Na Mwandishi Wetu
KWA muda mrefu Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanaepukana na mambo yanayoweza kuathiri afya zao.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imekuwa ikifanya kampeni mara kwa mara kuhamasisha wananchi kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwaletea magonjwa ya mlipuko.
Miongoni mwa magonjwa ambayo yamekuwa hatari, ni kipindupindu ambacho kinaenezwa kwa kiasi kikubwa na uchafu na kutozingatia kanuni za afya.
Leo tumelazimika kusema haya, baada ya gazeti hili toleo la jana kuchapisha habari kuwa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vyoo.
Habari hiyo, inasema zaidi ya kaya 5,551 hazitumii vyoo, badala yake zinajisaidia porini.
Pamoja na Serikali kuwa na timu ya hamasa ya kitaifa ya kampeni ya uhamasishaji matumizi bora ya vyoo ijulikanayo ‘usichukuliye poa nyumba ni choo’ inayoratibiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, mwitikio wa wananchi unaonekana bado uko chini na hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa.
Kwa mfano, Kaimu Ofisa Afya Wilaya ya Serengeti, Malima Ndagara, anasema hali ya matumizi ya vyoo katika wilaya hiyo si nzuri kutokana na mwamko kuwa chini.
Anasema pamoja na uhamasishaji wa mara kwa mara juu ya umuhimu wa kutumia vyoo kwa kushirikiana na mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali, bado wananchi wengi wanajisaidia vichakani, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa afya.
Lakini kibaya zaidi anasema wananchi wengi hawajachukua hatua ya kubadilika. Hali inayoonyesha kazi ya ziada inahitajika zaidi kutoa elimu.
Kinachotakiwa hapa, Serikali na wadau wengi wanapaswa kutafuta njia mbadala ya kufikisha elimu kwa wananchi wa wilaya hii. Kwa mfano kutumia matamasha ya asili ya maeneo husika yakiwa yamebeba ujumbe wa matumizi bora ya vyoo, kuonyesha sinema ambazo tunaamini zitavuta wananchi wengi kwenda kuangalia.
Pili, uongozi wa wilaya unapaswa kuweka utaratibu makini ambao utasimamiwa vizuri na mabwana na mabibi afya kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye kaya.
Tunakumbuka zamani, kulikuwa na utaratibu wa viongozi wa Serikali za mitaa na vitongoji kufanya ukaguzi wa vyoo, na kila mtu ambaye alikuwa hana alipigwa faini.
Hali hii ilisaidia kila kaya kuhakikisha haikosi vitu hivyo, lakini leo hii utaratibu huu umezikwa na waajiriwa wa Serikali ambao ni mabwana na mabibi afya wapo tu.
Tunasema haya kwa sababu kuna athari kubwa ya mwananchi kutokuwa na choo kwani magonjwa mengi kama kipindupindu, kuhara, minyoo, kichocho, amiba na homa ya matumbo ni rahisi kuyapata.
Tunaushauri uongozi wa wilaya chini ya Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara kuibana vya kutosha kamati ya afya ya wilaya ili itimize majukumu yake na si watumishi kukaa ofisini kusubiri mshahara.
Sisi MTANZANIA, tunasema hakuna sababu ya watu kwenda kujisaidia porini kwa sababu huo ni uharibifu mkubwa wa mazingira.
Pia tunashauri uongozi huo uhakikishe unawabana viongozi wa ngazi za vijiji, mitaa na kata kukagua kaya kwa kaya kama kuna choo tukiamini njia hii itasaidia kupunguza tatizo.
Tunawakumbusha wananchi wa Serengeti na maeneo mengine nchini kuwa umefika wakati wa kubadilika na si kusubiri Serikali iwasukume kujenga vyoo.