30.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

Kubenea kuzindua kampeni leo

ASHA BANI-DAR ES SALAAM 

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Kinondoni, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Saed Kubenea, amepanga kufungua kampeni zake za kuwani nafasi hiyo, leo jijini Dar es Salaam.

Kubenea ambaye amepata kuwa mbunge wa Ubungo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika uchaguzi mkuu uliyopita, katika uchaguzi huu, anakabiliana na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abasi Gulamhussen Tarimba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mratibu wa uchaguzi wa ACT- Wazalendo, katika jimbo la Kinondoni, Leila Madibi, mkutano wa kumnadi Kubenea, utafanyika kwenye viwanja vya Buibui, Mwananyamala.

Leila anasema, mgombea wao amechelewa kufungua kampeni zake, kutokana na matatizo mbalimbali, ikiwamo kufunguliwa kesi ya jinai, mkoani Arusha.

Amesema, “Ndio tunaanza mchakamchaka wa siku takribani 35 za kutafuta uungwaji mkono wa wananchi wa Kinondoni,” ameeleza Leila ambaye alikuwa diwani katika Manispaa za Kinondoni, Ubungo na jiji la Dar es Salaam, kati ya mwaka 2015 na Juni 2020.

Ameongeza; “Ni kweli kuwa tumechelewa kufungua kampeni zetu. Lakini tunaamini kwa aina ya mgombea tulienaye na kukubalika kwa chama chetu, tutashinda uchaguzi huu.”

Kubenea alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Septemba 5mwaka huu, akituhumiwa kwa makosa mawili.

Kwanza, Kubenea alidaiwa kuingia nchini kutokea nchi jirani ya Kenya, bila kupitia Idara ya Uhamiaji; na kutokutoa taarifa ya fedha alizoingia nazo Tanzania.

Mwanasiasa huyu wa upinzani nchini ambaye pia ni mwandishi wa habari alikaa gerezani kwa takribani wiki moja, kabla ya kupata dhamana. 

Aliweka fedha taslimu zinazofikia Sh. 14.5 milioni, kama sehemu ya dhamana yake.

Kubenea alikamatwa akiwa katika gari la abiria, kitokea mpakani mwa Tanzania na Kenya, eneo la Namanga akielekea jijini Arusha. 

Alikutwa na dola za Marekani 8,000 (elfu nane), noti za Kenya 491,700, pamoja na shilingi za Tanzania 71,000.

Ametuhumiwa kuvuka mpaka usio rasmi na kuelekea Nairobi nchini Kenya na kisha kurejea nchini Tanzania bila kutumia mpaka rasmi mnamo tarehe 5 Septemba 2020. 

Amekana madai yote hayo na kesi yake, bado iko mahakamani jijini Arusha.

Akizungumzia kampeni hizo, Leila amesema, mgombea wao amepanga kufanya kampeni zake kwa kwenda nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa na mtu kwa mtu, ili kuwashawishi wananchi wamchague.

Amesema, “Kubenea anafahamika. Anauzika. Anazo sifa zote za kuwa mbunge na kuwakilisha wananchi. Wengi wanamfahamu kutokana na kazi zake kwa jamii na ujasiri wake wa kutetea wananchi. Hivyo basi, tunaamini hatujachelewa.”

Mbali na uzinduzi wa kampeni hizo za kuwania ubunge, mkutano huo utakaohudhuliwa na kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Zuberi Kabwe, unatarajiwa kueleza kile kinachoitwa, “makubaliano ya ushirikiano wa kimya kimya, kati ya ACT- Wazalendo na Chadema.”

Katika siku za karibuni, Zitto amekuwa akieleza kuwa chama chake na Chadema, wamepanga kushirikiana kwa kusimamisha mgombea mmoja wa urais, ambapo ACT- Wazalendo, kitamuunga mkono Tundu Lissu, mgombea urais wa Chadema.

Kuhusu athari za kuchelewa kwa kampeni hizo, Leila anasema, haoni kuwa kuna shida kwa kuwa jimbo la Kinondoni, linafikika kwa urahisi na mgombea wao, bado anaweza kufikia wapigakura kokote waliko.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo anadaiwa kuwa anajivunia rekodi yake iliyotukuka ya kuwakilisha wananchi wa Ubungo bungeni na uwezo wake wa kuangusha vigogo.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Kubenea alimshinda kwa mbali aliyekuwa meya wa jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, aliyegombea nafasi hiyo, kupitia CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,509FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles