Na Malima Lubasha, Serengeti
VIJANA wawili wakazi wa Mtaa wa Morotonga mji wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti wakikabiliwa na kosa la kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja kinyume cha sheria.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aderina Mzalifu, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Faru Mayengela katika kesi hiyo namba 36/2023 akisoma mashtaka aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Simion Tibashimu(38) mzaliwa wa mkoani Kigoma na Laurian James(28) mzaliwa wa Issenye wilayani Serengeti.
Mayengela aliiambia mahakama hiyo kuwa Aprili 6, mwaka huu saa 7.00 usiku washtakiwa walikutwa wakifanya mapenzi ya jinsia moja ndani nyumba ya mshtakiwa wa kwanza.
Mayengela aliiambia mahakama kuwa, baba mwenye nyumba alihisi kuwa katika chumba wanachoishi watuhumiwa kuna jambo lisilo la kawaida aliposikia mgumio linafanyika ndani ya nyumba akamjulisha mwenyekiti wa kitongoji, Bruno Nyawera na kufuatilia na kuita watu wengine walipoingia nda ni walikuta watuhumiwa wakiwa uchi wanaendelea kufanya tendo hilo.
Alisema kufuatia kitendo hicho polisi walijulishwa ambao walifika haraka na kuwachukua hadi kituoni kisha kupelekwa hospitali kwa uchunguzi na daktari alipofanya uchunguzi akathibitisha kuwa ni kweli tendo hilo limefanyika.
Ilielezwa kuwa baada ya kuulizwa mshtakiwa wa pili, Laurian James alikiri kuwa ni kweli wamefanya tendo hilo na Aprili 17, mwaka huu walifikishwa mahakamani kusomewa maelezo ya awali ambapo walikana hivyo kurudishwa rumande hadi Juni mosi, 2023 waliendelea kukana.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa utaita mashahidi 13 ambapo Hakimu Mzalifu alisema dhama iko wazi kwa washtakiwa wote.
Hata hivyo, washtakiwa walikosa wadhamini na kurudishwa rumande hadi Juni 15, mwaka huu kesi itakapo tajwa tena.