KUMBE NI KUSOMA NA KUANDIKA TU, NIPENI JIMBO

0
499

Na RAMADHANI MASENGA

NIAJE wanangu? Mambo ni nini? Maisha matamu ama uhai nd’o mtamu? Ndiyo, kuna watu wanafaidi maisha na wegine tunafaidi uhai.

Ufaidi maisha una nini cha maana? Wenzako wanaita bilioni vijisenti wewe unatafuta pesa ya kodi. Maisha hayo unayafaidi katika engo gani sasa?

Wenzako wanapiga mtonyo kwenye makinikia wewe unaumiza kichwa kwa ajili ya pesa ya saluni ya kimanzi chako. Wewe endelea kufaidi hewa ya Mola tu kwa sababu ya uwepo wa uhai ndani yako.

 Ila wanangu mimi nimefikia uamuzi ili nitoke katika msoto wa maisha haya ya kiduwanzi. Miaka michache ijayo na mimi nataka kuingia mjengoni.

Ndiyo, mulemule mjengoni. Mle walipopozi kina Msukuma, Zitto, Lissu na Lusinde. Nami nataka niingie nipambane na magwiji, nigome, nipige kelele na mengineo. Au sio?

 Nakuhakikishia sishidwi kutuhumu watu wala kupiga kelele za ndiyoooo ama hapanaaaa. Hizo si nd’o shughuli muhimu za mbunge.

 Kwamba mbunge makini inabidi upige kelele za ndiyo ama ugome, utuhumu watu uzingue kisha ufungiwe vikao kadhaa.

Nasema najipanga kwa ajili ya kuibuka Bungeni neksti taimu. Vigezo na sifa ninazo. Mimi ni Mbongo, nimezaliwa na kusomea hapa hapa Bongo. Kigezo cha elimu nimetimiza. Najua kusoma na kuandika.

Nani atanibania hapo? Hakuna. Laifu ni suala la mbinu na mafekeche tu, kwani waliofika mjengoni walitimbaje na mimi mchizi wenu nishindwe?

Nami nikifika nitawatetea wana. Nitapeleka hoja za kutetea ganja, gongo, mirungi na kubeti. Kwa umakini kabisa, nitaomba serikali ikubali kuanzisha somo la kubeti shuleni, nitaomba bangi na mirungi iwe halali kama sigara. Wana si mtanipa kura?

 Haina kumbwela msidhani nimedata. Hii hoja kwani nikiipeleka mjengoni nitakuwa wa kwanza? Kwani hakuna mbunge, tena aliyepigiwa kura na watu aina zote, wakiwemo viongozi wa dini, wazee na washkaji wasomi, aliyetetea ganja na mirungi?

Mbunge wa namna hiyo hakuna? Sasa mimi nitashangaza vipi? Moja kati ya fursa adimu ni kuwa mbunge aisee. Zamani ubunge ilihitaji uwe na fikra za kizee, uwaze maendeleo tu.

Ubunge ulikuwa hauna kiki wala umaarufu wa Kibongo Fleva ila sasa mambo swafi kabisa. Ubunge una kiki, wabunge wanahusishwa na maduu, wabunge wanakesha klabu. Maisha yanataka nini sasa?

Majita nimejipanga na mimi kukanyaga mjengoni. Nimejipanga kusukuma V8 pamoja na kuvimba katika mijadala ya bajeti za wizara na kipindi cha maswali na majibu. Natosha sitoshi? Natosha.

Haina kuremba, nakamata fursa natembea nayo. Laifu ni kupanga na kuchagua. Mwanenu nimechagua kuingia kwenye lile jengo jeupe, nitatetea masuala yote muhimu ya huku maskani.

Nitavipigania vigodoro, Singeli na vijiwe vyote vya Pool Table. Kama ikitokea nitagombea kwa chama tawala basi nitaunga mkono kila hoja bila kupinga.

Ikiwa upinzani pia nitapinga kila kitu bila bila hoja. Wana jipangeni mnipe kura niwatetee. Waliotia maguu pale mjengoni si tunaona na mimi nipeni kura nikaungane na wana tuliamshe dude. Watu oyooo.

Kama tunavyoungana mkono katika misheni nyingine na katika hili wanangu tupigane tafu. Niungeni mkono baharia niingie Bungeni. Nipeni jimbo wana. Nasubiri kipindi cha kuchukua fomu tu. Tutakutana kwenye kampeni wanangu ila chondechonde, msinitose.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here