PARIS, UFARANSA
ALIYEKUWA nyota wa soka wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Patrick Kluivert, ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa michezo katika klabu ya mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa, PSG.
Nyota huyo aliwahi kuwika katika kipindi chake kabla ya kustaafu soka huku akiwa na klabu ya Lile ya nchini Ufaransa mwaka 2008, hivyo kutokana na uwezo wake na uzoefu katika soka, uongozi wa PSG umeona bora umpe jukumu hilo.
Ni miaka mitatu sasa tangu klabu hiyo iachane na Mkurugenzi wao, Leonardo Arauo, hivyo ilikuwa inaendesha shughuli zake bila ya nafasi hiyo kuzibwa.
Tangu Kluivert astaafu soka, alipata nafasi ya kuwa kocha msaidizi wa timu mbalimbali kama vile AZ Alkmaar, Brisbane Roar, NEC Nijmegen na timu ya Taifa ya Uholanzi, hata hivyo aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Jong FC Twente na Curacao.
Inadaiwa kwamba tangu nyota huyo astaafu soka, hakufanya makubwa sasa toka kipindi hicho hadi sasa cha kuwashawishi PSG kumpa nafasi hiyo, lakini wanaamini wanaweza kufanikiwa kupitia kiongozi huyo.
Naibu Mkurugenzi wa klabu ya Lille, Jean-Michel Vandamme, amedai kwamba PSG wanaweza kufanikiwa au kutofanikiwa mara baada ya kumchagua kiongozi huyo.
“Wengi wanajua uwezo wa Kluivert tangu akiwa mchezaji, lakini sidhani kama alikuwa amejiandaa kwa ajili ya kuwa kiongozi wa timu kubwa kama PSG, anaweza kufanikiwa au kutofanikiwa kwa kuwa hana uzoefu na idara hiyo, hivyo PSG wanatarajia kuona chochote kikitokea.
“Alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza soka, lakini inaweza kuwa ngumu kuwaongoza watu na kuleta mafanikio ndani ya klabu hiyo,” alisema Vandamme.
Hata hivyo, inadaiwa vyombo mbalimbali vya habari nchini Ufaransa vimekuwa vikimzungumzia kiongozi huyo na kushangazwa na klabu hiyo ya PSG kuwaacha viongozi mbalimbali ambao wanadaiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutumikia nafasi hiyo lakini wao wakaamua kumchukua kiongozi huyo.
Kluivert na viongozi wake katika nafasi hiyo wametakiwa kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuleta maendeleo ya soka ya klabu hiyo kubwa nchini Ufaransa, ili kuweza kuzima kelele zinazoendelea nchini humo.
Hata hivyo, Kluivert amewatoa wasiwasi viongozi na wadau wa soka kwamba ataweza kupambana na kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kutimiza malengo yao.
“Ninaamini klabu imeona kuwa ninaweza kuipeleka pale ambapo inataka kufika, kikubwa kilichopo kati yangu na viongozi wangu kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu yote kama inavyotakiwa.
“Sina maneno mengi, kilichobaki ni kufanya utekelezaji ili walionipa jukumu wawezi kufurahia na maamuzi yao, ninahitaji ushirikiano wa hali na mali kuweza kutimiza malengo,” alisema Kluivert.