KODI YA MAJENGO KUWA CHANZO KIKUU MAPATO YA NDANI

0
1005
MENEJA WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI WA TRA- GABRIEL MWANGOSI

NA KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


SERIKALI iliipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kusimamia na kukusanya Kodi ya Majengo kuanzia Julai mosi mwaka 2016.

Awali kabla ya jukumu hilo kuhamishiwa kwa TRA, halmashauri ndizo zilikuwa zikikusanya kodi ya majengo ambapo wananchi walikuwa wakienda kulipia katika ofisi za Serikali za Mitaa na baadaye kodi hizo kupelekwa halmashauri.

Majukumu hayo kwa TRA yalitokana na mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Majengo namba 2 sura ya 289, Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa na. 9 sura ya 290 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na 9 sura ya 399 ambayo imeainishwa kwenye sheria ya Fedha ya mwaka 2016.

Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Gabriel Mwangosi, anasema kuwa kwa mujibu wa sheria, kodi ya majengo ni tozo ambayo hutozwa majengo au nyumba ambazo zimekamilika na watu wanaishi.

Anasema sambamba na hayo pia ziwe zinamilikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na sheria nyingine za nchi na pia ziwe zimefanyiwa uthamini.

Anasema uthamini unaomaanishwa katika kodi ya majengo ni hali ya kujua thamani ya jengo au nyumba kwa ajili ya kutozwa kodi ya majengo na kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa ndizo zilizopewa jukumu la kuchagua wathamini ambao hutayarisha orodha ya majengo au nyumba katika maeneo ya miji, manispaa na majiji.

“TRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa tumeajiri wathamini ambao ndio watayarishaji wa orodha au jedwali kwa ajili ya kutoza kodi ya majengo katika mamlaka za Serikali za mitaa husika lakini wathamini hao ni lazima wawe amesajiliwa na sheria ya wathamini wa majengo kama mthamini.

“Wakati wa uthamini, mthamini atahitaji jina la mmiliki, anuani, namba ya kiwanja au jengo, hati ya kiwanja kwa maeneo yaliyopimwa au leseni ya makazi kwa maeneo ambayo hayajapimwa, ankara za maji au umeme kwa uthibitisho wa mmiliki wa nyumba au jengo.

“Pia utatakiwa mwaka ambao jengo lilijengwa, michoro iliyotumika kwenye ujenzi wa majengo makubwa, matumizi ya jengo husika iwapo ni makazi au biashara pamoja na kupimwa kwa eneo la jengo  ili kupata eneo lake,” anasema Mwangosi.

Anasema wamiliki wa nyumba watatambuliwa kwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kwamba TRA imetengeneza mfumo wa kukusanya kodi ya majengo ambao una uwezo wa kuandaa na kutoa hati ya madai ambayo itamwezesha mteja kujua kodi anayotakiwa kulipa na atailipia katika benki ya biashara ambayo imeunganishwa na mfumo wa malipo ya kodi.

Mwangosi anasema kutokana na sheria zilizotungwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa husika, tozo za kodi ya majengo zinatofautiana na kwamba hutozwa mara moja kwa mwaka ambapo mwaka wa Serikali unaanza Julai ya kila mwaka na kuishia Juni ya mwaka unaofuata.

Anasema kwa mujibu wa sheria, baada ya muda wa kulipia kodi za majengo kupita, wamiliki wa nyumba au jengo watalipa na riba na adhabu ikiwa ni pamoja na taratibu za kisheria kutumia ili kuzikusanya.

Anasema kwa mmiliki au mwakilishi aliyechaguliwa kisheria na mwenye nyumba au jengo ambaye atakuwa hajaridhishwa na kodi atakayokuwa ametozwa, anaruhusiwa kuweka pingamizi kwa mamlaka za utozaji kodi ya majengo zilizowekwa kisheria katika eneo husika.

Mwangosi anasema kuwa kwa mujibu wa sheria, nyumba zilizosamehewa kodi ni zile zinazotumika kwa matumizi ya rais, majengo yanayomilikiwa na kutumiwa na Serikali kwa matumizi ya umma, majengo yanayomilikiwa na taasisi za dini lakini hayatumiki na shughuli za biashara au kiuchumi kwa kujipatia faida, maktaba za umma na majengo ya makumbusho, makaburi na nyumba za kuteketezea maiti na  majengo ya shughuli za reli.

Anasema misamaha mingine imetokewa kwa majengo ya kuongozea ndege za umma na majeshi, majengo yenye maeneo ya viwanja vya michezo vinavyotumika kwa matumizi ya taasisi za elimu, majengo yanayomilikiwa na asasi zisizo za Serikali yasiyotumika kwa shughuli za biashara au kujipatia kipato pamoja na  majengo yanayomilikiwa na Serikali, taasisi za Serikali na taasisi nyingine za aina hiyo yasiyotumika kwa shughuli za biashara au kujipatia kipato.

Anaongeza kuwa, misamaha mingine hutolewa kwa nyumba au majengo ya yanayomilikiwa na Serikali za mitaa na taasisi zake ambazo hazitumiki kwa shughuli za biashara au kujipatia kipato pamoja na majengo yote ambayo waziri mwenye dhamana ataamua kuyatolea matangazo kwenye gazeti la Serikali.

“Kwa upande wa mzee mwenye umri zaidi ya miaka 60 na anamiliki zaidi ya nyumba moja, atasamehewa moja nyingine atalipia lakini nyumba anayoishi mlemavu asiyekuwa na kipato chochote pia atasamehewa kodi,” anasema Mwangosi.

Mwangosi anasema kodi ya majengo inatozwa kwa majengo tu na kwamba nyumba au majengo ambayo hayatatozwa kodi ni yale ambayo yatakuwa hayajakamilika ujenzi wake pamoja na majengo yanayomilikiwa na taasisi za dini lakini  yanatumika kufanya ibada.

Anasema hata kama mtu anamiliki nyumba zaidi ya moja katika kiwanja kimoja, zote atatakiwa kuzilipia na kwamba kama ni nyumba za udongo atatakiwa kuzilipia iwapo atakuwa amezipiga plasta kutokana na kuwa ameshazithaminisha  lakini kama hazina plasta hizo hazilipiwi.

Anasema ili kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa, TRA imejipanga kuhakikisha inafanya uthamini wa majengo ili kuwa na viwango ambavyo ni rafiki, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za ukusanyaji wa kodi ya majengo, kuelimisha jamii kuhusu ulipaji wa kodi ya majengo, kushughulikia pingamizi za kodi ya majengo katika muda mwafaka pamoja na kuboresha daftari la orodha ya uthamini ili kuwa na takwimu sahihi.

Uelewa wa wananchi

Deus Lymo mkazi wa Gongolamboto, anasema suala la kodi ya majengo hajui anatakiwa kulipa kiasi gani na hata alipofutailia katika ofisi ya Kata ya Gongolamboto, aliambiwa fomu yake haikuwepo.

“Mimi nilienda kwenye ofisi za kata kuulizia fomu yangu, mtendaji aliniambia haioni nikaamua kuondoka,” anasema Lymo.

Naye Nusura Mudirkat mkazi wa Kimara Baruti, anasema katika eneo hawakupelekewa barua na kwamba anaendelea kusubiri hadi atakapopelekewa ndipo atakapoenda kulipa.

Anasema eneo la kiwanja chake hakijapimwa na kwamba hana uhakika kama sheria itamtaka kulipa kodi ya majengo au asilipe.

“Kuna wenzetu nasikia walishapelekewa barua lakini mimi sijapata na eneo langu halijapimwa, hivyo naendelea kusubiri nione kama nitaletewa barua au sitaletewa,” anasema Nusura.

Naye John Daud mkazi wa Kimara Matete, anasema utaratibu wa zamani ulikuwa wakilipia katika ofisi za Serikali ya Mtaa ambako baada ya malipo hupewa risiti, lakini tangu jukumu hilo lihamishiwe TRA bado wananchi hawajaelewa utaratibu uliopo.

Anasema kulipa kodi ni uzalendo na kwamba watu wanatakiwa kulipa bila kushurutishwa lakini changamoto iliyopo ni uelewa mdogo wa watu kuhusiana na masuala ya kodi.

“Tunasikia kuna barua zimetolewa kwa baadhi ya watu, lakini wengine hatujapata sasa sijui itakuwaje maana siku zenyewe ndio zimeisha ila hata elimu ya kodi bado ni tatizo kwa wananchi, hali inayochangia watu kukwepa bila sababu yoyote ya msingi,” anasema Daud.

Serikali ya Mtaa wa Baruti

Susan Benjamini ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kimara Baruti, anasema watu wameitikia wito kwa kufika katika ofisi hiyo na kuchukua barua zao, lakini changamoto iliyojitokeza ni kwamba wengi walikuwa wakikuta majina yao hayapo huku wengine majina yakikosewa.

Anasema awali kabla ya jukumu hili kuhamishiwa kwa TRA, lilikuwa likisimamiwa na halmashauri ambayo ilikuwa ikitoa asilimia saba ya mapato yalikuwa yakikusanywa kwa ofisi za Serikali ya mitaa kwa ajili ya kuwalipa wajumbe motisha kutokana na kazi waliyokuwa wakifanya ya kuwasambaza kwa wanachi wao katika kila nyumba barua za kuwakumbusha kulipa kodi ya majengo.

Anasema hata hivyo zoezi hili lilipata changamoto baada ya halmashauri kusitisha utoaji wa ile asilimia saba kwa ajili ya wajumbe, hali iliyochangia kuwafanya wajumbe washindwe kujitoa kusambazia wanachi wao barua hadi leo.

“Changamoto hii bado ipo kutokana na kuwa TRA bado haijaweka utaratibu wowote, hivyo wajumbe wameshindwa kuendelea kujitolea na badala yake tunachofanya sisi ni kuwaelekeza kwa wananchi wote wanaofika hapa na kukuta majina yao yamekosewa au kukuta barua zao hazipo kuenda katika ofisi za TRA kwa ajili ya kupata maelekezo zaidi,” anasema Susan.

Taasisi za dini

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka, anasema majengo yanayotumika kama nyumba za ibada ni sahihi kutokutozwa kodi lakini kwa yale yanayotumika kwa biashara ili kuiingizia taasisi kipato yanastahili kulipa kodi.

Anasema hakuna kiongozi yeyote wa dini anayeweza kupingana na Serikali kuhusu kulipa kodi kutokana na kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Anasema majengo ya biashara yanayomilikiwa na taasisi za dini lengo lake ni kuendeleza pamoja na kutoa huduma, hivyo Serikali inatakiwa kuangalia namna ya kuyapa unafuu katika utozwaji wa kodi.

“Hatupingani na Serikali kuhusu kulipa kodi lakini katika majengo ambayo yanamilikiwa na taasisi za dini lakini yanatumika kuendesha biashara, Serikali ingeangalia namna ya kuyapunguzia kodi kutokana na kuwa pamoja na biashara lakini lengo lake kuu ni kuendeleza taasisi pamoja na kutoa huduma,” anasema Sheikh Mataka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here