Kova: Napenda kuwatumikia Watanzania

0
704

 MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM

KAMISHNA Mstaafu wa Jeshi la Polisi nchini, Suleiman Kova amesema licha ya kuwa amestaafu lakini bado anawapenda Watanzania na anahitaji kuendelea kuwatumikia.

Kova amesema katika kuhakikisha hilo linatimia, ameanzisha Taasisi yake ya Msaada, Majanga na Uokoaji (Sukos Kova) kwa lengo la kuwatumikia na kuwahudumia Watanzania pindi wanapopata shida na majanga mbalimbali.

Akizungumzia jana jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Mtandao wa nguvu ya pamoja ya wanawake (Women Tapo), Kova alisema anaendelea kufanya kazi na Watanzania katika nyanja mbalimbali.

“Nimestaafu ila bado nawapenda Watanzania wenzangu na nataka niwatumikie ndiyo maana nimeanzishaa taasisi ambayo inanifanya niwe karibu na Watanzania wenzangu,” alisema Kova.

Kuhusu mkutano huo alisema suala la wanamke kuwa wajasiriamali si la hiyari bali ni la lazima kwa maendeleo yao na jamii kwa ujumla.

 “Tena mwanamke usiwe mjasiriamali wa kawaida bali ingia kwenye biashara na upambane kwelikweli ili mnufaike katika maisha yenu pamoja na familia.

“Wakati wa kuwategemea wanaume umepitwa na wakati, ni muhimu kina mama wakaelewa wajibu wao katika kuchangia kipato cha maisha kama wanavyofanya wanawake waliopo vijijini,”alisema.

Alisema pamoja na ujasiriamali wanawake wanapaswa kuwa makini na masuala yanayohusiana na afya zao hasa kutokana na magonjwa ya milipuko kama corona na kipundupindu.

Mwenyekiti wa Women Tapo, Stella Mbaga, alisema kutokana na wanawake kuwa na mchango mkubwa katika jamii wamekuwa wakiwaletea vifaa vya kunawa mikono katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

“Msaada huu tumepata kutoka katika Mfuko wa Wanawake hivyo, tukasema tuwaletee ili nanyi muendelee kujikinga na corona,” alisema Stella.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here