28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Kondoa, Mkalama vinara ukeketaji

munuoNa Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

WILAYA ya Mkalama mkoani Singida na Kondoa mkoani Dodoma zinaongoza kitaifa kwa vitendo vya ukeketaji wanawake na wasichana, huku Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Arusha, Tabora, Mwanza na Zanzibar zikiongoza kwakuwa na mimba na ndoa za utotoni.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) mwaka jana, mikoa inayofutia kwa kuwa na idadi kubwa ya vitendo vya ukeketaji ni pamoja na Mara, Dodoma, Manyara na Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi kutoka Tamwa, Gladness Munuo, alisema wajawazito zaidi ya 2,265 waliofika katika vituo mbalimbali vya matibabu wilayani Mkalama walikeketwa.

Alisema utafiti huo pia umeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 39.9 ya wajawazito waliofika kwenye vituo vya matibabu Wilaya ya Kondoa walibainika kukeketwa.

“Utafiti tuliofanya mwaka jana katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mkalama na Kondoa umebaini kuwa wilaya hizo zinaongoza kwa vitendo vya ukeketaji,” alisema Munuo.

Aliongeza kuwa wananchi wanafanya vitendo hivyo kwa kushirikiana na mangariba ambao wamekuwa na mbinu mbalimbali ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa kwa siri.

Alisema miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na kuwahamisha wasichana wanaotakiwa kukeketwa na kuwapeleka kwenye vijiji vya jirani.

Alitolea mfano wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambapo mangariba wamekuwa wakiwapaka unga usoni wasichana wanaotakiwa kukeketwa ili ionekane kwamba hawafanyiwi vitendo hivyo wakati si kweli.

“Jamii hizo zinapaswa kuelimishwa na kuamini kwamba vitendo hivyo ni vya udhalilishaji na vinapaswa kukemewa kwa nguvu zote,” alisema Munuo.

Alisema mila na desturi potofu ambazo zimechangia kuwashawishi wazazi au walezi kukeketa wasichana hao, hazipaswi kuungwa mkono kwa sababu zinachangia kuwakandamiza wasichana na kuwasababishia matatizo.

Munuo alisema umasikini uliokithiri, kukosekana kwa uelewa juu ya haki za binadamu, mfumo dume, ukosefu wa sera imara pamoja na sheria dhaifu, vimechangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Alisema ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa, mangariba watakaobainika kuhusika wanapaswa kufikishwa kwenye mikono ya sheria na kuchukuliwa hatua kali ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

Kuhusu mimba na ndoa za utotoni, Munuo alisema kuwa mikoa ya Pemba, wasichana 240 walipata mimba wakati Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga, wasichana 605 ambao ni sawa na asilimia 47.47 kati ya wasichana 1,150 hawakumaliza shule ya sekondari kwa sababu ya ndoa za utotoni.

Alisema katika Wilaya ya Bagamoyo wasichana 12 wa shule waliripotiwa kupata mimba ndani ya miezi sita.

Munuo alisema ndoa hizo zinatokana na wazazi au ndugu wa wasichana hao kuwa na tamaa ya kupata mahari, jambo ambalo limechangia kuwaozesha wakiwa wadogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles