Korea Kusini yasema Kim yuko salama kiafya

0
662
KIONGOZI wa Korea Kaskazini Kim Jong Un

SEOUL, KOREA KUSINI

KIONGOZI wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameripotiwa kuwa katika hali nzuri ya kiafya.

Moon Chung In ambaye ni mmoja wa washauri wa usalama wa Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in  amesema kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amekuwa katika mji wa Wonsana tangu Aprili 13 na hajafanya ziara nyingi kama ilivyo ada yake.

Alisema kuwa Kim yuko salama kinyume na uvumi kuwa amefariki dunia.

Hata hivyo, picha za satelaiti zimeonyesha treni inayodhaniwa kuwa ni ya kiongozi huyo ikiwa imeegeshwa kwenye makazi yake yaliyoko pwani ya mashariki mwa nchi hiyo tangu wiki iliyopita.

Picha hizo za satelaiti zilizochapishwa na tovuti ya 38 North ambayo ni maalumu kwa masomo kuhusu Korea Kaskazini, hata hivyo hazielezi chochote kuhusu matatizo ya kiafya ya Kim, lakini zinaendeleza taarifa za kiintelijensia za Korea Kusini kwamba yuko nje ya mji mkuu, Pyongyang.

Uvumi kuhusu hali yake ya kiafya, kwa sehemu kubwa umesababishwa na kutoonekana kwake hadharani kwa kipindi kirefu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here