Klitschko: Hata Fury akitumia ‘dawa’ nitamdunda tu

0
824

tyson-furyLAS VEGAS, Marekani

KUELEKEA pambano lake na Tyson Fury, mwanamasumbwi Wladimir Klitschko amesema kuwa hajali ikiwa mpinzani wake huyo atatumia dawa za kuongeza nguvu wakati watakapozichapa Oktoba 29 mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa Klitschko alipoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Muingereza huyo wakati walipozitwanga jijini Dusseldorf mwishoni mwa mwaka jana.

Ushindi huo ulimfanya Klitscho kupoteza mikanda yake mitatu ya WBA, WBO na IBF.

Miezi kadhaa baadaye, taarifa zilidai kuwa wangerudiana lakini ilishindikana baada ya Fury kuumia kifundo cha mguu ‘enka’ alipokuwa mazoezini.

Baadaye Fury alikumbana na mkono wa sheria kwa kushukiwa kutumia dawa za kuongeza nguvu.

Imeripotiwa kuwa, bondia huyo atalazimika kufika mbele ya mahakama Novemba mwaka huu.

Hata hivyo, Klitschko ameonesha kutotilia shaka uwezekano wa mpinzani wake kupanda ulingoni akiwa ametumia dawa hizo.

“Ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya mkataba, pande zote zinatakiwa kufanyiwa vipimo, sijali kuhusu chochote na nimeelekeza akili yangu katika mchezo huo,” alisema Klitschko.

Juzi Fury alishindwa kutokea kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao ungemkutanisha na Klitschko, lakini gari lake lilipata hitilafu wakati alipokuwa njiani kuelekea kwenye tukio hilo.

Licha ya umri wake wa miaka 41, Klitschko ameweka wazi kuwa hana mpango wa kustaafu mchezo wa ngumi.

“Kustaafu si swali hivi sasa.

“Hata kama hivi sasa mimi si bingwa, nafurahi kuwa katika michezo na kutumia nafasi hii kuleta upinzani, si kila mtu ana nafasi kama hii,” aliongeza bondia huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here