24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Korosho za Pwani kununuliwa wiki ijayo

Na GUSTAPHU HAULE, PWANI

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, ametoa siku nne kwa vyama vya ushirika vilivyopo mkoani humu kuhakikisha wanaziondoa korosho katika maghala yao na kuzipeleka katika maghala makuu matatu yaliyoelekezwa na Serikali likiwamo la Kibiti, Mkuranga na Tanita kabla hazijaanza kununuliwa wiki ijayo.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipozungumza na viongozi wa idara za mkoa na wilaya baada ya kutembelea ghala la kuhifadhi korosho na kiwanda cha kubangulia zao hilo kilichopo eneo la Tanita, Halmashauri ya Mji wa Kibaha.

Alisema hatua hiyo ni mchakato wa Serikali kuanza kununua korosho kwa njia rahisi na salama ili kuhakikisha wakulima wanapata stahiki yao kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli ameagiza.

Alisema Pwani ina vyama vya ushirika zaidi ya 80 na hadi sasa wamehifadhi korosho hizo katika maghala yao hivyo huu ni wakati mwafaka wa kuhakikisha zinahamishiwa katika maghala makuu ya Serikali ili ununuzi ufanyike mara moja.

“Wenzetu Mtwara, Lindi na Ruvuma tayari wanaendelea kuuza korosho kama ambavyo mnasikia, lakini kwa upande wa Pwani tunaanza kununua korosho wiki ijayo kwa hiyo ili kuleta urahisi lazima korosho hizo zipelekwe katika maghala makuu matatu yaliyopangwa na Serikali,” alisema.

Ndikilo alisema Ghala la Tanita lina uwezo wa kuhifadhi tani 2,000, Kibiti tani 5,500 na Mkuranga tani 10,000.

Alisema baada ya korosho hizo kukusanywa katika maghala hayo, wataalamu watazipima kulingana na mwongozo wa Serikali na kisha mkulima kulipwa fedha zake bila usumbufu na baadaye magari ya jeshi yatakuja kuzisomba kama inavyofanyika Mtwara.

Alivitaka vyama hivyo kuendesha mchakato huo kwa haraka ili kuhakikisha wakulima wanafaidika kwa kuuza korosho zao kwa wakati kwa kuwa kuchelewesha kutachelewesha wakulima kulipwa.

“Sasa hivi magari ya jeshi hayatatumika katika kusomba korosho kutoka katika vyama vya ushirika kwa kuwa bado korosho ipo mikononi mwao, kwa hiyo wanalazimika kuzipeleka korosho zao katika maghala makuu yaliyoelekezwa na Serikali na zikishafika katika maghala hayo tayari korosho hizo zinakuwa mali ya Serikali na hapo ndipo magari ya jeshi yatakapoingia kazini,” alisema.

Kwa upande wake, Mpimaji wa korosho kutoka Ghala la Tanita, Joseph Malekano, alisema korosho zinapofika ghalani hapo hatua ya kwanza wanayofanya ni kukata gunia kwa gunia ili kuangalia ubora wake.

Alisema kila mkulima anapata haki yake kulingana na ubora wa korosho zake kwa sababu zilizo bora zinaanzia kiwango cha gredi 48 na kwenda juu wakati 47 kwenda chini zinakuwa chini ya kiwango.

Aliwataka wakulima kuhakikisha wanaanika korosho zao vizuri na kuzichambua ipasavyo ili kuepuka usumbufu wa kuzirudisha kwa sababu Serikali inataka wote wapate haki zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles