Na Fadhili Paulo
KUENDELEA kutegemea mazoezi au kufunga kula au kupunguza kula kunaweza kusiwe msaada kwa baadhi ya watu wanaotaka kupunguza uzito na unene.
Zipo mbinu chache unazoweza kuzitumia na ukaweza kudhibiti uzito wako.
Zifuatazo ni mbinu 11 za kupunguza uzito na unene bila mazoezi wala kufunga kula
Â
Kula chakula taratibu
Ubongo wako unahitaji muda wa kutosha kushughulika na tendo la kutafuna na kumeza.
Kula taratibu kunahusiana moja kwa moja na kuweza kula chakula kichache na kujisikia kushiba.
Muda unaotumia kumaliza chakula chako unaweza pia kuathiri uzito wako.
Utafiti unaonyesha watu wanaokula kwa haraka haraka huwa na uzito mkubwa ukilinganisha na wale wanaokula pole pole.
Â
Tumia sahani ndogo kwa vyakula visivyo na afya
Kama itakutokea ukataka kula vyakula visivyo na afya ambavyo huongeza uzito kirahisi, basi jaribu kutumia sahani ndogo na si ile unayotumia kila siku. Mara nyingi watu wengi chakula kinapoisha kwenye sahani hujiona tayari inatosha.
Sahani ndogo inakifanya chakula kionekane kingi hivyo huridhisha macho na njaa yako kwa ujumla.
Â
Kula zaidi protini
Vyakula vyenye protini vina matokeo makubwa upande wa njaa. Vyakula hivi vinakufanya ujisikie kushiba kwa kipindi kirefu kama ilivyo kwa vyakula vyenye nyuzinyuzi.
Kama kwa sasa asubuhi unakula chakula cha asubuhi chenye wanga mwingi kama mikate, chapati au maandazi au hata wali basi unaweza kuhamia kula vyakula vyenye protini nyingi kama vile mayai.
Vyakula vingine vyenye protini nyingi ni pamoja na korosho, samaki, mtindi, parachichi, karanga, mbegu za maboga na vinginevyo.
Â
Weka mbali vyakula visivyo na afya
Vyakula vile unavyofahamu kwa hakika kwamba huongeza uzito na unene kirahisi, ni vema ukavihifadhi mbali na macho yako hivyo hutashawishika kutaka kuvila.
Kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi
Vyakula vyenye nyuzinyuzi (faiba) vinao uwezo wa kukufanya ujisikie umeshiba kwa muda mrefu.
Vyakula hivi mara nyingi hutokana na mimea hasa maharagwe, machungwa, parachichi, mbegu za maboga, karoti, mayai na ndizi.
Acha kukaa kwenye kiti  kwa muda mrefu
Umewahi kujaribu kufanya mazoezi, kubadili chakula au hata kufunga na bado ukawa unasumbuliwa na kitambi au uzito kuwa mkubwa? Basi jibu la tatizo lako ni kukaa kwenye kiti muda mrefu.
Utafiti unaonyesha kukaa tu kwenye kiti hata kama hauli chakula kingi bado utaendelea kuongezeka uzito.
Kwahiyo, kama unataka kuondoa kitambi au tumbo au kupungua uzito kwa haraka acha kukaa saa nyingi kwenye kiti, hata kama kazi yako ni ya ofisini, jaribu kusimama kwa saa kadhaa huku ukiendelea na kazi yako.
Pakua vyakula visivyo na afya kwenye sahani nyekundu
Mbinu hii ya kushangaza ni kuwa unachohitaji kufanya ni kuweka chakula ambacho si afya yaani vile vinavyoongeza uzito kama chipsi, maandazi na vingine kama hivyo katika sahani ambayo ni nyekundu.
Utafiti unaonyesha kuwa watu walifanikiwa kula chakula kidogo baada ya kuwa wamewekewa chakula kwenye sahani nyekundu ukilinganisha na wakati walipowekewa kwenye sahani za rangi nyingine.
Mara nyingi tunahusianisha rangi nyekundu na alama ya kusimama na maonyo mengine katika maisha yetu ya kila siku.
Acha vinywaji vyenye sukari nyingi
Viongeza utamu vya kutengenezwa (artificial sweetners) na sukari kwa ujumla vimekuwa vikiwekwa kwenye vinywaji vingi.
Vinywaji vyenye sukari kama soda vimekuwa vikihusishwa na kuongezeka kwa mwili moja kwa moja.
Ni rahisi zaidi kuongezeka uzito ukitumia vinywaji hivi kwakuwa nishati yake ni rahisi kubebeka na kuvumilika tofauti na ile ya kwenye vyakula vigumu.
Kukaa mbali na vinywaji hivi na juisi nyingine zozote za dukani na hata za nyumbani zenye sukari, ni namna nzuri ya kudhibiti uzito bila kuhitaji mazoezi wala kufunga kula.
Badala yake, kunywa zaidi maji au chai ya kijani (green tea) au chai ya viungo mbalimbali (spiced tea) ukitumia asali kwa mbali badala ya sukari.
Pata usingizi mzuri na epuka msongo wa mawazo
Linapokuja suala la kuwa na afya bora kupata usingizi mzuri na kutokuwa na msongo wa mawazo (stress) ni vitu visivyoepukika. Usingizi na msongo wa mawazo vinaweza kuwa na matokeo ya moja kwa moja kuhusu njaa na uzito wako.
Ukosefu wa usingizi mzuri unaweza kuzisababishia homoni zinazohusika na kuweka sawa njaa (leptin na ghrelin) kutokufanya kazi zake vizuri. Homoni nyingine ya ‘cortisol’ inayohusika na utulivu pia inakuwa imeongezeka wakati unapokuwa na msongo wa mawazo.
Homoni hizi zikiwa zimesumbuliwa, njaa yako pia itaongezeka na uhitaji wako wa kula vyakula visivyo na afya utaongezeka mara dufu.
Usichofahamu ni kwamba kama hupati usingizi mzuri na wa kutosha unakuwa na uwezekano mkubwa wa kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya pili.
Wakati unakula usitumie simu au kompyuta
Kuwa makini na akili yote ukiiweka katika chakula tu kunaweza kusaidia kula kidogo.
Watu ambao wanakula huku wanatumia simu, kompyuta, wanaangalia luninga au wanacheza gemu huwa wanakula chakula kingi bila wao kujua.
Kunywa maji mara kwa mara
Kunywa maji mara kwa mara kunaweza kukusaidia kula chakula kidogo na hivyo kupunguza uzito hasa kama utakunywa nusu saa au robo saa kabla ya chakula.
Kunywa nusu lita nusu saa kabla ya chakula na utaona umefanikiwa kula chakula kidogo na hivyo utaweza kupungua uzito kirahisi.
Hutakawia kuona faida ya mbinu hii kama utakuwa umeamua kila siku kunywa maji kila mara na zaidi kila nusu saa kabla ya chakula.
Mwandishi wa makala haya ni tabibu wa tiba asili. Jaribu mbinu hii kisha wasiliana naye kwa WhatsApp +255769142586