24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Kubenea azua kioja bungeni

KubeneaNa Elias Msuya, Dodoma

MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea, jana alizua kioja bungeni huku akidaiwa kuwadhalilisha wanawake alipoomba mwongozo kuhusu hatua ya Jeshi la Polisi kuwakamata wabunge wanawake wa upinzani walipokuwa wakiwatoa katika ukumbi wa Bunge kwa nguvu.

Kubenea alikuwa miongoni mwa wabunge watano wa upinzani waliosimama kuomba mwongozo baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuwasilisha Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano mwaka 2016/17 – 2020/21.

Awali wabunge hao waliomba mwongozo baada ya kipindi cha maswali na majibu saa 4:30, baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, kuwaambia atawasikiliza baadaye.

Baada ya uwasilishaji huo, wabunge hao walisimama, huku Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akitaka kuwa msemaji wa kwanza, lakini Chenge alisema anachukua kwanza majina na akaanza na Kubenea.

Hata hivyo, Kubenea alianza kuzungumza bila kutumia Kanuni, hivyo Chenge alimtaka anukuu kwanza kanuni za Bunge.

Kubenea, ambaye hata hakuwa na kitabu cha Kanuni, alisaidiwa na Lissu kusoma kanuni ya 68(7) kwa kigugumizi, jambo lililowafanya wabunge wa CCM kumzomea:

“Kanuni ya… ya…ya 68(7) (akaisoma kisha akaendelea):

“Juzi bungeni walileta askari wa Bunge na Polisi ambao waliwakamata wanawake, waliwavua nguo za ndani, shanga, waliwadhalilisha kijinsia…” alisema Kubenea huku akikatishwa na zomea zomea za wabunge wa CCM na wengine wakiomba kutoa taarifa.

Hata hivyo, Chenge alisimama na kumtaka Kubenea kukaa na kumwambia kuwa alipaswa kusema ‘mapema hiyo siku… huku pia akimsisitiza kuzisoma kanuni na kuzielewa.

Hata hivyo, Kubenea alisimama na kumtaka Chenge aendelee kutoa hoja yake, lakini alikataliwa.

Baada ya Kubenea, Chenge alimkaribisha Mbunge wa Viti Maalum,u Jesca Kishoa, aliyehoji kuhusu hatua kwa watuhumiwa wa kashfa ya Escrow.

“Hivi karibuni Takukuru ilisema itawachukulia hatua vinara 36 wa Escrow, najua hata wewe Mwenyekiti unahusika, naomba mwongozo wako, ni lini Serikali itatekeleza maazimio manane ya Bunge kuhusu kashfa hiyo, akiwemo Herbinder Singh,” alisema Kishoa.

Akijibu hoja hiyo, Chenge alisema iko nje ya hoja za siku hiyo.

Mbunge mwingine aliyeomba mwongozo alikuwa wa Simanjiro, James Millya, lakini alikataliwa na Chenge.

Baada ya wabunge hao kumaliza ndipo Chenge aliwakaribisha Zitto na Lissu, waliohoji kuhusu hoja ya Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles