NA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM
MMOJA wa wanariadha wa mbio ndefu ‘Marathon’ watakaoiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki itakayoanza Agosti 5-21 jijini Rio de Jeneiro, Brazil, Fabiano Joseph, ameitaka Serikali kutoka haraka kiasi cha Sh milioni 80 kwa ajili ya safari yao.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Filbert Bayi, kusema kuwa hadi sasa Serikali haijawajibu ombi lao la bajeti ya safari hiyo iliyowasilishwa kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu kutoka Ilboru, Arusha ambako ameweka kambi kujifua kwa maandalizi ya michezo hiyo, Fabiano alisema yeye binafsi anasikitishwa na kitendo cha Serikali kukaa kimya juu ya jambo hilo.
“Mimi naendelea kufanya mazoezi kujiandaa na safari lakini hadi sasa nimekuwa nikijikuta nakata tamaa baada ya kuona Serikali hadi sasa haitusapoti, hivyo ningependa kuchukua fursa hii kuiomba Serikali itoe haraka fedha hizo kutuondoa wasiwasi,” alisisitiza mwanariadha huyo.
Fabiano ataambatana na wenzake watatu ambao ni Saidi Juma Makula, Alponse Felix Simbu na Sara Ramadhani Makera, wote kwa pamoja wamefuzu vigezo vya kushiriki michezo hiyo ya kimataifa.