa wa Dar e salaam una wagonjwa 4,029 na vifo vitatu, Dodoma wagonjwa watatu na kifo kimoja, Tanga wagonjwa 207 kifo hakuna, Pwani 57 hakuna kifo, Morogoro 16 hakuna kifo, Arusha watatu hakuna kifo, Singida wawili hakuna kifo, na Kagera wawili hakuna kifo.

“Vifo vilivyotolewa taarifa ni kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, kimoja, Hindu Mandal 1 na Hospitali ya Regency wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles