LIVERPOOL, ENGLAND
KOCHA wa klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp, amesema hajafurahishwa na kauli ya kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ya kudai kwamba Liverpool itakuwa na wakati mgumu msimu ujao.
Mourinho mwishoni mwa wiki iliyopita alifunguka na kusema kwamba, usajili ambao unafanywa na Liverpool katika kipindi hiki cha majira ya joto, utawafanya wawe na wakati mgumu msimu ujao wa ligi.
Mbali na kuzungumzia suala la usajili kwa Liverpool, Mourinho aliendelea kwa kusema kwamba, Liverpool na Chelsea wamekuwa wakipambana juu ya soka la Ulaya, hivyo watakuwa na shida kubwa mara baada ya kuanza kwa msimu mpya kwa kuwa soka la Ulaya ni gumu.
Kutokana na kauli hiyo, Klopp ameweka wazi hajapendezewa na maneno ya kocha huyo mzoefu hasa katika kuizungumzia klabu ambayo haimhusu.
“Sijafurahishwa kabisa na kauli ya Jose Mourinho, kwanini mimi sizungumzii habari za Manchester United? Mourinho amekuwa akituzungumzia Liverpool, wote tupo kwenye maandalizi ya msimu, sidhani kama kuna klabu ambayo inaweza kuiuliza klabu nyingine maendeleo yao.
“Inawezekana kuwa Mourinho yupo sahihi, lakini hakuwa na sababu ya kuzungumza, ni kweli soka la Ulaya ni gumu, Chelsea wanaweza kuona utofauti msimu ujao kwa kuwa kikosi chao kilionekana kama kina wachezaji 13.
“Lakini hayo yote yanatokana na mipango ya timu husika, ila ukweli ni kwamba, si kauli sahihi, kila mmoja ana mipango yake,” alisema Klopp.
Kocha huyo amesisitiza kwamba anafurahia mipango yake ya usajili jinsi inavyokwenda katika kipindi hiki cha majira ya joto na hawana mpango wa kuongeza wachezaji wenye majina makubwa kwa sasa.
Hadi sasa Liverpool imefanya usajili wa wachezaji watatu kipindi hiki cha usajili, ambao ni Mohamed Salah kutoka AS Roma kwa kitita cha pauni milioni 36.9, kinda wa Chelsea, Dominic Solanke kwa pauni milioni 8 na beki wa pembeni wa Hull full, Andy Robertson, lakini bado Liverpool inaonesha nia ya kuwania saini ya nyota wa Southampton, Virgil van Dijk na mshambuliaji kutoka RB Leipzig, Naby Keita.
“Wengi kwa sasa wanaangalia juu ya usajili, nadhani kwa upande wangu sina wasiwasi kwa kuwa mambo yanakwenda vizuri, usajili unatikisa tofauti na ligi yenyewe, ninafurahi kuona ushindani uliopo,” aliongeza.