29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

KUMBE DIDA ANATAKA KUWA MSHAMBULIAJI!

Na ZAINAB IDDY


LICHA ya Yanga kuwa na walinda mlango watatu ambao ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Ally Mustapher ‘Barthez’ na Beno Kakolanya, lakini hakuna anayeweza kupewa asilimia 100 kuhimili mikikimikiki ya mashindano ya ndani au ile ya nje na hii inatokana na baadhi yao kuhisi hawapo sehemu sahihi kwenye namba wanazocheza huku wengine wakikosa bahati ndani ya timu hiyo.

Ukimwangalia Kakolanya ni kama hana bahati ndani ya Yanga, kwani toka alipojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu mechi alizodaka hazizidi tano na hiyo inatokana na kuwa majeruhi mara kwa mara, kwa upande wa Barthez hivi sasa anaonekana ni sawa na duka kila mmoja anaweza kununua kile anachotaka na hilo lilianza kutafsiriwa baada ya mchezo wao na Simba waliotoka sare ya 1-1 mzunguko wa kwanza.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa hao wawili, Dida ndiye anayeaminiwa ndani ya timu hiyo hivi sasa kuanzia mashabiki, viongozi hadi benchi la ufundi, lakini hivi karibuni ameanza kuonyesha hayupo sehemu sahihi katika namba anayocheza.

Ingawa mabeki wana jukumu la kuhakikisha hakuna adui anayeingia kwenye ngome yao, lakini kipa naye ana majukumu mawili makuu ambayo ni kulinda lango lake na kuipanga safu yake ya ulinzi ambayo kwa Dida ameshindwa kuyatekeleza.

Ni wazi Dida ameshindwa kuthamini kuaminiwa kwake na benchi la ufundi la Yanga pamoja na lile la Taifa Stars, wanaompa nafasi na kuwaacha makipa wengine lukuki wakihaha kuisaka nafasi hiyo.

Dida anapata nafasi kwenye mechi za Ligi Kuu, FA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano ya kimataifa ya timu yake na hata ile ya Taifa Stars, lakini kote huko ule mzaha na masihara ya kushindwa kutimiza majukumu yake amekuwa akiendelea kuufanya.

Ameshindwa kuthamini heshima anayopewa na ndio maana mara nyingi anakubali kufungwa mabao ya kizembe kama lile alilofunga na Laudit Mavugo kwenye mechi ya kirafiki baina ya Stars na Burundi Jumanne iliyopita, mchezo uliomalizika kwa Stars kushinda 2-1.

Mbali na mechi hiyo, ukirudi nyuma kidogo kwenye Ligi Kuu upo ule mchezo baina yao na Simba mzunguko wa kwanza, Mavugo alifunga bao kama hilo alilofunga Jumanne iliyopita akiwa na Burundi, mwingine ni ule dhidi ya Mbeya City mkoani Mbeya, Stand United, kwenye mashindano ya Mapinduzi pamoja na mechi za Ligi ya Mabingwa  Afrika, mabao mengi yamechangiwa na Dida kushindwa kutimiza majukumu yake.

Tatizo kubwa la Dida ni kushindwa kukaa langoni mwake, huku akiwa pia hayupo makini kuipanga safu yake ya ulinzi hivyo kutoa mwanya kwa wapinzani kufanya kile wanachokitaka.

Si mara moja Dida amekuwa akitoka nje ya 18 mfano wa beki au straika, jambo linalomgharimu mara kwa mara, hii inadhihirisha kuwa kipa huyo anahitaji kupewa majukumu mapya nje ya nafasi yake.

Imeandikwa kila mtu anafanya kazi kulingana na nafasi aliyopo, iweje  afanye kazi za wengine? Hili ni jambo la kushangaza sawa makipa wengi wanatoka, lakini Dida hawezi kutoka na kurudi kwa wakati langoni mwake na ndio maana wenye mapungufu kama Dida mara nyingi huamua kubaki eneo lao tu.

Kwanini usijifunze kwa mdogo wako Aishi Manula, anayeidakia Azam FC ambaye kwa sasa si vibaya kumwita ‘Tanzania One’, kutokana na uwezo mkubwa alionao pamoja na kujua mipaka, sheria na maadili ya nafasi aliyopo.

Kitendo kinachofanywa na Dida ni kuwanyima Wanayanga furaha kipindi ambacho si kizuri kwao kutokana na kuwa tayari wameuweka rehani ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya watani zao Simba kupania kufuta kilio walichonacho cha kukosa taji kwa misimu minne iliyopita.

Kiroho safi ina hakika kama Oscar Joshua anayecheza beki ya kushoto Yanga kocha wake George Lwandamina aliweza kumpanga mshambuliaji, ni wazi hata Dida anataka kupangwa nafasi ya mshambuliaji.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles