Na KOKU DAVID
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mlipaa kodi anafahamu maana ya kodi na umuhimu wa kulipa kodi.
Baadhi ya watu wamekuwa wakibuni njia mbalimbali za kukwepa kodi hali ambayo inasababisha serikali kukosa mapato yake kwa mujibu wa sheria.
Hali hiyo inatokana na watu kukosa uzalendo kwa nchi yao au yawezekana inatokana na kutokujua umuhimu wa kulipa kodi.
Hata hivyo mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha kila mmoja anaelewa umuhimu wa kodi ili waweze kulipa kwa hiyari bila shuruti kama ambavyo sheria inawataka kufanya.
Kila mtu mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi ambayo ndiyo itakayoiwezeshe serikali kutekeleza majukumu yake kwa wananchi wake.
Pia mikakati mbalimbali imewekwa ili kuhakikisha kodi zinakusanywa ikiwa ni pamoja na kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi na kuwachukulia hatua wale wote wanaokwepa kulipa kodi.
TRA imekuwa ikifanya doria mbalimbali katika mipaka isiyo rasmi, bandari bubu na sehemu ambazo zinaweza kutumika kama vichochoro vya kukwepea kodi ili kuweza kuwakamata wanaovunja sheria kwa kukwepa kulipa kodi.
Kwa upande wa wasanii, TRA kwa kushirikiana na kampuni ya Yono Auction Mart pamoja na Jeshi la Polisi imekuwa ikifanya ukaguzi wa stempu za kodi katika kazi za wasanii ili kubaini wakwepaji wa kodi.
Mwanzoni wa mwaka jana, mamlaka hiyo iliweza kukamata CD na DVD za muziki na Filamu zipatazo 7,780 ambazo hazikuwa na stempu za kodi kutoka kwa wasambazaji mbalimbali jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Pia mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata baadhi ya CD na DVD zikiwa zimedurufiwa pamoja na stempu za kodi kinyume cha sheria.
Zoezi hilo la ukamataji wakwepa kodi kupitia kazi za wasanii lilifanyika Februari 26 mwaka jana katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambapo wasambazaji wa kazi za wasanii walibainika kuvunja wa sheria kwa kukwepa kulipaji kodi.
Sambamba na hilo mamlaka hiyo ilibaini udanganyifu kutoka kwa baadhi ya wasambazaji wa kazi hizo za wasanii kwa kutumia stempu za kodi kinyume na sheria.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo anasema kuwa baadhi ya wasambazaji huweka CD au DVD mbili kwenye kasha moja huku nakala moja ya CD/DVD ikiwa imebandikwa stempu halali ya kodi na nyingine ikiwa haina stempu jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Anasema pia waliweza kukamata kazi zinazoingizwa nchini zikitokea nje ya nchi zikiwa hazina stempu za kodi jambo ambalo ni kinyume cha sheria na pia hupoteza mapato ya nchi kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo mamlaka ya mapato imekuwa ikitoa wito kwa wasambazaji wa kazi za wasanii kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kutumia stempu za kodi kwa mijibu wa sheria.
Pia ni sharti wahusika wanaoingiza kazi za wasanii kutoka nje ya nchi wapate vibali kutoka Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili wapate vibali vya kubandika stempu za kodi kwenye kazi hizo na si vinginevyo.