31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU: Viongozi wakubali kukosolewa walipokosea, wajirekebishe

WAKATI Watanzania wakijiandaa kupiga kura kuchagua madiwani, wabunge na rais, kuna hoja nyingi muhimu ambazo zinatakiwa kujadiliwa kitaifa, kwa maslahi ya jamii nzima.

Miongoni mwa hoja hizo ni inayoangazia kundi la vijana, ikiwa
wanatambua wajibu wao kwa taifa, kutokana na ukweli kwamba wao ndio
wengi kuliko rika lingine nchini. Kama ilivyo kwa makundi mengine ya jamii, vijana wamegawanyika katika makundi mbalimbali; kwa upande wa siasa, wamegawanyika kiitakadi za vyama huku baadhi yao wakiwa hawana kabisa mlengo wa chama chochote cha siasa.

Katika hali ya kawaida vijana wanapaswa kuunganishwa na dhamira ya
utaifa, ambayo huwaunganisha wote kutokana na rika lao licha ya kila
mmoja kuwa na mlengo wake wa itikadi za kisiasa. Kabla ya ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa, suala hilo lilikuwapo na asilimia kubwa ya vijana walikuwa na uelewa wa pamoja, kuhusu sera za nchi, dira ya taifa na malengo yao ya wakati uliyopo na ujao
kitaifa.

Hali hiyo imetetereshwa na ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa,
kutokana na ukweli usiyopingika kuwa umoja na mshikamano wa kitaifa
kwa vijana, hususani katika kufanikisha maendeleo ya nchi haupo kwa
kiwango kinachotakiwa. Hakuna anayeweza kupinga kwamba kuna aina fulani ya uadui wa kiitikadi na kivyama miongoni mwao, tofauti na matarajio kwamba linapokuja suala la changamoto zinazowakabili wananchi, kundi hilo linatakiwa kuungana na kuweka kando tofauti zao kisiasa.

Hii inaashiria kuwapo wakati ambao taifa liliyumba, katika kusimamia
maadili na misingi ya taifa na bila shaka kipindi cha kunzia mwaka
1992, ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi nchini. Pamoja na nyufa zinazotokana na tofauti za itikadi za kisiasa miongoni mwa vijana, imebainika hata wale ambao wanaunganishwa na itikadi za vyama vyao, wanapokuwa ndani wamegubikwa na mgawanyiko unaotokana na maslahi binafsi.

Kutokana na dosari hizo, imekuwa sawa na kawaida kushuhudia kijana
akipinga hoja ilitolewa na kijana mwenzake, kwa sababu ya
tofauti zao za itikadi za vyama vya siasa. Ukiacha itikadi za vyama vya kisiasa na maslahi binafsi, vijana ndani ya vyama vyao vya siasa wamekumbwa na kasumba ya kupinga hoja bila kujali umuhimu wake kwa jamii, kutokana na silka ya mtu, uhusiano na historia ya mtoa hoja.

Ingawa ni kweli kwamba kasumba hii imetiwa nguvu na ujio wa vyama
vingi, historia inaonesha kwamba ilikuwapo tangu miaka ya 1960 lakini
zilikemewa na mamlaka zilizokuwa zikidhibiti mienendo ya vijana
nchini.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuandika machapisho,
ili kukosoa na kuongoza jamii katika misingi inayostahili. Mathalani
vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere
kikiwamo kinachofahamika kwa jina la Tujisahihishe.

Andiko hilo lilitiwa nguvu na mwongozo wa CCM wa mwaka 1981, ambapo
hatua za kukosoa, kujikosoa na kukosoana zinapewa maana anuai. Kwanza wanachama na viongozi wanatakiwa kuwa tayari kusema ukweli,
kuuishi ukweli wanaousema na kukubali kuambizana ukweli. Pili wanachama, hususani viongozi wanatakiwa wawe tayari kukosolewa bila kuhamaki na inapobidi wakubali kujirekebisha. Tatu wanachama au vyama vya siasa vinapofanya vikao vya ngazi zote, vinatakiwa kuwa na utaratibu wa kujitathmini na kujikosoa.

Kwa mujibu wa historia, enzi za mfumo wa chama kimoja tabia za
kufichiana makosa maarufu, kuleana kulichochewa zaidi na kufahamiana
kulikojikita katika maslahi  binafsi. Hoja iliyotolewa na kijana kwenye kundi lenye nguvu ndani ya chama lina maslahi naye, hata kama ilikuwa hoja dhaifu iliungwa mkono kwa nguvu, tofauti na hali ilivyokuwa kwa hoja sawa na hiyo ambayo ilitolewa na ambaye kundi lenye nguvu halikuwa na maslahi naye.

Ni katika mazingira hayo msemo wa “Hoja ya Nguvu na Nguvu ya Hoja” ulipotumika.

Kasoro hizo ndizo zinazoshuhudiwa zikiota mizizi nyakati hizi, tofauti
ni kwamba awali hoja zilipingwa au kuungwa mkono kutegemeana na mtoa hoja anaungwa mkono na wenye nguvu ndani ya chama kwa kiwango gani, sasa hoja inapingwa au kuungwa mkono kwa kutegemeana na itikadi za kisiasa za mtoa hoja.

Bila kujali athari zinazolipata taifa, kundi la wanachama wa chama
fulani halioni taabu kukejeli, kupiga vijemba mtu aliyetoa hoja yenye
maslahi kwa taifa, eti kwa sababu tu ni kijana wa chama tofauti na
chama chao cha kisiasa. 

Pia mara nyingi imeshuhudiwa upendeleo usiyokuwa na tija kwa taifa ukifanywa, kuteteana na kufichiana makosa miongoni mwa vijana kwa kusababu ya itikadi za vyama vya kisiasa, bila kujali kuwa taifa lipo
mikononi mwa vijana wote.

Ni ndoto za alinacha kuamini kuwa vijana wenye mlengo mmoja kisiasa
ndiyo pekee wenye hoja, zinazoweza kulifikisha taifa kwenye malengo
liliyojiwekea. Ifike mahali ule ukweli kwamba vijana wote wana nafasi sawa katika kutoa hoja, uzingatiwe na kila hoja inayotolewa ipimwe kwa ubora, umuhimu wake kitaifa ili hoja zenye tija zitumike katika ujenzi wa nchi.

Baadhi ya nchi, ikiwemo China, North Korea, Rusia na Marekani vijana
bila kujali tofauti zao zikiwemo za itikadi za vyama vya siasa, wamewekewa misingi na imani ya utaifa.

Misingi hiyo imewafikisha hatua ya wengi wao kuamini kuwa, hakuna haki
nje ya taifa lao  jambo ambalo ni aghalabu nchini Tanzania. Nchi yoyote ambayo vijana wameiva kwa misingi na imani za utaifa, huwa hodari na thabiti katika kupambania maendeleo ya nchi yao. Hali hiyo pia husababisha vijana kuwa na ndoto kubwa, ambazo huzifikia kutokana na kuwa na bidii katika kuhakikisha wanazifikia bila kuchoka
wala kukatishwa tamaa na hali au mtu yeyote.

Kwa kijana aliyepikwa akaiva katika misingi na imani ya utaifa, malengo ya nchi kwake hayatofautiani na malengo yake binafsi. Hii inatokana na ukweli kwamba misingi hutoa uelekeo katika maisha, na imani huonesha njia ya kuelekea mafanikio hivyo bila kuwa na nyenzo hizo muhimu umoja katika kuelekea ndoto kubwa kitaifa huwa dhaifu. Ili kuwa na vijana wenye manufaa kwa taifa, lazima taifa liwe na lengo la pamoja, lifahamike kinagaubaga kwa jamii katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, kuanzia katika umri wa utoto ndani ya familia na shuleni.

Bila shaka, rika la vijana ambalo limekuzwa likiimba lengo la taifa,
itakuwa vigumu kugawanywa na itikadi za vyama na hivyo watakuwa vijana
wenye ustadi wa kitaalam na uchu wa kuanzisha au kung’amua njia mpya
za kutatua changamoto, ili kulifikia lengo kuu la taifa. Badala ya kutofautiana kwa itikadi za vyama vya siasa, jambo lisilo na tija kubwa katika maendeleo ya nchi, vijana watatofautiana katika njia za kutatua changamoto huku wakilenga kufikia lengo kuu la taifa.

Wakati ikiwa dhana hiyo itafanikiwa, ni dhahiri vijana watakuwa mfano katika kazi yoyote wanayokabidhiwa kusimamia.

Ni katika mzingira hayo kona hii ikaja na hoja inayohoji ikiwa vijana
nchini Tanzania, wanajitambua na wanatambua umuhimu wao katika
maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla? mbali na lengo kubwa la taifa, vijana wana ajenda mfanano inayotumika kwa mustakabali wa maeneleo ya nchi miaka 20 ama 30 ijayo? Haya yote ni masuala ya mjadala.

Mwandishi; Said Said Nguya Mchambuzi wa masuala ya Siasa na Maendeleo Nchini Kutoka Jijini Dodoma 0742102913

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles