Na KULWA MZEE
-DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA, Hamis Almas (51), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia fedha na kutakatisha Dola za Marekani 251,600 maeneo ya ofisi za Pride Come Limited.
Mshtakiwa huyo alipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Salimu Ally.
Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alidai, mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya Agosti 17 mwaka jana na Aprili 30 mwaka huu, Dar es Salaam.
Alidai mshtakiwa huyo akiwa katika ofisi za Pride Come Limited, alijipatia dola 251,600 kutoka kwa Joan Blanch Domenech ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Spove Nuts Company.
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo akijaribu kudanganya kuwa Kampuni yake Pride Come Limited, ingesafirisha tani 6.8 za korosho kwenda nchini Hispania kwa niaba ya Kampuni ya Spove Nuts wakati akijua si kweli.
Katika shtakà la pili, mshtakiwa huyo anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha kwa kuzipokea kupitia akaunti yake iliyopo katika benki ya Equity wakati akijua fedha hizo zimetokana na kosa la udanganyifu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu alimfahamisha mshtakiwa kwamba hatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Wankyo alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi iliahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu itakapotajwa.