NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KLABU ya Yanga sasa akili zao zote ni kujipanga kwa Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, inaelezwa tayari Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amewamulika baadhi ya wachezaji nyota kutoka Afrika Magharibi ili kuwasajili.
Katika mpango huo wa Mholanzi, inadaiwa ametamanishwa na wachezaji wawili kutoka Ghana, ambao anafikiria kuwanasa kwa msimu ujao ili kuipa makali zaidi Yanga ambayo msimu huu imeishia raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kutolewa na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Habari za uhakika kutoka Yanga zilizolifikia MTANZANIA zimeeleza kuwa, Yanga imepanga kuwa na kikosi hatari zaidi msimu ujao ili kuweza kupambana vizuri na timu kubwa za Afrika kama vile TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kila mwaka.
“Yanga tumefurahishwa na mwenendo wa timu yetu kwenye michuano ya kimataifa kwa miaka miwili hii, tuna mpango mkakati wa kufanya vizuri zaidi mwakani (Ligi ya Mabingwa) na moja ya mambo ya kufika huko ni kutengeneza kikosi imara zaidi,” alieleza mpasha habari huyo.
Chanzo hicho kilizidi kueleza kuwa hivi sasa wanapigana ili wachezaji wa kimataifa waongezwe kutoka watano na kufikia 10, ili kuongeza ubora wa kikosi na kufanikisha malengo yao.
“Tuna kocha mzoefu (Hans van Pluijm) anayelijua soka la Afrika hususani Ghana anapoishi na aliwahi kuzinoa timu kadhaa za pale, hivyo kuna baadhi ya wachezaji wawili wakali kiungo mshambuliaji na mshambuliaji, anawajua kutoka Ghana ambao anawahitaji kikosini ili kukiongezea makali,” kilieleza zaidi.
Msimu uliopita Pluijm alipoifundisha Yanga kwa mara ya kwanza kwa muda wa miezi sita na kuiongoza kushika nafasi ya pili kwa pointi 56, aliahidi kuiletea timu hiyo wachezaji bora wawili (mshambuliaji na kiungo mshambuliaji) kutoka Ghana.
Mpango huo ulikwama baada ya kocha mpya wa Yanga, Marcio Maximo kuipa masharti timu hiyo ya kufanya usajili wake mwenyewe, jambo ambalo liliwalazimu viongozi kusitisha ujio wa Waghana na Mbrazil huyo akaja na Wabrazil wake, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ aliyeondoka na Andrey Coutinho ambaye bado yupo.