23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

KUKUMBATIANA; MOJA YA BIASHARA ZA KUSHANGAZA ZINAZOFANYWA DUNIANI

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA


PENGINE unafikiria kuanzisha biashara au huduma za kibiashara, lakini unahofu kuchekwa kwa wazo lako lisilo la kawaida au linaloonekana la biashara dhalili.

Lakini fahamu hauko peke yako, kuna wajasiliamali wengi walioweza kufanikiwa kwa mawazo ya biashara yasiyo ya kawaida, mengine yakionekana kama kioja.

Ukiachana na zile biashara zinazoweza kuwa za kawaida lakini wengi wetu tunazidharau kwa kuziona ni dhalili au za watu wa hali ya chini, kuna zile zisizo za kawaida kabisa.

Naam, unaweza kuziita tofauti kabisa, za kushangaza, au ambazo hujawahi kuzisikia.

Lakini haiondoi ukweli huu-ni biashara, ujasiliamali au huduma za kibiashara ambazo zipo katika dunia hii yenye kila aina ya vituko na kutokana na upekee wake zinalipa!

Katika safu yako hii uipendayo tunakuletea baadhi ya biashara hizo zisizo za kawaida, ambazo huwezi kuamini kama zipo.

 

Kulipia makazi mbinguni

Ni ajabu na kweli, wajasiliamali Nate Davis na Edgar Kim wakazi wa Seattle nchini Marekani wanauza mahala pa kuishi mbinguni kupitia mtandao wao wa Reserve A Spot In Heaven. Wanasema kuna nafasi chache mbinguni, fanya hima kujiwekea mahali kwa ajili yako au wapendwa wako mbinguni.:

“Iwapo unaweza kulipia chumba katika hoteli mahala unakopanga kwenda iwe katika mji au nchi nyingine kwanini usifanye hivyo mbinguni?

Iwapo mtu hutoenda mbinguni, kampuni hiyo inadai itarudisha fedha, ijapokuwa namna fedha zitakavyorudishwa ilhali mteja atakuwa ameshafariki dunia, kampuni hiyo haijaweka hilo wazi.

‘Tunaahidi kurudisha asilimia 100 ya fedha zako iwapo kwa sababu yoyote ile hutofika mbinguni, tutakurudishia fedha zako zote bila maswali yoyote. Lakini usihofu, tuna imani utafika mbinguni.

 

Biashara ya viwanja mwezini

Wengi wetu wanafahamu mwanaanga Mmarekani, Neil Armstrong: mtu wa kwanza kukanyaga mwezini. Mara tu aliposhuka kutoka chombo cha anga za juu cha Apollo 11 na kutua katika uso wa mwezi alizungumza maneno haya ya kukumbukwa, “Hiyo ni hatua moja ndogo kwa mwanadamu, mapinduzi makubwa kwa ubinadamu.” Kwa maneno mengine unaweza kusema kuifanya mwezi kuwa koloni la dunia ni hatua inayofuata.

Ukoloni huo wa mwanadamu katika mwezi unaweza usitokee nyakati zetu, lakini kampuni kama Lunar Registry imekuwa ikiuza vipande vya ardhi mwezini kwa watu walio na ndoto za kuishi huko. Mfanyabiashara mwingine Dennis Hope anayedai kuumiliki mwezi ametengeneza zaidi ya dola milioni 10 sawa na zaidi ya Sh bilioni 25 kuuza vipande. Miongoni mwa wateja wake milioni sita aliowauzuia ni pamoja na wacheza filamu nyota wa Hollywood, Tom Cruise, Tom Hanks na Clint Eastwood na wa Star Wars, George Lucas.

Pia wapo wanasiasa kama marais wa zamani Marekani, Ronald Reagan (marehemu), Jimmy Carter na George Bush mtoto.

 

Masaji ya kofi usoni

Ni huduma isiyo ya kawaida, lakini unaweza kulipia kwa kupigwa kofi usoni kwa dakika kadhaa ili kuimarisha ngozi yako na kuondoa mikunjo.

Hata hivyo, matokeo tarajiwa ya huduma hii si ya kudumu na hivyo unaweza kujikuta ukirudi tena na tena kupokea huduma hii vichapo hivyo vya uso.

Aina hii ya masaji, inayofahamika pia kama ngumi ya uso ni maarufu zaidi nchini Thailand. Nchini Marekani kuna eneo moja tu inakopatikana baada ya kupewa leseni ya kuiendesha kule San Francisco. Kampuni hii ya Marekani inaonya wateja kujiepusha na matapeli wanaodai kutoa huduma hiyo yasije yakawapata, isipokuwa kwao tu walio na wataalamu wa ukweli wa ina hiyo ya huduma ya ‘hekima ya Kithai.’

 

Ukodishaji mbuzi

Iwapo una ardhi au shamba lenye majani mengi, ukataka yakatwe sawa sawa. Mbuzi wanaonekana kuiweza kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi. Kwa sababu hiyo, Ulaya na Marekani ziko kampuni zinazotoa huduma ya kukodisha mbuzi kwa ajili ya kazi hiyo. Katika hilo mmiliki wa mbuzi huua ndege wawili kwa jiwe moja; si tu anapata fedha kwa kukodisha mbuzi hao bali pia haingii gharama kununua chakula kwa mifugo yake hiyo.

 

Viazi badala ya barua

Kampuni ya Samwise nchini Marekani imebuni aina ya biashara ya kutuma ujumbe wa posta kwa kutumia viazi. Chakula hiki badala ya kuliwa kinatumika mahala pa nyaraka kama barua. Huandikwa ujumbe unaokusudiwa kwenye kiazi na kutuma vifurushi kwa njia ya posta ua magali maalumu kwenda kwa mhusika.

 

Huduma ya kukumbatiana

Nchini Marekani, Canada, Australia na Ulaya kuna huduma za kukumbatiana kwa kuanzia mtu mmoja hadi kundi la watu ambazo hufahamika kama tafrija ya kukumbatiana, ambazo hazihusishi kitendo cha ngono. Inaelezwa ‘tafrija’ hizi za kukumbatiana kwa staili tofauti tofauti ikiwamo kuviringishana iwe sakafuni, kitandani, kitini au popote pale pafaapo si tu hufariji, kuliwaza na kuleta afya ya akili bali pia hufundisha stadi mbalimbali za uhusiano.

 

Masaji ya nyoka

Kuna njia na mbinu nyingi linapokuja utoaji wa huduma za masaji, ambazo kwa kawaida hufanywa na wanadamu. Lakini inawezekana kabisa kazi hiyo kufanywa na kitu kingine, moja wapo ni matumzi ya nyoka kusaidia kutoa huduma hizo na hivyo kuondoa shinikizo na kuchangamsha misuli na viungo.

 

Usafi na wadada watupu

Kuna kampuni nyingi ambazo zinatoa huduma za usafi katika nyumba au ofisi kwa kutumia wadada watupu kwa kuchaji hadi dola 100 sawa na Sh 230,000 kwa saa katika mataifa ya magharibi na hata Asia.

Kwa mfano, ukiishi katika mji wa Texas-unaweza kupata huduma za aina hiyo kutoka kampuni kama Lubbock Fantasy Maid Service, kwa dola 100 kwa saa. Melissa Borrett, ambaye ameianzisha kampuni hiyo atasafisha nyumba yako akiwa amevaa kitopu au kichupi tu ama mtupu kabisa. Ukiongeza dola 50 utaletewa wadada wawili zaidi wakati huo huo kwa huduma hii ya usafi.

Licha ya kutoa huduma hiyo ya usafi, mabinti wakiwa watupu, kwa mujibu wa tovuti za kampuni hiyo si biashara ya ngono na haihimizi vitendo vya aina hiyo baina ya wateja na wafanyakazi.

 

Samani mbaya

Katika mtandao wa UglyFurnitures.com kampuni ya fenisha hujinadi kuuza samani mbaya kabisa duniani. Wajasiliamali hawa nchini Marekani wanatengeneza samani mbalimbali za nyumbani na maofisini wakidai ni mbaya mno, lakini ukweli ukienda kununua utaondoka samani za aina yake usizoweza kuziona pengine popote pale. Kwa maana wanatengeneza samani nzuri za aina yake kinyume na madai kuwa ni mbaya.

 

Kampuni inayokodisha vibibi

Rent-a-Grandma ni kampuni iliyopo Texas na Virginia nchini Marekani, ambayo inatoa huduma za kulea watoto kwa kukodisha wanawake wenye umri mkubwa kuanzia miaka 50. Kampuni hiyo huajiri na kukodisha wanawake hao wenye uzoefu wa kutunza watoto majumbani au katika vituo vya kuelelea watoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles