Na ASHA BANI
MAISHA hayatabiriki na hakuna aijuaye kesho. Hivi ndivyo naweza kusema kutokana na historia ya maisha ya watu wengi.
Katika maisha tunayoishi, kila siku kuna kupanda na kushuka lakini juhudi zako pekee ndizo ambazo zinaweza kukufanya uwe juu au chini.
Mbunge wa Liwale kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Zuberi Kuchauka, ni miongoni mwa watu ambao hawakukata tamaa katika mapambano ya maisha.
Alianza kwa kujishughulisha na shughuli zake ndogondogo, ikiwa ni pamoja na kuendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu wiki iliyopita, Kuchauka anasema tangu mwaka 2001 hadi 2005, alikuwa akiendesha bodaboda ya abiria eneo la Tabata Barakuda jijini Dar es Salaam.
HARAKATI ZA KISIASA
Kuchauka anasema katika harakati zake za kisiasa, aliwahi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2005.
“Mwaka huo niligombea ubunge wa Liwale ambapo kulikuwa na washindani wengine kwenye kura za maoni ambao ni Hassan Chande na Garama Kindeu.
“Nikachukua nafasi ya tatu na Hassan Chande alipita kwa kura 300, huku mimi nikipata kura 16 tu. Baadaye mwaka 2008 nilijiunga na CUF katika tawi lililopo Kijiji cha Mpiga Mti.
“Mwaka 2010, niliamua kurudi tena jimboni na kugombea ubunge kwa tiketi ya CUF ambapo kwenye kura za maoni walikuwa wagombea wawili.
“Katika uchaguzi ule wa kura za maoni, mwenzangu Madaraka Bei alinishinda kwa kura 90 huku mimi nikiambulia kura 90,” anasema Kuchauka.
Pamoja na hilo, mbunge huyo anasema katika uchaguzi huo, Bei hakufanikiwa kushinda na hatimaye mgombea wa CCM, Faith Mtambo, alishinda.
“Sikuwa na tamaa niliendelea na kujenga chama kwa kushirikiana na wana Liwale kwa hali na mali na mwisho wa mwaka 2015, nikajitosa tena katika kinyang’anyiro hicho kupitia CUF na nikashinda,”.
Akizungumzia changamoto alizokumbana nazo katika uchaguzi huo, Kuchauka anasema alikumbana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na uchaguzi kutawaliwa na rushwa.
MAFANIKIO NDANI YA MWAKA MMOJA
Kuchauka anasema amepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa karibu mauzo ya zao la korosho kwa mwaka huu.
Anasema wakulima wameweza kupata bei nzuri ya juu ambapo kwa Liwale, kilo ni 3,710 ukilinganisha na wilaya nyingine.
Anasema amefanikisha kutembelea maeneo mbalimbali yenye migogoro likiwemo la Bwana la Kiulumila lililopo Kikulyungu, lililokuwa na mgogoro uliodumu kwa takribani miaka 10 kati Pori la Akiba la Selous lililopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wananchi.
Anasema Selous ndio waliomega eneo la wananchi na kulipeleka upande wao, hivyo wamefanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha linarudi katika eneo la wananchi.
“Tayari hadi sasa Mkuu wa Mkoa na Wilaya wameshafika kuangalia eneo jingine na kuahidi watalitafutia ufumbuzi, huku Waziri wa Malisili na Utalii naye akiahidi kufika katika eneo hilo,” anasema Kuchauka.
Anasema amefanikiwa kutembelea vijiji zaidi ya asilimia 75 ya vijiji na maeneo mengine kuwapelekea mahitaji yao.
Amefanikiwa kujenga vyoo vya shule sita za msingi na sekondari, vyumba vya madarasa ya shule za awali katika vijiji viwili.
Kuchauka anasema amekagua miradi mikubwa ya Umeme Vijijini (REA), maji katika skimu ya umwagiliaji.
CHANGAMOTO JIMBONI
Mbunge huyo anasema changamoto kubwa ni ya sekta ya afya, ambapo wanakabiliwa na uhaba wa vituo vya afya.
“Jimbo nzima lina kituo kimoja cha afya huku uhitaji ukiwa ni vituo 20. Hospitali ya wilaya haina daktari bingwa, majengo ya kutosha na ina uhaba wa wafanyakazi.
“Changamoto nyingine ni maji ambapo Mji wa Liwale hauna maji safi na salama ya kutosha hivyo wakazi wake wakiongozwa na akina mama wamekuwa wakihangaika.
“Kwa upande wa miundombinu, barabara zote ni za vumbi na hivyo kusababisha majira ya masika kushindwa kupitika,” anasema.
Akizungumzia kwa upande wa elimu, anasema kuna uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa kwa elimu ya msingi huku sekondari wakikabiliwa na uhaba wa maabara na walimu wa masomo ya sayansi.
KUCHAUKA NI NANI?
Akizungumzia historia yake, Kuchauka anasema alizaliwa mwaka 1962 katika Kijiji cha Mpigamiti, Liwale. Mwaka 1974 hadi 1980, alisoma shule ya msingi Mpigamiti.
Mwaka 1981 hadi 1984 alisoma Sekondari ya Ufundi Mtwara (Mtwara Technical Collage). Mwaka 1985 hadi 1988 alienda Arusha Chuo cha Ufundi, Mwaka 1988 alipata ajira katika Kampuni ya National Milling Cooperation kama fundi mchundo.
Mwaka 1992-1996 alijiunga na mafunzo ya usindikaji wa nafaka ‘Milling engeneering’ akiwa kama msindikaji wa nafaka.
Mwaka 1996 alijiunga na Kampuni ya Mohamed Enterprises hadi mwaka 1998 ndipo akajiunga na Farai Group kikundi kilichopo Singida kama msindikaji mkuu wa nafaka.
“Hapo nilifanya kazi mwaka mmoja nikarudi Dar es Salaam, nikajiunga na Mohamed Enterprises na kufanya kazi katika kipindi cha mwaka mmoja na kurudi tena kwa Kampuni ya Bakhersa,” anasema Kuchauka.
Anasema alifanya kazi Bakhresa kwa kipindi cha miaka 10 hadi mwaka 2010 Januari, akaacha na mwaka 2011 hadi 2014 kujiunga na Kampuni ya Mikoani Traders Milling Injinia.
Baada ya hapo, niliachana na shughuli hizo na mwaka 2005 nikajiandaa na uchaguzi.