KOCHA wa klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp, ameanza mwaka kwa kumsajili kiungo wa Serbia, Marko Grujic, kwa kitita cha pauni milioni 5.1.
Mchezaji huyo ambaye alikuwa anakipiga katika klabu ya Red Star Belgrade ya nchini Serbia, alikuwa anaitumikia timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 21.
Mkataba huo na klabu ya Liverpool, utamfanya aitumikie hadi kiangazi mwaka 2020, ambapo Klopp anaamini kuwa mchezaji huyo atakuza kiwango chake na kutoa mchango kwa klabu hiyo.
Hata hivyo, mchezaji huyo ataanza kuitumikia klabu hiyo ifikapo Julai mwaka huu baada ya kumaliza mkataba wake na Belgrade.
“Tuna furaha kubwa kufanikiwa kuipata saini ya Marko Grujic, kwa kuwa ana kipaji cha hali ya juu na nilikuwa ninamwangalia mara kwa mara katika michezo yake mbalimbali.
“Tangu nilipofika hapa baadhi ya viongozi walinionesha wachezaji ambao wangependa kuwaona kikosini kutoka klabu ya Red Star Belgrade, lakini niligundua kwamba huyu ni mchezaji mwenye kipaji cha pekee hasa kutokana na umri wake.
“Kutokana na nilivyomuona anafaa kuwa katika kikosi changu, ni mrefu, anaweza kukaa na mpira, kutoa pasi za haraka, kutokana na umri wake anaweza kubadilika,” alisema Klopp.