KODI MAJENGO SI VILE, MTAZAMO MPYA WAHITAJIKA 

0
508

Na Mwandishi Wetu


PAMOJA na kuongeza muda mara mbili juu ya ulipaji kodi ya majengo, sasa ni wazi kodi hiyo inachoweza kufanywa ni kuwa kijungu jiko tu kwani jumla ya mapato yake yaliyokusanywa hadi sasa ni kiduchu.

Taarifa ya awali ya Wizara ya Fedha na Mipango ni kuwa kiasi kilichokusanywa kimefikia shilingi bilioni 32.5 chini ya matarajio ya wengi kuwa ingekuwa msingi mkubwa wa mapato ya Serikali.

Makisio ya makusanyo 2016/17 ni shilingi bilioni 58/- na  taarifa ya awali inaonesha kuwa hayo ni mapato kutoka  miji, majiji na halmashauri  30 kama mfano kwa mamlaka 183 kwa nchi nzima ili kupata uzoefu wa jumla. Ni makusanyo ya miezi sita kuanzia Oktoba 2016 hadi Julai 15 mwaka huu kikiwa ni asilimia 56 ya malengo.

Mapato hayo ni zaidi ya yale yaliyopatikana kwa mwaka 2015/16, ambapo kiasi kilichokusanywa na halmashauri kilikuwa ni asilimia 56  ya malengo na kukusanya shilingi bilioni 28.3/- pekee.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ametoa shukurani kwa wananchi ambao wameitikia wito wa kulipa kodi hiyo kwa wingi na kuwa mfano wa utekelezaji kama watu wakipata elimu na wakiamini matumizi yanayofanyika ya kodi zao.

Hii ni muhimu kwa sababu Serikali zote duniani huishi kwa kutegemea kodi na mafanikio ya nchi ni namna inavyoweza kukusanya na kutumia kodi kwa maendelo ya nchi.

Wananchi husika ndio walipaji wakubwa  wa kodi wa nchi  husika na hivyo  hukatwa kodi kutokana na mapato  yao kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mapato ya majengo kiduchu

Mpaka sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haijaainisha kwa nini kumekuwa na mapato kidogo zaidi.

I ya kusema zoezi linaendelea na huenda mambo yakawa mazuri zaidi pamoja na kusema ni mmapato ya miezi sita tu kwa hiyo sio mabaya kwani yamepita yale yale yaliyokusanywa na  halmashauri kwa mwaka jana.

 

Lakini kuna malalamiko toka mamlaka za serikali za mitaa zikidai kuwa TRA kama mtendaji wa Serikali Kuu inapora madaraka na mapato ya serikali za mitaa na hivyo kuzifanya zikose uwezo wa kushughulikia matatizo ya kijamii na kijirani kwani ni rahisi kwa serikali ya mtaa kuona tatizo na kulishugulikia mapema badala ya Serikali Kuu iliyoko mbali na wananchi na walipa kodi husika na hivyo kukosa kipaumbele.

Serikali Kuu ilishatoa tamko kuwa awali kuwa kusiwe na kuchanganya mambo kwani TRA ni mkusanyaji tu na sio mpanga matumizi kwani baada ya kutoa  gharama za uwakala fedha hiyo itapelekwa kwenye Mamlaka husika ya Utawala na wao ndio watapanga matumizi yake. Vilevile ni TRA yenye Mamlaka na jukumu kisheria kukusanya mapato mbalimbali ya serikali nchi nzima na hapo awali ilikasimu majukumu hayo Serikali za Mtaa na sio vinginevyo.

Isitoshe, TRA inasema kuwa majalada ya walipa kodi na jedwali zake pamoja na kiwango kitapangwa na halmashauri husika kutegemea na hali halisi ya uchumi wa wakazi wake. Hivyo basi madai yanayotolewa  ni athari ya mpito tu na hivyo hayana msingi na kusema kuwa TRA ndio yenye wataalamu stahiki wa kukusanya kodi na mapato mbalimbali.

 

Ni kweli kuwa kuna msingi mmoja wa kodi ni kuwa hakuna kodi bila uwakilishi lakini msingi huu madhubuti wa utozaji kodi hiyo upo  na unaiwezesha TRA kwa kupitia maamuzi ya Bunge na Baraza la Mawaziri kama wawakilishi wa wananchi.

Kipindi cha Mpito 

Lazima tukubali kwa muda mrefu hatujafanikiwa kukusanya kodi stahiki na kutoka kwa watu wengi.

Tumekuwa na mfumo wa kodi kinzani ambao huwaacha wengi bila kulipa kodi na kufanya wachache ambao ni wafanyakazi (PAYE) kulipa kwa niaba yao na hivyo kufanya viwango vyetu kuwa juu sana na vya kutisha. Isitoshe matajiri wetu hawalipi kodi ipasavyo wakati masikini wanalipa ingawa kwa mbinde.

Hali hiyo imeifanya kodi ya majengo ionekane kama  kitu kisichostahili na wanasiasa wanapigia upatu kudai inaonea wananchi kwa kuwakatisha tamaa kuwekeza katika uchumi wa nchi yao.

Kwa upande mwingine watu wanasema viwango vya kodi hiyo ni vidogo sana ukifananisha na kile walichokuwa wanalipa mwanzoni katika maeneo yasiyopimwa ilikuwa shilingi elfu hamsini (50,000/) kila jengo jijini Dar es Salaam; utafanya  nayo nini fedha hiyo  kwa kutoza shilingi 10,000kwa matamko ya wanasiasa?

Kiwango hicho ni kidogo sana hivyo hakifai kwani haileti mantiki kuwaweka watu wengi bila majukumu ya kulipa kodi.

Wenye majengo wanategemea kwa wao kulipa kodi hiyo ni kuwa barabara zao za mitaani zitajengwa kwa lami na sio vumbi na kuweko kwa mitaro ya maji machafu na nyumba kunyunyuziwa dawa za kuua wadudu na mbu. Elfu kumi itafanya nini kwa hayo?

Vipi ulinzi wa zimamoto, wanahoji wenye majengo kwani wanaona ni kichekesho kama mchuzi wa kuku kwenye chakula cha msiba!

Wanahoji walipaji kodi hii haikutenganisha au kuchambua kati ya mtu anayetoza kodi kwa nyumba ambayo kwa Dar es Salaam ni zaidi ya Sh 500,000 na yule mwenye wapangaji wa vyumba kwa shilingi 50,000 ni makosa kuwafanya wote walipe kodi ya Sh 10,000 wakati wanapata kipato cha aina mbalimbali?.

Wataalamu wa uchumi wanasema kigezo kingekuwa kiasi cha kodi cha mwenye nyumba anachopata na si jengo pekee, kwani haitoshi.

Wakikamatwa kwa kukwepa kodi wahusika hawapewi adhabu kubwa zaidi ya ‘kuombwa’ walipe haki ya Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here