30 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

KRISMASI YA MASWALI MAGUMU KIFO CHA FARU JOHN

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akionyeshwa pembe za faru John na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori Robert Mande, (kulia) Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akionyeshwa pembe za faru John na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori Robert Mande, (kulia) Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

NA EVANS MAGEGE,

FARU John, mnyama mwenye misuli mikubwa, jabali na baba wa faru 26 kati ya 37 walioko katika Kreta ya Ngorongoro, kifo chake kwa sasa kinapasua vichwa vya baadhi ya watu.

Faru huyo ambaye sikupata fursa ya kumwona wakati wa uhai wake, ingawa nimewahi kudokezwa sifa zake kwamba alikuwa ndiye mkuu wa himaya ya faru wote, mbabe aliyekosa mpinzani na mwingi wa mitara ndani ya Kreta ya Ngorongoro.

Mbali na jina la John, baadhi waliobahatika kumwona mara kwa mara walipotembelea hifadhini, walimtungia jina la utani kwa kumwita Mfalme Suleiman. Sababu za kumtungia jina hilo la utani ni matendo yake, kwamba muda mwingi alionekana akiwa kwenye juhudi za kutafuta watoto kwa faru majike waliomo ndani ya kreta hiyo ya Ngorongoro.

Utata wa kifo chake ambacho kimetokea miezi takribani tisa tangu wataalamu wa uhifadhi wamhamishe kutoka katika himaya yake ya Ngorongoro, unatazamwa kwa jicho la shaka kuanzia  mchakato wa kumhamisha, taarifa za ugonjwa, matibabu hadi uthibitisho wa kifo chake.

Mazingira ya utata huo yanachagizwa na kitendo cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwahoji wahusika wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kama Faru John ameshakufa ama yuko hai.

Siku chache baada ya Waziri Mkuu kuhitaji taarifa ya ufafanuzi juu ya uhai wa Faru John, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliwasilisha taarifa ya kifo cha Faru John huku akimkabidhi Waziri Mkuu pembe zinazodaiwa kuwa ni za faru huyo.

Katika maelezo yake, Profesa Maghembe  alisema kabla ya kifo cha Faru John, mnyama huyo alianza kuzorota afya yake tangu Julai 10 na akafa Agosti 18, mwaka huu.

Akaenda mbali zaidi na kufafanua sababu za kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti, Serengeti, mkoani Mara.

Alisema sababu kuu ilikuwa ni kuruhusu kuongezeka kwa faru weusi, huku akitoa historia yake kwamba hadi Desemba mwaka 2015, Faru John alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwapo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26, sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumwondoa Faru John ulikuwa ni muhimu, ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘in breeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Profesa Maghembe.

Baada ya Profesa Maghembe kuwasilisha taarifa hiyo, sakata la kifo cha Faru John likachukuwa sura nyingine baada ya Waziri Mkuu kutaka kujua mahali lilipo kaburi la faru huyo na kuagiza lifukuliwe ili mabaki yatumike katika uchunguzi wa vipimo vya vinasaba (DNA) na kwamba uchunguzi huo ulinganishwe na vinasaba vya watoto wake 26 pamoja na pembe walizoziwasilisha kwake.

Agizo hilo la Waziri Mkuu, likaibua mtikisiko mpya na wenye kishindo juu ya sakata la kifo cha Faru John. Kishindo hicho kinatokana na Waziri Mkuu kutangaza kuunda timu mpya ya kuchunguza mazingira ya kifo cha faru huyo, huku akihoji mambo manne yaliyozua utata.

Mambo hayo ni Faru John aliumwa lini, aliumwa ugonjwa gani, daktari gani aliyemtibu na taarifa za matibabu yake zilikuwaje na nani alithibitisha kifo chake.

Maswali hayo ya Waziri Mkuu yametoa taswira ya mtihani mwingine mgumu juu ya utata wa kifo cha Faru John, lakini wakati uchunguzi ukiendelea, gazeti moja la kila siku, lilimkariri mmoja wa wahifadhi wa Sasakwa Grumeti ambaye hakutaka jina lake kutajwa, akieleza utaalamu unaofanyika pindi mnyama anapokufa hifadhini.

Mtaalamu huyo alidai kwamba, kitaalamu wanyama wanaokufa bila kuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya hifadhi, hawazikwi.

“Faru John baada ya kufa aliondolewa pembe zake na kutupwa ili kiwe chakula cha wanyama wengine wanaotegemea mizoga, lakini kuna mifupa yake.”

Akaongeza kwamba faru huyo aliombwa na Grumeti kwenda kupanda faru waliopo katika eneo hilo, hasa baada ya dume aliyekuwapo huko kuuliwa na tembo.

“Baada ya kuonekana kuna haja ya kutafuta dume, ndipo tuliomba kupata faru dume, tukaletewa na baadaye alikufa,” alisema.

Akifafanua hatua zinazochukuliwa baada ya mnyama kufa katika hifadhi, huzikwa au kuchomwa moto pale tu wanapobainika kuwa na magonjwa kama kimeta.

“Kama mnyama ana magonjwa ambayo yanaweza kuambukiza, basi anachomwa moto au hufukiwa lakini kama anakufa kwa ugonjwa wa kawaida huwa anatupwa ili fisi, bweha na wanyama wengine wanaokula mizoga, wale na hii ndiyo ikolojia,” anasema.
Maelezo ya mtaalamu huyo ni sehemu tu ya mengi yanayozungumzwa na yenye tafsiri nyingi juu ya sakata la kifo cha Faru John. Lakini kikubwa tusubiri ripoti nzima ya uchunguzi wa timu teule ya Waziri Mkuu.

Hadi tunaadhimisha leo siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo (Sikukuu ya Krismasi), sakata la kifo cha Faru John tunaweza kusema ndiyo habari kuu iliyosikika kila kona ya mipaka ya nchi.

Inawezekana kabisa kishindo cha sakata hili kikaendelea kubebwa hadi mwisho wa mwaka 2016, kama itakuwa ndivyo, basi sakata la Faru John tutaliita kuwa ndiyo habari kuu ya kufunga mwaka huu.

Mtazamo huo naujenga katika mchanganyiko wa taswira ambazo zimezua maswali mengi tangu faru huyo ahamishwe kwenye himaya yake ya awali iliyokuwapo katika kreta ya Ngorongoro na kupelekwa Sasakwa Singita Grumeti.

Tayari upo mtazamo unaohusisha mazingira ya rushwa kuhusu mchakato wa kumhamisha Faru John kutoka kreta ya Ngorongoro na kumpeleka Hifadhi ya Sasakwa Grumeti ambako mauti yalimkuta.

Mtazamo huo unajazwa nguvu na kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyoitoa Desemba 6, mwaka huu mjini Arusha, alisema asingeweza kuvumilia sakata la faru huyo aliyedai kuwapo taarifa kuwa alihamishwa kwa siri kwenda V.I.P Grumeti Desemba 17, mwaka jana ambako waliahidiwa kupatiwa Sh milioni 200 na tayari walikuwa wamepatiwa Sh milioni 100 kama fedha za awali.

Kwa kuwa uchunguzi wa sakata hilo bado unaendelea, yangu macho na masikio, nasubiri kishindo kingine kitakachojitokeza nyuma ya sakata la Faru John.

KWA MAONI; 0718-814926

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles