KLOPP: EVERTON HAWAKUWA NA SABABU YA KUTUFUNGA

0
709

LIVERPOOL, ENGLAND


 KLOPBAADA ya Liverpool kufanikiwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Everton kwenye uwanja wa Goodison Park, Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amedai kuwa hawakuwa na sababu ya kupoteza mchezo huo.

Kocha huyo amedai kuwa, aliamini mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ushindani uliopo dhidi ya wapinzani wao, lakini alijua timu yake ina nafasi kubwa ya kushinda.

Bao la pekee ambalo liliwapa alama tatu katika mchezo huo wa juzi lilifungwa na mshambuliaji wao, Sadio Mane, huku bao hilo likifungwa katika dakika za nyongeza baada ya dakika 90 kukamilika.

Hata hivyo, kocha huyo amemmwagia sifa mshambuliaji wake, Daniel Sturridge, ambaye alipiga shuti na kugonga goli na kisha Mane kumalizia.

“Nikisema kuwa tumefurahia ushindi huo linaweza kuwa ni neno la haraka sana, lakini acha iwe hivyo, ni kweli kwamba kila mmoja alikuwa na furaha kutokana na ushindi huo, kikubwa ni kwamba tumeweza kuondoka na alama tatu ambazo zinatufanya kupunguza nafasi ambayo tumeachwa na vinara Chelsea, wenye alama 43 na sisi tukiwa na alama 37.

“Ni wazi kwamba wachezaji wote walikuwa wanapambana kwa ajili ya kutafuta alama tatu, ninashukuru kuona mchango wa Sturridge pamoja na Mane ambao wametufanya tuzidi kuwa na furaha.

“Naweza kusema kwamba, Everton hawakuwa na uwezo wa kutufunga, japokuwa walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani, nilikuwa na asilimia kubwa ya kushinda mchezo huo, kilichobaki kwa sasa ni kuongeza jitihada kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Stoke City, Desemba 27,” alisema Klopp.

Kocha huyo ameongeza kwa kusema, kilichowaponza Everton ni kucheza mipira mirefu ambayo iliwasaidia kipindi cha kwanza, lakini hawakuweza kufanya lolote.

“Kipindi cha kwanza walituweza kwa kuwa walikuwa wanapiga mipira mirefu, lakini baadaye nikaweza kuwapanga vizuri wachezaji wangu na ndiyo maana tukawa tunacheza sawa.

“Hata hivyo, wapinzani walikuwa katika kiwango kizuri, lakini walishindwa kuzitumia nafasi ambazo walizipata zaidi yetu,” aliongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here