26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kodi za nyumba, ada maumivu

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

MFUMUKO wa bei umeripotiwa kwa mara ya kwanza tangu kuingia kwa Januari mwaka huu, huku sekta ya makazi na elimu zikionekana kuathirika zaidi kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei za kodi za pango kwa wapangaji na kuongezeka kwa ada kwa shule za sekondari za binafsi.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa Januari, 2020, kumekuwa na ongezeko la mfumuko wa bei katika baadhi ya bidhaa zisizokuwa za chakula, lakini zaidi katika eneo la kodi za pango za nyumba na ada za shule kwa shule binafsi.

“Vitu visivyo vya chakula vilivyochangia ongezeko hilo ni pamoja na kodi halisi inayolipwa na wapangaji ambayo imeripotiwa kuongezeka kwa hadi asilimia 2.3, petroli kwa asilimia 1.4 na ada ya shule kwa shule za msingi zimeongezeka kwa asilimia 1.9 na kwa shule za sekondari za binafsi imeongezeka kwa asilimia 1.8,” ilieleza taarifa hiyo ya NBS.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mtakwimu Mkuu wa NBS, Albina Chuwa Februari 10, mwaka huu, ilieleza kuwa fahirisi ya jumla ya mfumuko wa bei imeongezeka hadi 117.60 Januari, 2020 kutoka 117.10 iliyorekodiwa Desemba, 2019.

“Kuongezeka kwa faharisi kwa jumla kunahusishwa na ongezeko la bei ya vyakula na vitu visivyo vya chakula.

“Baadhi ya vitu vya chakula vilivyochangia ongezeko kama hilo ni pamoja na samaki kwa asilimia 1.7, mboga kwa asilimia 4.1, maharagwe kwa asilimia 2.2, mihogo kwa asilimia 2.4 na ndizi za kupika kwa asilimia 1.7,” ilieleza ripoti hiyo.

Ilieleza kuwa kwa upande mwingine, mabadiliko ya fahirisi ya bei ya miezi 12 kwa bidhaa zisizo za chakula katika mwezi wa Januari, 2020 zimeongezeka kidogo hadi asilimia 2.4 kutoka asilimia 2.3 zilizorekodiwa Desemba, 2019.

“Kiwango cha mfumuko wa bei ukiondoa chakula na nishati, kiwango cha mfumuko wa bei ambao haujumuishi chakula na nishati kwa mwezi wa Januari, 2020 umetulia katika asilimia 2.1. kama ilivyorekodiwa mwezi Desemba, 2019.

“Mwelekeo wa Mfumuko wa Bei (NCPI) ulitumika kulinganisha aina hii ya kiwango cha mfumuko wa bei bila kuhusisha chakula kinachotumiwa nyumbani na migahawani, petroli, dizeli, gesi, mafuta ya taa, mkaa, kuni na umeme,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo ya NBS.

Ilieleza kutohusisha pia chakula na nishati ambavyo ni vitu muhimu na tete zaidi katika kupata jumla ya mfumuko wa bei ili kutoa takwimu ya kiwango cha mfumuko wa bei iliyo bora kwa watunga sera.

Katika ripoti hiyo, pia iliainisha kuwa kielelezo cha bei ya matumizi ya kitaifa kutoka Desemba, 2019 hadi Januari, 2020 iliongezeka kwa asilimia 0.4 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.6 iliyorekodiwa kutoka Novemba, 2019 hadi Desemba, 2019, hatua inayoonyesha kushuka kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa.

Hiyo inatokana na utafiti uliofanywa kuhusu viwango vya mfumuko wa bei kwa kichwa ambao mara nyingi hupungua kiwango cha mfumko wa bei wakati vitu vyote kwenye kikapu cha Mwelekeo wa Mfumuko wa Bei (CPI) vilivyojumuishwa vimejumuishwa.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa kichwa unaelezea kuwa kasi ya mabadiliko ya bei kwa bidhaa kwa mwaka uliomalizika Januari, 2020 imepungua ikilinganishwa na kasi ya mabadiliko ya bei iliyorekodiwa kwa mwaka uliomalizika Desemba, 2019,” imeeleza ripoti hiyo.

Ilieleza kuwa kwa uwiano wa kila mwaka, fahirisi ya jumla iliongezeka hadi 117.60 Januari, 2020 kutoka 113.38 zilizorekodiwa Januari, 2019.

“Lakini inaonekana kumekuwa na ahueni katika viwango vya bei ya uingizaji wa chakula na bidhaa zisizo za chakula, pamoja na vinywaji visivyo vya pombe. Kwa mwezi wa Januari, 2020 vimepungua hadi asilimia 5.7 kutoka asilimia 6.3 iliyorekodiwa katika Desemba, 2019,” ilieleza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha mfumuko wa bei wa kila mwaka kwa chakula kinachotumiwa nyumbani na mbali na nyumbani kwa mwezi wa Januari, 2020 pia kimepungua hadi asilimia 6.4 kutoka asilimia 6.9 iliyorekodiwa mwezi Desemba, 2019.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles