Ashura Kazinja, Morogoro
AFYA ya uzazi kwa vijana wa rika la balehe ni muhimu mno. Hii ni kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwamo mimba za utotoni, magonjwa, utoaji mimba usio salama na hata kifo.
Afya ya uzazi inahusisha uzazi wa mpango ambao umeanzia katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2018-2023, lengo likiwa ni taifa kuwa na idadi ya watu ambao linaweza kuwahudumia.
Hata hivyo, suala hili la uzazi wa mpango limekutana na vipingamizi kadhaa hususani kwa nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kutokana na watu kuupokea kwa maana tofauti kwa madai ni mpango wa nchi za magharibi kupunguza idadi ya watu Afrika, wakichukulia mfano wa nchi za Japan na Ujerumani ambako idadi ya wazee ni kubwa kuliko vijana.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mtamba, Halmashauri ya Morogoro, Florence Mwambene, anasema afya ya uzazi kwa vijana waliopo na wasiokuwa shuleni ni muhimu kutokana na vijana wengi kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo.
Anasema wameendelea kutoa elimu na kuhimiza elimu ya malezi na makuzi kwa makundi rika, pamoja na kutunga sheria ndogo za kuzuia vigodoro kwa lengo la kumlinda mtoto na kumuwezesha kusoma ili awe na maendeleo mazuri ya baadae na kwa taifa pia.
Anasema wanatoa elimu ya kujitambua na afya ya uzazi kwa vijana ambao wako katika rika la balehe walioko shuleni na wale walioko nje ya shule ili waweze kujilinda, kuijua thamani yao na kuepuka kudanganywa na watu wanaopenda watoto wadogo.
Akizungumzia suala la uzazi wa mpango kwa vijana, anasema kwa vijana walioko shuleni wanazingatia kuwafundisha kusubiri hadi wakati wao utakapofika na kwamba, hawahimizi zaidi upatikanaji wa kondomu shuleni na njia zingine za uzazi wa mpango.
“Kwakweli kwa halmashauri yetu, shuleni tunazingatia zaidi kuwafundisha wasubiri hadi wakati wao utakapofika, hatuhimizi upatikanaji wa kondomu shuleni. Lakini kwa wale walioko nje ya shule tunawaelekeza malezi ya kujitambua, na wale wanaoshindwa tunawashauri kutumia kondomu kwa sababu ni njia mojawapo ya kujilinda,” anasema Mwambene.
Anasema wanatekeleza sera na miongozo ya serikali juu ya ulinzi wa watoto na wanawake kwa ujumla, kwa kushirikiana na dawati la jinsia la polisi kwa ajili ya kuhakikisha mtoto anakuwa salama katika nyanja zote.
Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kisemu, Kanga Mazengo, anasema katika shule hiyo vijana wanapata elimu inayohusiana na uzazi na afya ya magonjwa mbalimbali.
Mazengo anasema wahudumu wa afya toka zahanati ya Kijiji cha Kisemu, huwa wanafika mara kwa mara shuleni hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi, ingawa hawakuwahi kutoa kondomu kwa wanafunzi.
Anasema hali ya mimba shuleni hapo kwa sasa si changamoto inayowasumbua tofauti na awali, kutokana na shule kuwa na utaratibu wa kuwapima wanafunzi wa kike ujauzito kila baada ya miezi mitatu, na hivyo kuwajengea hofu ya kushiriki vitendo vya ngono.
“Shule yetu inautaratibu wa kuwapeleka wanafunzi wa kike hospitali kupima ujauzito kila baada ya miezi mitatu, na akigundulika ni mjamzito kama sheria inavyosema anafukuzwa shule,” anaeleza Mwalimu Mazengo.
“Unapompima binti kwanza unampa woga na tahadhari hivyo, anaogopa kufanya tukio hilo kwa sababu anajua baada ya muda mfupi atapimwa na atajulikana, na madhara ya kukutwa na ujauzito anayajua,” anasema Mazengo.
Anasisitiza kuwa si vyema kumpa mwanafunzi kondomu, au kumpa njia zingine za uzazi wa mpango, kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kumtuma akafanye vitendo vya ngono hivyo, anaona ni bora kumpa elimu ya kujitambua na madhara ya kushiriki ngono katika umri mdogo.
Kwa upande wake Mkunga mkongwe wa Zahanati ya Kisemu, Tabia Salum, anasema kwa sasa vijana wanajitokeza kwa wingi kupata huduma ya uzazi wa mpango tofauti na awali na kwamba, vijana wa kiume wengi wanapendelea kondom kama njia ya kupanga uzazi, pia huitumia kujikinga na maradhi yatokanayo na kujamiiana.
“Vijana wanajitahidi mno, wengi wanahudhuria kliniki, hata wanaume kwa sasa wanakubali kuongozana na wake zao wanapokuwa wajawazito kuja kliniki, na wanakubali kutumia uzazi wa mpango,” anasema mkunga Tabia.
Anasema wanatumia mbinu mbadala kumfanya baba kuhudhuria kliniki pamoja na mke wake, huku akisema kwa wale ambao wamepewa mimba na wanaume wenye wake zao huwashauri kuhudhuria kliniki kwa nyakati tofauti mbinu ambayo imezaa matunda.
“Mama anapokuja bila baba kliniki hatumpokei, hii imesaidia akina baba kujitokeza na kuwasindikiza wake zao, kama baba ni mume wa mtu tuna tumia mbinu mbadala ya mama kuja siku ya leo na baba anakuja kesho yake,” anaeleza.
Akizungumzia kundi la vijana walioko shuleni, anasema wanazungumza nao kuhusu tahadhari na mimba za utotoni, huku wakiwasisitizia juu ya changamoto zinazosababishwa na kushiriki ngono katika umri mdogo ikiwamo kupata ugonjwa wa fistula, kujifungua kwa njia ya upasuaji na hata kupoteza maisha.
Naye Meneja Utetezi Mradi wa Advance Familiy Planning (AFP), James Mlali, anasema kumekuwapo na changamoto mbalimbali zinazotokana na uzazi wa mpango na afya salama ya uzazi kwa jamii, ambayo inahitaji kutiliwa mkazo kwa elimu kuwafikia watu wote mjini na vijijini, ili kuondoa imani potofu iliyojengeka kuwa uzazi wa mpango una madhara na ni mbinu ya watu weupe kupunguza idadi ya watu Afrika.
Mlali anasema ili kuwapo utetezi wenye ufanisi katika elimu ya uzazi wa mpango, mradi wa AFP umelenga zaidi ulimwengu wa nchi za kusini mwa dunia zikiwamo nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria, Indonesia na Kongo.
Hata hivyo, anasema awali chanzo kikuu cha fedha kilikuwa ni kutoka serikalini, lakini kuanzia mwaka 2014 hadi sasa halmashauri nazo zinapanga bajeti juu ya uzazi wa mpango ingawa imekuwa ikitoa kiasi kidogo na kwamba mkakati uliopo ni kuyashawishi mashirika binafsi ya bima na bima ya taifa ili yaweze kuingiza uzazi wa mpango katika mfumo wao.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, anasema ni muhimu ikapatikana katika maeneo yote mjini na vijijini huku kukiwa na watoa huduma wenye sifa, pamoja na njia za uzazi wa mpango kuwa nyingi ili kutoa nafasi kwa mhitaji kuchagua.
Ni vyema serikali na jamii kwa ujumla kutilia mkazo suala la afya ya uzazi kwa vijana, kwani kundi la vijana kuanzia miaka 10 hadi 19 limesahaulika, na hii husababisha mtoto hadi wa miaka 11 kushtukia ana mimba huku akiwa haelewi kitu, ni vyema kundi hili likapewa umuhimu na elimu ya kutosha.