NA MWAMVITA MTANDA, Kigali
LICHA ya aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma, kuondoka ndani ya kikosi cha AS Kigali, lakini mashabiki wa soka nchini Rwanda wanataka arejee kuinoa Rayon Sport.
Kabla ya kupata kibarua ndani ya klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba, Djuma alikuwa akiifundisha Rayon Sports, ambayo aliiwezesha kutwaa ubingwa.
Na baada ya kutemana na Simba, kocha huyo alijiunga na AS Kigali ya hapa ambayo hakudumu nayo, baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na watendaji wengine wa benchi la ufundi la timu hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA, jana, shabiki maarufu wa Rayon Sports, Akizimana Godfrey alisema anaamini Djuma ni kocha mwenye uwezo mkubwa na bado wanamkumbuka kwa kuisaidia Rayon Sport kutwaa ubingwa.
Aliutaka uongozi wa klabu hiyo kuangalia uwezekano wa kumrudisha kufanya kazi naye kwa mara nyingine.
“Kitu ambacho timu zetu zinashindwa kubaki na Djuma ni kwamba hawaelewi nini anataka, Djuma anataka kupewa nafasi ili afanye kazi yake vizuri.
“Kwa uwezo alionao, hata akikabidhiwa timu bila msaidizi anaweza kufanya vizuri, ni kocha mzuri na mwenye mbinu za kimataifa,”alisema Akizimana na kuongeza.
“Hata kama Rayon inafanya vizuri,lakini bado haijafikia kiwango ilichokuwa nacho Djuma.”