26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

kondom feki, kutoangalia ubora kunavyochangia maambukizi VVU

AVELINE KITOMARY 

KONDOM ni mipira inayotumika wakati wa kujamiiana kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwamo Virusi vya Ukimwi (VVU), kisonono, kaswende na magonjwa mengine.

Kondom za kiume ndio zinazotumika kwa wingi ambapo licha ya kujikinga na maambukizi pia hutumika kujikinga na mimba zisizo tarajiwa.

Hata hivyo, matumizi ya mipira hiyo kwa sasa yamekuwa wazi zaidi tofauti na zamani ambapo watu wengi walikuwa wakiona aibu kununua.

Katika vituo vya afya na nyumba za starehe imekuwa ikitolewa bure, hii ni kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanazuiwa.

Mara nyingi elimu imekuwa ikitolewa kwa vijana kuwahamasisha au kujua umuhimu wa kutumia bidhaa hizo katika kujikinga na magonjwa ya zinaa.

Ubora wa mipira hiyo na njia za matumizi sahihi ina nafasi kubwa katika kuwasaidia watumiaji kwani licha ya kuwa ni biashara inayowaingizia watu kipato, pia hulinda afya za watu.

Endapo mipira hiyo itatumika kwa usahihi inauwezo wa kukinga maambukizi kwa asilimia 90 hadi 95.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imekuwa mstari wa mbele kudhibiti ubora, usalama, ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Katika kuhakikisha ubora wa kondom unazingatiwa, mamlaka hiyo imekuwa ikifuata hatua zote za kupima ubora wake kwa kutumia mashine za kisasa.

Kuna hatua ya kupima kiasi cha mafuta, matundu, kiwango cha kustahimili msuguano na vipimo vya urefu.

Viwango hivyo vyote hupimwa na kuhakikiwa na wataalamu wenye mafunzo ya kutosha na uzoefu wa kazi hizo katika maabara.

Hivyo, baada ya kuonekana kutokuwa na kasoro yoyote ndipo toleo hilo la kondom huruhusiwa kusambaa mitaani.

JINSI YA KUPIMA KONDOM

Mchunguzi wa Vifaa Tiba na Vitendanishi wa TMDA, Samson Mwambele, anasema mashine zinazotumika kupimia matundu inayoitwa kwa kitaalamu ‘Visual leak Tester’ inaweza kubaini hata tundu dogo kwenye mipira.

“Inauwezo wa kupima na kugundua shida iliyopo kwenye kondom, ikishavishwa hapa mashine inaruhusu kondom iingie kwenye maji yanayosaidia kuonyesha tatizo.

“Kama kuna tundu lolote dogo unaweza kuona, lakini sio kwamba tukiangalia hapa ndio tunaridhika hapana, tutahamishia sehemu ya kubana kama itakuwa na kitobo utaona maji yakitoka.

“Mashine hii pia hutumika kuangalia gloves, hapa kunasehemu nyingine tofauti na ya kondom hata kiasi cha maji kitakachongia kwenye glovu haitafanana,” anasema.

Anasema kama kondom ikiingia hewa ya oksijeni, mafuta yaliyoko yanatoka na kusababisha kupasuka hivyo haitakuwa salama kwa matumizi.

Anataja mashine inayotumika kupima mafuta kuwa kitaalamu inaitwa electric leak tester.

 “Kondom ikiwa na kitobo huingiza oksijeni ambayo huiharibu, kwanza mafuta yanatoka, pia itakuwa rahisi kupasuka hivyo wakati wa matumizi haitakuwa salama.

Anabainisha kuwa mafuta yaliyoko kwenye kondom hayana athari yoyote kwa afya ya binadamu.

AINA TANO ZAONDOLEWA SOKONI 

Katika kuhakikisha udhibiti wa vifaa bandia sokoni unafanikiwa, TMDA kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iliondoa sokoni takribani paketi za kondomu 17,076 baada ya kushindwa kukidhi vigezo vinavyotakiwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa Tiba, Akida Khea, anasema bidhaa hizo zilizoondolewa ni zile feki ambazo hazikidhi matakwa ya viwango zinazoweza kuwa na madhara na nyingine ni zile ambazo zilikuwa zikiuzwa kwa kutumia jina la mtu mwingine.

“Kwanza kabla ya kondomu kuingia sokoni huwa tunapima ubora wake kama kiwango cha mafuta, ustahimili wa matumizi na urefu wake hivyo endapo tukipima na tukakuta haina vigezo tunaizuia kuingia sokoni.

“Pia licha ya hiyo huwa tunafanya ukaguzi katika maduka mbalimbali hapa nchini kwa kuangalia ubora wa bidhaa zilizopo na kama muda wa matumizi ya bidhaa hizo hazijaisha hivyo tuko makini katika udhibiti wa usalama wa ubora wa bidhaa,” anaeleza Khea.

Khea anasema kondomu zilizoondolewa sokoni ni takribani aina tano ambazo ni Life Guard, Ultimate, Maximum Classic, Prudence na Chishango.

MADHARA YA KONDOM FEKI 

Khea anasema kuwa yapo madhara makubwa kiafya endapo mtu atatumia kondom ambazo hazijathibishwa usalama  na ubora wake.

Anathibitisha kuwa madhara yanayotokana na matumizi ya kondom zisizo na ubora ni kuambukizwa VVU na magonjwa mengine ya zinaa.

Kutokana na hilo, anasema ni bora watumiaji kuhakikisha ubora wa kondom wanazozitumia ili kuepusha madhara hayo.

“TMDA kwa sasa imebaki na jukumu la kulinda afya ya jamii  kwa kudhibiti  ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi  hivyo bidhaa kama kondom isipokubalika tunasema haina ubora kwa matumizi hapa nchini.

“Na kama kondom ikithibitishwa kuwa haina ubora kama itatumika haitaweza kumlinda mtumiaji kwa magonjwa ya kujamiiana na Ukimwi  hivyo kondom kama hizo ni hatari kwa afya.

“Huwa tukigundua kuwa kondom haina ubora tunaiondoa haraka kwenye soko, ni vizuri jamii wakatumia kondom zilizothibitishwa na ni vizuri kutoa taarifa endapo watakutana na kondom zisizo na ubora,” anaeleza Khea.

ASHAURI WA UMAKINI 

Khea anatoa wito kwa jamii kuangalia mwisho wa matumizi ya bidhaa (Expire date) hasa kwa bidhaa kama kondom ili kulinda afya zao wenyewe. 

“Kama una bidhaa ambazo huna uhakikia nazo ni vizuri ukatoa taarifa TMDA ili tukafanyie uchunguzi na tubaini usalama na ubora wake,” anashauri Khea.
Vijana ni walengewa wa kundi la matumizi ya bidhaa za kondom kwani ndio wanaozitumia kuliko kundi lingine.

Kutokana na maoni ya vijana mbalimbali waliohojiwa na gazeti la MTANZANIA  wengi wao wamesema hawana kabisa desturi ya kuangalia mwisho wa matumizi wa bidhaa za kondom(expire date).

Sababu zilizotolewa na vijana wengi ni   pamoja na wengine  kuweka bidhaa hizo  ndani kwa muda mrefu hivyo endapo ikitokea bahati ya kutumia ni vyema wasipoteze muda.

Na wengine wanasema wanashindwa kuwa makini katika hilo kutokana na shauku kubwa waliyonayo ya matamanio ya kimwili. 

Mmoja  wa Mkazi wa Ubongo jijini Dar es Salaam  aliyejitambulisha kwa jina la John anasema kuwa  ni kweli wanaume wengi hawana desturi ya kuangali mwisho wa matumizi ya kondom kutokana na sababu kama hizo lakini zipo zingine zaidi. 

“Wengine utakuta anapofika dukani akakuta watu ni wengi anakuwa anaona aibu kuikagua badala yake anapewa tu kwa kufungiwa kwenye gazeti  na kuodoka nayo hivyo hatajua kama muda wake wa matumizi umeaisha,”anaeleza John.

Naye Fatuma Abdallah, sio jina lake halisia anasema kuwa hata wanawake hawana desturi ya kuangalia mwisho wa matumizi ya kondom kutokana na kuona kama suala hilo linawahusu wanaume zaidi.

“Sidhani kama wanawake walinafikiariaga kuhusu hilo wengi tunaona linawahusu wanaume zaidi kwa sababu wao ndio wanaenda kununua na wakati mwingine wanavaa wenyewe.

“Mimi binafsi niwe mkweli sijawahi kufikiria kuangalia ‘expire date’ ya kondom, kuanzia sasa nitaanza kuangali  pia nitamshawishi hata mpenzi wangu awe anaangalia hilo,” anasisitiza Fatuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles