Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
KLABU ya mchezo wa kriketi nchini, Aga Khan SC, imeingia mkataba wa miaka miwili na kampuni ya HÄFELE East Africa Limited kwa udhamini wa jezi zitazotumika msimu wa 2025/2026.
Mkataba huo uliosainiwa mapema wiki hii jijini Dar es Salaam ambapo uongozi wa klabu hiyo umesema udhamini huo ni msaada mkubwa kwa klabu katika juhudi zake za kusaidia maendeleo ya mchezo wa kriketi nchini.
” Mkataba huu unasherehekea nia ya kampuni ya HÄFELE kujituma kuzalisha bidhaa bora za ujenzi na dhamira ya klabu ya Aga Khan kuandaa na kuendeleza vipaji vya mchezo wa kriketi nchini,” imesema taarifa ya uongozi wa klabu hiyo.
” Ushirikiano ambao Aga Khan SC inao na HÄFELE East Africa Limited, utakaoshuhudia kampuni hiyo ikiwa ni mdhamini rasmi wa jezi za klabu kwa misimu ya 2025 na 2026, ni ushuhuda wa kufanana kwa maono bora ya taasisi hizi mbili katika kazi na michezo”, amesema Kiongozi Mwandamizi wa klabu hiyo Ayzaz Jassani.
Amesifu ushirikiano huo na kubainisha kuwa ni hatua muhimu kuelekea katika mafanikio ya klabu hiyo na kuzifanya taaasisi hizo mbili kuonekana za kipekee.
“Kila mchezaji wa Aga Khan SC atavaa jezi hii kwa ufahari mkubwa, akionyesha heshima na utendaji bora unaozitanabaisha taasisi hizo mbili,” amesema.
Mchezaji mwandamizi wa klabu hiyo, Vipin Abraham, ameeleza kuwa udhamini huo unatoa fursa kwa mchezo kupiga hatua na kutengeneza mazingira bora kwa wachezaji chipukizi ambao ndio lengo kuu la shughuli za klabu yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HÄFELE East Africa Limited, Snehal Bakrania, akizungumza katika hafla kusaini mkataba huo amesisitiza kuwepo kwa uwiano wa kuthamini ubora kati ya kampuni hiyo na mchezo wa kriketi.
“Katika mchezo wa kriketi, wachezaji hujituma kuboresha mbinu za uchezaji na viwango. Katika namna hiyo hiyo, kampuni ya HÄFELE inaendelea kuwa mbunifu ili kuwa bora zaidi katika sekta iliyopo, ikitoa huduma bora zaidi. Leo tunasherehekea historia bora ya klabu, tukionyesha mlingano wa klabu hiyo na usahihi, ushirikiano, na ubunifu unaothaminiwa na kampuni ya HÄFELE”, amesema Bakrania.