23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

KUNA KILA SABABU KUWA NA MIKOPO YA NYUMBA

Na MWANDISHI WETU

HAKIKA kila Mtanzania anatamani kuwa na makazi bora na yenye mazingira mazuri kwa ustawi wa familia yake.

Pamoja na hitaji hilo kwa kila mtu, wengi wamekuwa wakikwama na kushindwa kufanya na mwisho wa siku hujikuta wakiishi maisha ya kupanga ambayo wakati mwingine huwa na manyanyaso ya kila aina kutoka kwa wenye nyumba.

Hata hivyo, kwa sasa hali imebadilika tofauti na miaka ya nyuma ambapo Watanzania wengi walikuwa wakijikuta maisha yao yote wamekuwa ni wapangaji hadi mwisho wa maisha yao.

Ni wazi suala la nyumba limekuwa na historia ndefu hapa nchini ambapo mwanzoni mwa miaka ya 1960, mikopo ya nyumba ilikuwa ikitolewa First Permanent Building Society iliyokuwa imesajiliwa Zambia, wakati huo Rhodesia Kaskazini.

Lakini pia ilikuwa na matawi katika nchi za Afrika Mashariki. Mwaka 1963 muundo wa matawi ya kampuni hiyo yaliyokuwa Afrika Mashariki, ulibadilishwa na kusababishwa kuundwa kwa First Permanent East Africa Ltd, ambapo wawekezaji kwenye kampuni hiyo walikuwa ni Serikali za nchi za Afrika Mashariki pamoja na Commonwealth Development Corporation.

Mwaka 1968, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Commonwealth Development Corporation iliunda Permanent Housing Finance Company (PHFC) Ltd ambayo ilirithi majukumu ya First Permanent East Africa Ltd.

Hata hivyo, mwaka 1972, Serikali ya Tanzania ilitaifisha  Permanent Housing Finance Company (PHFC) Ltd. baada ya kuonekana kama kampuni hiyo ilikuwa ililinda masilahi ya wageni zaidi. Kufuatia utaifishaji huo, Serikali ilianzisha Benki ya Nyumba Tanzania (Tanzania Housing Bank). Wawekezaji katika Benki ya Nyumba Tanzania walikuwa ni Serikali ya Tanzania- asilimia 46.5; Shirika la Bima la Taifa-asilimia 30.2 na National Provident Fund-asilimia 23.3.

Urejesheshaji wa mikopo ya nyumba kutoka THB  haukuwa wa kuridhisha. Inakadiriwa  kiwango cha ulipaji wa madeni kilikuwa asilimia 22 tu.

Hali hiyo ilisababisha kusuasua kwa huduma ya Benki hiyo na hatimaye kufilisika na kufungwa kabisa ilipofikia mwaka 1995. Baadhi ya wakosoaji wanadhani kuwa Serikali inapaswa kubeba sehemu ya lawama za kufilisika kwa THB kwa sababu ilirihusu watu mbalimbali kuchukua mikopo pasipo kujiridhisha na uwapo wao kurejesha deni husika. Baadhi ya wakopaji walichukua mikopo bila kuweka dhamana.

Katika kipindi cha kuvunjika kwa THB, sekta ya fedha ilikuwa ikiyumba. Hivyo hapakuwepo na chombo rasmi kilichochukua nafasi ya THB. Mfumo wa mikopo ya nyumba ulidumaa. Benki za biashara ambazo zote zilikuwa zikimilikiwa na Serikali hazikuwa zikitoa mikopo ya nyumba.

Kutokana na kupanda na kushuka kwa sekta ya nyumba hapa nchini, hivi karibuni Benki ya NMB Plc ilitangaza kampeni ya kutoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania yenye masharti nafuu.

Kupitia mfumo huo, benki hiyo imewataka wananchi wenye uhitaji wa kumiliki nyumba, kwenda katika matawi ya Benki ya NMB ili waweze kupatiwa mikopo nafuu ya kumiliki, kujenga na kumalizia ujenzi wa nyumba.

Akizungumza hivi karibuni katika maonyesho ya nyumba yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Tom Borghols, anasema benki hiyo inatoa mikopo hiyo hadi Sh milioni 700.

Anasema ni vigumu kuweka akiba kidogo kidogo kwa ajili ya ujenzi, hivyo benki hiyo imeamua kuwawezesha ili waweze kumiliki nyumba za ndoto zao.

“Wateja wa NMB na wasio wateja wetu waje kuchagua wanachohitaji, kati ya mkopo wa kununua nyumba iliyokwisha kujengwa, wa kumalizia ujenzi au mkopo wa mwenye nyumba kutumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli nyingine,” anasema  Borghols.

Anasema baada ya kuwakutanisha wadau wa ujenzi wa nyumba, jukumu alilonalo mteja ni kuchagua nyumba anayoitaka na benki hiyo itamlipia.

“Mikopo ya nyumba ni nafuu kwani riba yake ni asilimia 17 na huwa na masharti nafuu,” anasema Borghols.

Licha ya hali hiyo, anasema mkopo huo utakuwa ni wa aina tatu ambapo mtu anaweza kupata hadi Sh milioni 700, huku muda wa kurejesha ukiwa ni hadi miaka 15 na haina gharama za uendeshaji.

“Tumefikia uamuzi huu wa kutoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania kama ambavyo tunatambua umuhimu wa makazi.

“Mikopo yetu itakuwa na aina tatu ambapo aina ya kwanza ni ile inayohusisha mteja kununua nyumba yoyote anayoipenda iwe imejengwa na shirika au mtu anauza basi anakuja kwetu tunampa mkopo,” anasema Borghols.

Aina ya pili ni kwa mteja ambaye tayari amejenga nyumba na anahitaji pesa kwa ajili ya kufanya mambo mengine, basi akija kwetu tunampa mkopo iwapo tu nyumba hiyo itakuwa na hati.

“Mkopo wa tatu ni kumrahisishia mteja ambaye nyumba yake imefikia hatua ya linta, basi sisi tutakusaidia hadi hatua ya mwisho ambayo ni kupaua na kumalizia, kwani eneo hili limekuwa likiwashinda wengi na hivyo kumfanya mtu ajenge nyumba kwa muda mrefu,” anaeleza Borghols.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles