31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

KUKOSA ABIRIA KUSIWAFANYE MUWE WAHALIFU

 

Na FARAJA MASINDE

KAMA wewe ni mfuatiliaji wa habari hizi zinazowahusu waendesha pikipiki maarufu bodaboda, ni wazi kuwa utakuwa umesikia juu ya kuwapo kwa vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu hawa.

Hatari hii inaelezwa kuwapo maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam na kwingineko ambapo baadhi ya vijana wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia bodaboda kufanya uporaji.

Hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara nchini ambapo waendesha bodaboda hupora mikoba ya waenda kwa miguu, kuwapora abiria wao na kuvamia benki kupora fedha.

Maeneo yanayopendwa zaidi na majambazi hao ni pamoja na Mikocheni, Kijitonyama, fukwe za Coco na mengine ambayo hayana msongamano mkubwa wa watu.

Kwa wale akinadada ambao hupenda kutembea huku wakiwa wameshikilia simu zao mkononi ndio waathirika wakubwa.

Vijana hawa wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia pikipiki aina ya boxer ambazo zinaelezwa kuwa na kasi zaidi barabarani katika kufanikisha uhalifu wao.

Kinachofanyika pindi wanapomkuta dada njiani akiwa anatembea peke yake huku amebeba mkoba au simu, humsogelea na pikipiki ambapo dada kwa kuhofia usalama wake mawazo huamia kwenye pikipiki. Kwa kuwa dada akili yake uhamia kwenye bodaboda, hapo ndipo hujikuta akiporwa kwa urahisi.

Hali ngumu ya maisha inatajwa kuwa ni sababu ya vijana wengi wanaoendesha bodaboda kuhamia kwenye kazi ya kupora watu mitaani na kwenye taasisi za fedha.

Ukipita kwenye vituo vingi vya bodaboda, wengi wao hulalamika wakisema maisha yamekuwa magumu wateja nao hakuna, ndio maana wameamua kugeukia kazi nyingine zinazoweza kuwaongezea kipato kwa haraka. Naomba niwashauri kuachana na wizi huu kwani unaweza kuwaharibia kabisa maisha yenu badala ya kuyaboresha.

Licha ya kwamba wengine mnajitetea kuwa wanaofanya hivyo si ninyi bali ni watu wengine tofauti, ni vema kutoa taarifa kwenye vituo vya polisi kuliko kuacha uhalifu huu ukiendelea.

Bila kuwafichua wahalifu, itafikia hatua mtapata wakati mgumu katika kazi zenu. Watu wataogopa kupanda bodaboda kwa kuhofia kuporwa mali zao na matokeo yake biashara itazidi kuwa ngumu kwa upande wenu.

Jambo la muhimu ni kufahamu kuwa maisha magumu yapo kwa kila mtu, hivyo jambo la kuzingatia ni kubuni njia mbadala ya kuwavutia wateja.

Jitahidini kutafuta kipato kwa njia zilizo halali, kama bodaboda hailipi tafuteni biashara nyingine ambayo mnadhani inaweza kuwakwamua na hali ngumu mliyonayo sasa.

Biashara zipo nyingi, msing’ang’anie wote kwenye bodaboda kwani abiria siku hizi ni wachache kuliko idadi ya pikipiki. Kila kijana anayefeli maisha anakimbilia huko, ni lazima biashara itakuwa ngumu. Wengine hata kuendesha vizuri bado wanataka kuingia mjini kusaka abiria, matokeo yake mnapata ajali kila kukicha. Kama huko mliko hakulipi geukieni kwingine si kuanza kuiba mali za wateja wenu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles