Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto amesema halmashauri hiyo imepokea Sh bilioni 5.1 za ujenzi wa vyumba vya madarasa 225 na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuboresha sekta ya elimu.
Fedha hizo ni sehemu ya mkopo wa Sh trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo Serikali imezielekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya Shule ya Sekondari Kinyerezi, Kumbilamoto amesema fedha hizo tayari zimeingizwa katika akaunti za shule mbalimbali za Jiji hilo huku Kinyerezi ikiingiziwa Sh milioni 160.
“Kwa kweli mtu asiyeijua historia ya Tanzania anaweza akaliona hili jambo ni dogo, madarasa 225 si jambo dogo kwahiyo tunamshukuru sana mama yetu. Niahidi tutazisimamia vizuri na tutahakikisha miradi yote inakamilia kwa wakati,” amesema Kumbilamoto.
Meya huyo pia amempongeza mkuu wa shule hiyo kwa kuboresha kiwango cha taaluma na kuahidi kushirikiana na wadau wengine kutatua changamoto zinazowakabili.
Aidha amewaasa wahitimu hao kutumia vema elimu waliyoipata kwa kujiendeleza na kuepuka kujihusisha na vitendo viovu kwenye jamii.
“Kumaliza kidato cha nne si mwisho wa maisha, usipofanikiwa usikate tamaa jitathmini una kipaji gani au una jambo gani ambalo mzazi anaweza kukuendeleza kimaisha. Sitegemei uende kukaba au kudanga,” amesema Kumbilamoto.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Kinyerezi, Mwalimu Veronica Mwaisaka, amesema kiwango cha taaluma shuleni hapo kimeongezeka ambapo kwa miaka mitatu wastani wa ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 52 hadi 67 mwaka 2020.
“Tuna mikakati ya kuhakikisha malengo ya kitaaluma yanafikiwa licha ya changamoto zilizopo, tunaomba wazazi kusisitiza utii na nidhamu kwa wanafunzi wetu, waje shuleni kila siku na wazazi wafike angalau mara moja kwa mwezi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi,” amesema Mwalimu Mwaisaka.
Hata hivyo amesema wana changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo 17 kwa wasichana na 18 kwa wavulana, nyumba 49 za walimu, umaliziaji maabara ya baiolojia, ukarabati wa maabara ya kemia pamoja na ujenzi wa uzio na ukumbi wa kufanyia shughuli mbalimbali.
Shule hiyo iliyoanza mwaka 2007 kwa sasa ina wanafunzi 1,419 na kati yao wasichana ni 776 na wavulana ni 643.
Katika mahafali hayo wanafunzi 456 walihitimu na kati yao wasichana ni 249 na wavulana ni 207.