27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUMWELIMISHA MSICHANA KUTALIONGEZEA TAIFA MABILIONI YA DOLA

Na HAMISA MAGANGA,

UTAFITI uliofanyika hivi majuzi umebaini kuwa kumaliza tatizo la ndoa za utotoni kunaweza kusaidia nchi zinazoendelea kukuza uchumi kwa kuongeza mabilioni ya dola za Marekani.

Hii ni kwa kupunguza kasi ya ukuaji wa idadi ya watu waliotegemezi, kuboresha elimu na afya kwa wasichana wadogo na watoto wao, kupunguza bajeti za serikali na kuongeza uwezo wa wanawake kujiongezea kipato.

Ndoa za utotoni ni chanzo cha matatizo mbalimbali ya kijamii ikiwamo afya na kukosa elimu kwa wasichana wenyewe, ambapo tatizo hili pia huwakumba watoto wao na kizazi chao kwa ujumla.

Wakati idadi ya wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 wanaoolewa ikipungua katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni mpango wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kukomesha ndoa za utotoni, juhudi hizo zimekwama katika nchi nyingi za Kiafrika na Kusini mwa Asia.

Katika nchi hizo, ndoa za utotoni zimeshamiri. Mfano, nchini Niger asilimia 77 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 18 na 22 wameolewa licha ya kuwapo mikakati mingi ya serikali kuondoa hali hiyo.

 Je, kunahitajika mikakati mipya kumaliza tatizo?

Hali ilivyo duniani ni kwamba wasichana zaidi ya milioni 15 kila mwaka wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18.

Wanaharakati wanaopinga ndoa za utotoni wanasema Jumuiya ya Kimataifa inahitaji kutafuta njia mbadala za kumaliza tatizo hilo.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya wanawake milioni 700 duniani waliolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, zaidi ya theluthi moja waliolewa kabla ya miaka 15.

Iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, idadi ya ndoa za utotoni hasa katika nchi za Afrika zitaongezeka.

Hivyo, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa ifikapo mwaka 2050 wasichana wengi walio chini ya miaka 18 watakuwa majumbani bila shughuli zozote za kijamii.

Ukweli ni kwamba, uwekezaji katika kumaliza ndoa za utotoni bado unasumbua nchi nyingi duniani.

Ripoti mpya ya athari za kiuchumi zinazotokana na ndoa za utotoni iliyotolewa wiki iliyopita na Benki ya Dunia (WB) na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti juu ya Wanawake (ICRW) imebainisha hali hiyo.

Utafiti huo unatoa makadirio mapya ya kitaifa na kimataifa kwa kiasi cha fedha ambacho kinaweza kuokolewa iwapo tatizo hilo litakwisha.

“Ndoa za utotoni si tu zinaathiri matumaini na ndoto za wasichana, bali piahuzuia juhudi za kukomesha umasikini na kufikia ukuaji wa uchumi na usawa,” anasema Quentin Wodon ambaye ni Mkurugenzi wa Mradi wa WB na mwandishi mwenza wa ripoti hiyo. Anasema; “kumaliza tatizo hili si tu jambo la haki na kimaadili, bali pia linalenga suala zima la kukuza uchumi.”

Ripoti hiyo inatoa mfano kwamba nchini Niger faida inayoweza kupatikana kwa kupiga marufuku ndoa kwa watoto waliochini ya miaka 18 itafikia Dola za Marekani bilioni 1.7 ifikapo mwaka 2030; wakati nchini Ethiopia itakuwa Dola za Marekani bilioni 4.8 na karibu Dola za Marekani bilioni moja kwa upande wa Nepal.

Hiyo inatokana na utafiti kuonesha kuwa wasichana wanaoolewa wakiwa na umri wa miaka 13  kwa ujumla wake- wana uwezekano wa kuongeza asilimia 26 zaidi idadi ya watoto wanaozaa kulinganisha na wale wanaoolewa wakiwa na umri wa miaka 18 au zaidi na hivyo kuongeza idadi ya watu tegemezi na madeni makubwa kwa serikali.

Zaidi ya hayo, katika ngazi ya kimataifa, utafiti huo unabainisha kuwa iwapo ndoa za utotoni zingekoma mwaka 2015, uchumi wa dunia ungeongezeka kwa Dola za Marekani bilioni 566 ifikapo 2030; hii ni kutokana na nguvu kazi ambayo ingekuwapo.

Sasa basi, tafiti mbalimbali zinahitajika ili kubaini gharama zinazotokana na ndoa za utotoni katika nchi zilizoendelea kama Marekani, ambako pia wanakabiliwa na tatizo hili, pamoja na nchi masikini ambako hali ni tete zaidi.

Uchunguzi mpya wa ICRW na Utafiti wa WB, pia umebaini kuwa asilimia kubwa ya watoto walioolewa walilazimika kuacha masomo yao na hivyo kukatisha ndoto zao za kimaendeleo.

Ndoa za utotoni pia zinahusishwa na matukio ya vifo vya watoto chini ya miaka 5 na hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa husika.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa maboresho katika umiliki wa ardhi, ushiriki wa wanawake katika uamuzi, pamoja na kupunguza unyanyasaji wa kijinsia – mambo ambayo yanachangiwa kwa namna moja au nyingine na ndoa za utotoni, yanaweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

“Matokeo ya gharama za kiuchumi yatasaidia kuleta majadiliano kuhusu kumaliza ndoa za utotoni katika nchi zinazoendelea,” anasema Lakshmi Sundaram, Mkurugenzi Mtendaji wa Wasichana wasioolewa.

“Baadhi ya watu wanadhani kuwa ndoa za utotoni haziligharimu chochote taifa, lakini ripoti hii inaweka wazi ukubwa wa tatizo na mabilioni na trilioni za dola zinazopotea… hii inaweza kufungua majadiliano kwanini ni muhimu kwa wasichana kufanya uamuzi kuhusu maisha yao,”anasema.
Naye Mkurugenzi wa Mradi wa ICRW na mwandishi mwenza wa ripoti hiyo, Suzanne Petroni anasema:

“Umaskini, ukosefu wa usawa wa kijinsia, upatikanaji duni wa elimu bora, ukosefu wa huduma za afya ya uzazi, ukosefu wa fursa za ajira, kusaidia kuendeleza ndoa za utotoni na kuzaa kabla ya umri ni miongoni mwa mambo yanayochangia kudumaza uchumi.”

Hali ilivyo Tanzania

Suala la ndoa za utotoni Tanzania limesababisha idadi kubwa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kukatisha masomo yao.

Mwaka jana, Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International lilifanya utafiti na kugundua kuwa nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani machoni pa watu.

Liligundua kuwa takwimu zinazowahusu watoto wa kike ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na wakati mwingine mapendekezo ya tafiti zake hayafanyiwi utekelezaji.

Hapa nchini imeonekana hakuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazozipata mtoto wa kike kutokana na ndoa za utotoni, hivyo kusababisha thamani yake kushuka katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo ambapo madhara yake huonekana baadae akiwa mtu mzima.

Akitoa ripoti hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka shirika hilo kwa upande wa Tanzania, Jane Mrema anasema kiwango cha ndoa za utotoni kwa Tanznia kimefikia asilimia 36 ambacho ni kikubwa zaidi ya kiwango cha Dunia cha asilimia 34 na kwa hesabu za kimkoa ni asilimia 59 kwa kila mkoa.

Utafiti huo ulifanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na mashirika yasiyo ya kiserikali likiwamo Plan International, Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika linalohusiana na Utafiti na maendeleo ya Afya ya Wanawake (FORWARD) na Shirika la Utafiti juu ya Kupunguza Umasikini (REPOA).

Ripoti ya utafiti huo ulioitwa Visababishi na Madhara ya Ndoa za Utotoni Nchini Tanzania, ulionyesha kuwa umasikini ndio sababu kubwa ya kuwapo kwa ndoa za utotoni.

Baadhi ya mikoa ambayo wananchi walihojiwa wakati wa utafiti wamekubali kwa nguvu zote kuwa fedha zinazolipwa kwa ajili ya mahari ndizo zinazowasababisha kuwaoza watoto wao wakiwa bado wadogo.

Utafiti huo unaonesha Mkoa wa Mara wananchi asilimia 59 wanakubalina na majibu ya utafiti huo wakati jijini Dar es Salaam asilimia 56, Dodoma asilimia 53, Lindi asilimia 52 na Tabora asilimia 51.

Sababu nyingine ya ndoa za utotoni ni mtazamo wa tamaduni, mila na desturi baina ya jamii mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa kuolewa, unyago, ukeketaji pamoja na ngoma za asili zinazochangia watoto kuozwa mapema.

Tafiti hizo zinaonyesha kuwa maeneo ya vijijini asilimia 18 ya wanawake wamekeketwa wakati

mijini ni asilimia saba na mikoa inayoongoza na asilimia yake kwenye mabano ni Manyara (81) Dodoma (68), Arusha (55), Singida (43) na Mara (38).

Aidha, asilimia 24 ya waliohojiwa mkoani Shinyanga na asilimia 20 mkoani Tabora wamesema mikoa hiyo ina kiwango kikubwa cha ndoa za watoto walio na umri chini ya miaka 18.

Utafiti huo pia umegundua kuwa ukosefu wa elimu unasababisha wasichana kuingia kwenye ndoa wakiwa bado wadogo kiumri, hii inatokana na kushindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi ama kukatisha kabisa masomo yao kabla ya kuhitimu.

Kutokana na utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen anasema:

“Matokeo ya utafiti huo yanawapa mwongozo wa kujua sehemu zilizoathirika zaidi ili kuweka nguvu za kutosha na kufahamu namna mbalimbali za kutumia kuwafikia waathirika hao.”

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema anapinga kwa vitendo ndoa na mimba za utotoni kwa kuwa ni changamoto kwa maendeleo ya Tanzania.

“Tunataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hatutaweza kuwa na nchi yenye viwanda wakati watoto 36 katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 na watoto 27 wa Kitanzania wanapata mimba kabla ya umri huo, hili ni tatizo kubwa ambalo athari zake zitaonekana baadaye”anasema Ummy.

Katika kuhakikisha ndoa hizo zinakoma, ameanza kutumia marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge Juni 2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto wa shule ya msingi au sekondari kwa kuwa ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30 jela.

Pia, amewataka maafisa maendeleo ya jamii wa kila halmashauri kupita nyumba kwa nyumba kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo na kuwasilisha taarifa hizo sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo.

Viongozi wa dini nao wanasisitiza suala la kusomesha watoto wa kike ili waweze kufahamu mabaya na mazuri hatimaye wajiepushe na vitendo viovu vikiwamo vya kudanganywa na kuingia katika mapenzi wakiwa na umri mdogo.

Pia wanashauri kuangalia utaratibu wa kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili nao waje kuwa wanawake wanaoweza kuleta maendeleo katika taifa lao.

Hata hivyo, ili kulimaliza suala hili ni muhimu wazazi kuelimishwa juu ya madhara ya ndoa za utotoni.

Mimba za utotoni nazo juu

Takwimu zinaonesha kuwa tatizo la mimba za utotoni nchini limeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2016/17.

Sababu kubwa inatajwa kuwa ni ukosefu wa huduma pamoja na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 19.

Takwimu hizo zilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana- Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Venerose Mtenga wakati akizindua mradi wa ‘AMUA Innovation Accelerator, Sexual and Reproductive Health Challenge.’

Anasema: “Tatizo hili ni kubwa, mimba za utotoni bado changamoto hasa kwa vijana wa vijini kutokana kwamba hawajafikiwa na huduma au elimu ya afya ya uzazi.”

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk. Felix Bundala anasema tatizo la mimba za utotoni limechangia kuongezeka kwa vifo vya kina mama na watoto ambapo kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa kati ya vizazi 100,000 kina mama zaidi ya 550 hupoteza maisha wakati kati ya watoto wachanga 1,000 watoto 25 hufariki dunia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles