25.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Kukamatwa Bobi Wine kwasababisha vifo saba

KAMPALA, UGANDA

WATU saba wamefariki dunia nchini Uganda kufuatia maandamano yaliyofanyika juzi Jumatano, kupinga kukamatwa kwa mgombea wa urais, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Msemaji aliiambia BBC jana kuwa kuwa zaidi ya waandamanaji 40 wamejeruhiwa katika makabiliano hayo na polisi.

Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda lilisema kuwa wafanyakazi wake waliwasaidia watu 11 waliokuwa na majeraha ya kupigwa risasi.

Wakati huohuo, wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao, Bobi Wine atakapoachiwa huru.

Wagombea hao walisema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.

Bobi Wine alikamatwa juzi Jumatano, Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.

Na punde tu baada ya wafuasi wake kupata taarifa, walianza kuandamana wakidai aachiliwe huru.

Machafuko hayo yalisambaa katika miji kadhaa na kusababisha watu wengi kujeruhiwa kutokana na risasi na mabomu ya kutoa machozi. 

Mayowe yalifuata machafuko yaliyozuka hapo siku ya Jumatano katika miji ya Kampala, Jinja, Tororo, Mbale, Soroti na Masaka. 

Hii ni baada ya watu kadhaa kubainika kupoteza maisha yao huku wengine wakipata majeraha mabaya sana.

Ijapokuwa habari mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na zile kutoka shirika la msalaba mwekundu zinaelezea kuwa angalau watu 11 waliuawa, jeshi la polisi limetoa taarifa kuwa ni watu watatu tu waliopoteza maisha yao na bado wanachunguza chanzo cha vifo vyao. 

Polisi inawalaumu wagombea urais na wafuasi wao kwa kuwachokoza na kusababisha hata askari wenzao kujeruhiwa katika machafuko hayo. Hayo ni kulingana na Msemaji wa polisi Fred Enanga.

Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa polisi na majeshi walitumia nguvu za kupindukia katika kukabiliana na makundi ya wafuasi katika miji mbalimbali na kusababisha wengi kujeruhiwa. 

Wanaelezea kuwa mazingira ya kampeni ni ya shamrashamra na watu hawawezi kudhibitiwa hisia zao za kushangilia wagombea na ukiwatatiza basi hisia hizo zinageuka kuwa za ghadhabu.

Katika mojawapo ya visa, gari lililokuwa na rangi za chama tawala cha NRM liliwagonga na kuwasababishia majeraha mabaya watu katika eneo lenye shughuli nyingi katikati mwa mji wakati dereva wake alipojaribu kuwakimbia watu waliokuwa wakitaka kuliharibu gari hilo.

Picha kadhaa za machafuko hayo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha kuwa hali ya taharuki ilikuwa imetanda kote. 

Rabsha aidha zilizuka mjini Gulu Kaskazini mwa Uganda wakati polisi walipomkamata mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha FDC Patrick Oboi Amuriat lakini akaachiwa usiku wa kuamkia leo.

Hata hivyo hadi wakati wa kuandaa taarifa hii Bobi Wine alikuwa bado amezuiliwa katika korokoro ya polisi mjini Jinja chini ya ulinzi mkali na viongozi wa chama chake cha NUP hawajaruhusiwa kuonana naye. 

Licha ya baadhi ya shughuli za biashara kuanza tena mjini Kampala, bado kuna taharuki kutokana na doria kali sehemu mbalimbali za mji. Wengi wanaelezea kuwa hawawezi kutoka nyumbani hadi pale watakapojua hatima ya suala la kukamatwa kwa mgombea urais Bobi Wine ambaye amejitokeza kuwa mshindani mkuu dhidi ya rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa safari hii.

Taarifa ya polisi haikusema watu hao wamefariki vipi, ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu waliotapakaa damu huku wengine wakioneshwa kutoweza kufanya lolote yaani wamepigwa risasi na kufariki dunia.

Polisi pia imesitisha matukio kadhaa ya kampeni ya wagombea wa upinzani. Mawakili wa Bobi Wine wanasema bado mteja wao hajafikishwa mahakamani.

Mgombea mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia alikamatwa na kuachiwa huru. Mikutano ya kampeni ya Bobi Wine imekuwa ikizuiwa na polisi katika matukio kadhaa.

Marekani imeshutumu ghasia zilizojitokeza katika mji mkuu wa Kampala na miji mingine nchini Uganda kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa Bobi Wine.

Ujumbe wa Marekani umesema kuwa “pande zote zipinge vita” na kuchukua hatua za kupunguza hofu iliyotanda nchini humo.

Bobi Wine alikamatwa wakati wa mkutano wa kampeni kwa madai ya kukiuka miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliyowekwa na Tume ya uchanguzi.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, wafuasi wake walianza maandamano wakidai aachiliwe huru. Uganda itafanya uchaguzi wa urais mnamo mwezi Januari 2021.

BBC, AFP

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,454FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles