29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kodi ya VAT kujadiliwa na wadau wa utalii Arusha

gamboNa JANETH MUSHI-ARUSHA

WADAU zaidi ya 150 kutoka sekta ya utalii mkoani Arusha, wanatarajiwa kujadili maendeleo ya sekta hiyo ikiwamo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika shughuli za utalii.

Serikali ilifuta msahama wa kodi katika masuala yote yanayohusiana na utalii baada ya Bunge kutunga sheria mpya ya kodi ya mwaka 2016 na hivyo kusababisha wadau wa utalii nchini kupinga sheria hiyo.

Akizungumza mjini hapa jana juu ya kufanyika kwa mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
Gambo alisema mkutano huo ambao umefadhiliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), unatarajiwa kujadili hali ya maendeleo ya utalii ya mkoa, fursa zilizopo pamoja na mafanikio.

Alizitaja mada nyingine zitakazojadiliwa ni pamoja na changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma mbalimbali za utalii pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Alisema Waziri Maghembe ataongoza mkutano huo wa siku moja ambapo wadau wengine ni pamoja na Bodi  ya Utalii (TTB), Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), wamiliki wa hoteli, kampuni za kitalii na wadau wengine wakiwemo viongozi wa Serikali.

“Tunataka tujitathmini baada ya kuwapo kwa kodi ya VAT katika shughuli za utalii kwani kumekuwapo na maneno mengi ikiwamo madai ya kupungua kwa idadi ya watalii.

“Tumeona sisi kama mkoa tuite wadau wote wa utalii tukutane kwa pamoja na kujadiliana masuala ya kukuza na kuendeleza utalii hasa kwa maendeleo ya Jiji letu,” alisema Gambo.

Mkuu wa mkoa huyo alisema mkutano kama huo wa wadau wa utalii ulifanyika mwaka 2012, hivyo kwa muda mrefu wadau hao hawajakutana kwa kipindi kirefu kujadili kuhusu sekta hiyo.

Alisema Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ambapo kwa kipindi cha mwaka jana watalii walioingia nchini walikuwa ni 1,137,182 na waliweza kuliingizia taifa Dola za Marekani bilioni 1.9, huku kati ya watalii hao asilimia 80 wakitembelea vivutio vya Mkoa wa Arusha.

Akizungumzia suala la utalii wa ndani, kiongozi huyo alisema kwa kushirikiana na wadau wengine wataendelea kutoa elimu ya kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles