23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

KUKOSEKANA KWA MIKOPO KULIVYOKIMBIZA WANAFUNZI VYUONI

01

Na FARAJA MASINDE,


 

ELIMU ya Tanzania bado inaelezwa kuwa na safari ndefu katika kuhakikisha kuwa inafikia kwenye hatua ya mafanikio kama nchi kujivunia wasomi wake wa vyuo vya ndani katika kufanya mambo mbalimbali ya kujenga Taifa.

Hii inatokana na kuwapo kwa msululu wa changamoto ambazo zimekuwa zikiutafuna mfumo wa elimu hii kwa kipindi kirefu sasa, ambao mara kwa mara umekuwa ukija na sura mpya kulingana na uongozi wa juu wa elimu unavyowekeza.

Tumeshuhudiwa kuwapo kwa hali ya sintofahamu juu ya seriakali na hatima ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Wapo waliofanikiwa kupata mikopo hiyo huku wengine wakikosa kabisa. Changamoto kubwa kwasasa iko kwa wale waliokosa ambapo kundi kubwa la wanafunzi kutoka kwenye vyuo vikuu mbalimbali wamelazimika kuhairisha mwaka wao wa masomo kwa maana ya kuacha masomo.

Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na uwezo duni wa familia za wanafunzi hao baada ya watu waliowaahidi kuwasomesha mara baada ya kukosa mkopo wa serikali kushindwa kufanya hivyo kulingana na hali ngumu ya kiuchumi.

Wakufunzi katika vyuo mbalimbali nchini wanabainisha kuwa wimbi la wanafunzi waliokosa mikopo ambao tayari walikuwa wameshasajiliwa na vyuo kuacha masomo limekuwa kubwa.

Sababu za wanafunzi hao kuacha masomo zimeelezwa kuwa ni pamoja na kushindwa kumudu gharama za masomo kwani awali walitarajia kupata mkopo kutoka serikalini lakini imekuwa kinyume na matarajio yao.

Wasomi mbalimbali wameelezea hali hiyo huku wakitoa rai kwa serikali juu ya hatua hiyo inayoendelea kuchukuliwa na wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni kuacha masomo.

Profesa Mwesigwa Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tawi la Dar es Salaam anasema hili ni tatizo kubwa na kwamba hakuna budi kuhakikisha linatatuliwa kwa serikali kuweka mifumo sahihi.

“Hali ya mikopo na elimu ya juu kwa ujumla ni jambo ambalo bado linakanganya. Serikali iliwahi kuahidi kuwa mikopo itatolewa kwa watoto wote wa masikini  lakini hali ni tofauti.

“Inaonekana kuna ubabaishaji wa namna fulani ambao umetokea na serikali haitaki kuliweka jambo hili wazi …

“Elimu yetu na sera ya mikopo ni vitu vya kufikiriwa upya. Orodha ya waliokopa ni ndefu na masharti yanayotumika kutoa mikopo hiyo si sahihi,” anasema.

Anasema suala la elimu linapaswa kupewa uzito wa hali ya juu, si kama ilivyo sasa.

Anasema suala si mikopo bali jambo la kujiuliza ni tunataka kuwekeza kiasi gani katika elimu iliyobora na ile ya juu kwa watoto wetu?

Profesa Baregu anasema bado kunahitajika mjadala mkubwa zaidi ili kujadili elimu ya Tanzania kwa ujumla kwani tunapoelekea wanasiasa wanaweza kuiua.

“Binafsi nimekuwa nikifanya utafiti juu ya suala hili kwa muda mrefu nikabaini kuwa chama kilichopo madarakani kinaona kama kuwekeza kwenye elimu kunahatarisha uwezekano mkubwa wa wao kuendelea kuongoza nchi.

“Hii ni kwa sababu kuwaongoza wasomi ni kazi ngumu kuliko kuwaongoza watu wasioelimika. Wasomi hawawezi kupelekwa bora liende, lakini kama mtu hajaelimika ni wazi kuwa atakuwa na hofu hata ya kuhoji haki zake za msingi.

“Suala hili tumekuwa tukilichukulia kama linatokana na matatizo ya kiutaalamu au kiufundi, hii si kweli. Ninachoweza kusema ni kwamba imeuawa na wanasiasa,” anasema.

Anasema kuwa chuo chake ni miongoni mwa vyuo vilivyokumbwa na changamoto hiyo ya wanafunzi kuacha masomo baada ya kushindwa kumudu gharama.

Anasema kuwa Serikali hainabudi kuweka bayana ni utaratibu gani waliouandaa kwa ajili ya hawa vijana kuweza kuendelea na masomo. “Kama hakuna uwezekano wa kuwasaidia kuendelea na elimu basi ibainike mapema kwani wanahaha tu bila ya kujua hatma ya maisha yao kielimu,” anassema Profesa Beregu.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha, Iringa (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala anasema serikali hainabudi kutafuta mbinu za kutatua changamoto hii kwa kutoa fursa kwa wanafunzi wengi ikiwezekana wote waweze kupata elimu ya juu.

“Serikali haina sababu za msingi za kuzuia mikopo kwa wanafunzi wenye sifa, hali iliyopo vyuoni ni mbaya, wanafunzi hawana fedha za kujiendeleza kielimu.

“Karibu wanafunzi wote ambao tuliwasajili kwa ajili ya kuanza mwaka wa kwanza wa masomo wamelazimika kuacha kutokana na kushindwa kumudu gharama.

“Suala hili kamwe si la kuendelea kulifumbia macho… haiwezekani mtoto asome kwa bidii miaka yote akiwa shuleni halafu ashindwe kuendelea na chuo kikuu kisa hana fedha,” anasema Profesa Mpangala.

Pamoja na vyuo hivyo, chuo kingine kilichoathirika na mikopo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Duce, ambacho pia kimepoteza adadi kubwa ya wanafunzi.

 Wanafunzi

Chuo Kikuu cha Ardhi nacho ni ni miongoni mwa vilivyokumbwa na kadhia hii, wanaojaribu kupambana na masomo ni wale waliopata angalau asilimia 20 ya mkopo na wale wanaotoka kwenye familia zenye uwezo.

“Kuna watu ulikuwa unawaangalia unasema kabisa huyu bodi ya mikopo wamemuonea kumnyima mkopo, lakini kuna baadhi ya wanafunzi ambao ukiwaona unaona kabisa kwamba hata wangekosa mkopo wangeendelea tu.

“Nafikiri kuna haja ya bodi kubadili utaratibu wa utoaji mikopo. Ni vema bodi ikazingatia makundi maalumu kama yatima, walemavu na watu wasiokuwa na uwezo,” anasema Veronica Haule ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika fani ya Geomatis, Chuo Kikuu cha Ardhi.

Mmoja wa wanafunzi ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, anasema awali alikuwa amejiunga na Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu DUCE, fani ya elimu, amelazimika kuhairisha mwaka wake wa masomo baada ya kukosa mkopo.

“Hili jambo linasikitisha mno,  wakati mwingine unasema ni bora hata nisingehangaika kusoma kwani ndoto zangu zote zimeyeyuka.

“Familia yangu haiwezi kumudu gharama za kunisomesha, wakati najiunga na chuo nilijua ningepata mkopo lakini mambo yamekuwa tofauti.

“Nilijaribu kuomba misaada kwa ndugu na jamaa lakini hakuna aliyekuwa tayari kunisaidia,” anasema Julias.

 Wazazi

Baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamekosa mikopo wanaitupia lawama serikali kwa kusema kuwa haitendi haki.

“Nimebaki kusikitika tu na mwanangu hapa ambaye alikuwa amepangiwa Chuo Kikuu cha Dodoma, mwenyewe siwezi kumudu kumsomesha, hivyo nimemshauri tu akae nyumbani tuangalie kama itawezekana mwakani ndio aendelee na masomo,” anasema Mary Mwita.

 Bodi ya Mikopo

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Cosmas Mwasiobwa anasema kuwa kwa mwaka huu wamefanikiwa kufikia malengo waliyokuwa wamejiwekea.

“Serikali ilikuwa imeweka lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,400 ambapo idadi hiyo imefikiwa kulinga na kiwango ambacho kilikuwa kimepangwa.

“Kila mwaka tutatoa mikopo kulingana na mapato yetu,”anasema Mwasobwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles