Na LEONARD MANG’OHA
Serikali za Tanzania na Korea zinatarajia kushirikiana kutekeleza miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuondoa maji taka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la ushirikiano katika masuala ya mazingira baina ya Tanzania na Korea, lililofanyika juzi Dar es Salaam, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, alisema mradi huo pia utahusisha uondoaji wa taka ngumu, kama vile chupa za plastiki.
“Wenzetu tumeona wanao uwezo mkubwa katika uhifadhi wa mazingira na wanaweza kuzichakata taka ngumu na kuzitumia kwa matumizi mengine.
“Ukipata nafasi ya kushirikiana na nchi iliyoendelea na inatumia teknolojia kuhifadhi mazingira, ni jambo la faraja kwa sababu linatoa nafasi kwetu kujifunza wanavyofanya,” alisema Lwenge.
Alisema hapo kabla Tanzania haikuwa na mkakati wa kuyaondoa maji taka, si tu katika Jiji la Dar es Salaam, bali hata katika miji mingine nchini.
Aliongeza kuwa, maji yatakayoondolewa yanaweza kusafishwa na kutumika katika shughuli mbalimbali, ikiwamo kupooza mitambo inayotumika kuendesha viwanda.
Akizungumza kuhusu upatikanaji wa maji safi na ya uhakika, alisema hadi kufikia mwaka 2020, kati ya asilimia 85 na 95 ya wananchi wanatarajiwa kupata maji ya uhakika kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano 2016/2021.
Naye Balozi wa Korea nchini, Son Geum-young, alisema Serikali yao itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kufungua ubalozi nchini humo mwaka huu.