25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KENYA: RAILA ANAMUANDAA BINTIYE KUMRITHI?

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA,

NANI atakayemrithi Kiongozi wa Chama cha upinzani cha ODM nchini Kenya, Raila Odinga kisiasa katika familia yake yenye mizizi ya kisiasa?

Ni swali lililokuwa likiumiza vichwa vya wengi kwa muda mrefu hasa baada ya kifo cha mwanawe Fidel Odinga mwaka juzi katika taifa, ambalo viongozi tangu enzi za mwasisi wake, baba wa Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, Mzee Jomo Kenyatta wamekuwa na tabia ya kuwaandaa kisiasa watoto wao.

Hatimaye kitendawili hicho ni kama kimeteguliwa wiki mbili zilizopita baada ya Rosemary Odinga, binti wa kigogo huyo wa upinzani kutangaza kuwania kiti cha ubunge cha Kibra, Kaunti ya Nairobi.

Kabla ya kutangaza nia hiyo awali alionekana akiongozana na vigogo wa ODM mjini Nairobi katika kampeni ya kuhamasisha wakazi kujiandikisha kwa wingi kupiga kura jimboni humo, ambamo kuna ‘wafuasi vichaa’ wa Raila.

Ni hatua ambayo iliibua swali kuu: Atafanikiwa kujaza pengo kubwa litakaloachwa wakati baba yake atakapostaafu siasa?

Nchini Tanzania, mwaka jana Rosemary anakumbukwa aliposababisha malumbano makali baina ya Watanzania na Wakenya katika mitandao ya jamii.

Ni pale aliposikika akizungumza katika kongamano moja la vijana kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, akisema Bonde la Olduvai Gorge liko nchini Kenya.

Kauli hiyo ilizua mijadala na hisia baina ya pande mbili za mataifa haya jirani, huku Watanzania wakidai Wakenya wanawachokoza.                             

Kwa kuona hilo, Rosemary alilazimika kujirudi na kuomba radhi, akisema hakuwa na nia mbaya aliposema Olduvai Gorge ipo Kenya ilhali ni Tanzania kwa vile mataifa yote yako ndani ya Afrika Mashariki.

Rosemary ambaye hufahamika zaidi kutokana na biashara yake ya kipekee ya kufuga konokono alisema;” nitajitafutia ufanisi kisiasa bila kutumia kivuli cha umaarufu wa familia ya baba au babu yake Marehemu Mzee Jaramogi Oginga Odinga.”

Maswali kuhusu atakayechukua mahali pa Odinga atakapoamua kustaafu siasa yalianza kuibuka tangu wakati Katiba mpya ilipopitishwa ikizuia wagombeaji urais kuwania ubunge.

Ilitarajiwa mmoja wa wanawe angemrithi ubunge baina ya Kibra na Lang’ata, ambayo yaligawanywa kutoka lililokuwa Jimbo la Lang’ata, alilowakilisha Raila kwa miaka 20 kuanzia 1997 hadi 2013.

Lakini waliokuwa watu wengine kutoka chama chake, Ken Okoth alishinda kiti cha ubunge cha Kibra huku Joash Olum akinyakua kile cha Lang’ata.

Kifo cha mwanawe, Fidel kiliwakanganya zaidi wadadisi wa kisiasa kwa kuwa wengi wao walimchukulia kuwa mrithi namba moja wa babake kisiasa.

Uamuzi wa Rosemary umezidi kuibua hisia tofauti huku baadhi wakiusifu, wakisema ana haki sawa na Mkenya yeyote kugombea wadhifa popote pale anapotaka, lakini wengine wameushambulia. Kwamba unatoa picha kuonesha familia ya Odinga ni lafi na yenye kupenda makuu.

Aliyekuwa kiongozi wa kampeni za urais 2013 na msiri wake Odinga, Eliud Owalo alisema uamuzi huo huenda ukamharibia Raila nafasi ya kushinda urais mwaka huu.

“Ni vyema Raila achague kati ya kujishindia kiti cha ubunge Kibra kupitia Rosemary na urais. Kwa bahati mbaya, hawezi kushinda vyote viwili kwa wakati mmoja” alisema Owalo ambaye pia anamezea mate ubunge wa jimbo hilo kupitia ODM.

Mwaka uliopita, Owalo aliandika barua kwa wasimamizi wa uchaguzi ODM kulalamika fununu kuwa kutakuwa na upendeleo wakati wa kura za mchujo chamani.

Hata hivyo, Rosemary alisema wakati wa mahojiano yake kuwa, anaamini ODM kuna uwazi na hatarajii kupendelewa kwa vyovyote vile.

“Kama kuna nafasi yangu kuingia katika siasa, sitaogopa kwa sababu Kenya ni nchi yetu na mimi pia ni Mkenya. Ninataka kuona Kenya ikipata maendeleo,” alisema.

Kwa sasa, macho yote yako kwa Mbunge Okoth, ambaye amemwagiwa sifa kuleta maendeleo eneo hilo na hata kuibuka wa pili kitaifa miongoni mwa wabunge waliotumia vyema Fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Majimbo (CDF).

Okoth alisema haoni shida kwa Rosemary kujitosa kwenye kinyang’anyiro eneo hilo kwa vile yeye amekuwa akipigania wanawake zaidi kuwania nyadhifa za kisiasa.

“Ninasema amekaribishwa. Tutakutana naye kwa heshima na taadhima,” alisema na kueleza matumaini yake kuhudumu kwa zaidi ya muhula mmoja.

Ingawa itakuwa mara ya kwanza kwa mtoto wa Odinga kugombea wadhifa wa kisiasa, jamaa zake wengine tayari wamo katika siasa.

Dk. Oburu Oginga ambaye ni kaka yake alikuwa Mbunge wa Bondo kuanzia mwaka wa 1995 hadi 2013 baada ya kufariki kwa baba yao Jaramogi Oginga Odinga. Kwa Oburu ni mbunge wa viti maalumu.

Katika Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga ambaye ni dadake ndiye naibu gavana na amesemekana kumezea mate ugavana wakati wa uchaguzi mkuu ujao, ilhali Mbunge wa Gem, Jakoyo Midiwo ni binamuye Odinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles