KIZUNGUMKUTI OPEC KUIKABILI MAREKANI

0
404

Na Shermarx Ngahemera


MAMBO si shwari tena kwenye OPEC, umoja wa wauza mafuta duniani, baada ya Marekani kuamua kuwa muuzaji na si mnunuzi tu wa bidhaa hiyo.

Hali hiyo ilitarajiwa kwa muda mrefu, baada ya matatizo ya makinikia ya mafuta (shale) kupatiwa suluhisho la kiufundi na bei nzuri ya mafuta kuruhusu utengenezaji wa hazina iliyojaa tele Kanada na Marekani na hivyo kuruhusu kufanyika mageuzi ya uzalishaji na hasa kufuatia sera ya kihafidhina ya Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump na sera ya Amerika Kwanza.

Sera hiyo inaifanya Marekani kutojali lolote, ikiwamo mazingira, mradi kwa kufanya hayo inaipa Marekani faida kiuchumi na kubaki huru na kutoingiliwa kwenye mambo yake.

Habari hiyo si njema kwa OPEC, ambayo kwa muda mrefu imekuwa yenyewe ndiyo inapanga na kupangua bei kwa kutumia ushirika wao kwa kupanga kiasi gani cha mafuta kichimbwe na kuuza katika kutunza ule urari unaotakiwa kwao wa upatikanaji (supply) na wa mahitaji (demand) na dunia nzima.

Hali hiyo inatokea wakati OPEC haijapona kuuguza majeraha ya mdororo wa bei ya mafuta ulioletwa na mdororo wa uchumi wa dunia na kufanya bei ya mafuta kuanguka vibaya na kuuzwa chini ya dola 30 kutoka kawaida yake ya dola 100 kwa pipa miaka minne iliyopita.

Wakitafakari hali hiyo mbaya kwao, wanachama wa OPEC walikutana Paris, Ufaransa wiki iliyopita, ili kuona namna gani wanaweza kujinusuru kutokana na hali hiyo mbaya sokoni kutokana na ujaji wa Marekani sokoni kama muuzaji mafuta wakati miaka zaidi ya 60 amekuwa mnunuzi mkubwa na kushika soko la asilimia 25 ya manunuzi  ya mafuta ya dunia.

Wataalamu wa masuala ya biashara  ya mafuta wanasema kuwa hii ni hali mbaya sana kwa OPEC, ambayo inakabiliwa  na soko lililojaa mafuta yanayotafuta wanunuzi ambao hawapo wa kiwango cha Marekani na nchi inayokaribia mahitaji kama hayo ni China, ambayo uchumi wake umesimama kidogo kutokana na kuanguka mahitaji ya dunia ya bidhaa na hivyo kutishiwa kudorora uchumi.

Hali hiyo ni matokeo ya juhudi za Marekani kama nchi kuwa na sera ya kuhifadhi mafuta kwa woga wa rasilimali hiyo kwisha na hivyo kuwa na akiba kubwa sana inayohitaji kuvunwa kwa kutumiwa na nchi hiyo na ziada yake kuuzwa kwa nchi nyingine kutokana na mabadiliko ya sera, kwani sasa wafanyabiashara wanaruhusiwa kuuza mafuta chini ya himaya yao kwa nchi nyingine. Zamani kampuni za Marekani zilikuwa haziruhusiwi kuuza mafuta nje ya nchi hiyo kwa yale yanayochimbwa nchini humo. Marekani ni mzalishaji wa 3 hapo awali na sasa ni 2 kwa kiwango cha mafuta yazalishwayo nchini humo na ya kwanza kama muuzaji mafuta kama mfanyabiashara.

 

Juhudi za pamoja zahitajika

Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa, hali iliyopo sasa ni sawa na hali ya mwaka 1973, ambapo ulianzishwa umoja huo wa OPEC kulinda masoko ya bidhaa ya mafuta ambayo ilikuwa inauzwa kiholela na kuleta hasara kwa nchi zinazozalisha mafuta duniani.

Wanachama wa OPEC ni nchi 12 ambazo ni pamoja na Algeria, Nigeria, Saudi Arabia, Kuwait, Iran,  Qatar, Venezuela, Ecuador. Nyingine ni Angola, Ecuador, Libya na Iraq.    Saudi Arabia ni kiongozi mkuu.

Jumla ni nchi  12 ambazo zimejitahidi kuondokana na unyonyaji dhalimu wa rasilimali zao kwa wazi na kuziweka chini ya himaya ya OPEC, ili iweze kuilinda kwa umoja wao ambao ulifanikiwa sana na kuwa na nguvu kubwa sana katika ulimwengu usiotaka mabadiliko.

Mwanzoni hawakusikilizwa, lakini baadaye walikuwa huru na kusikilizwa na wote waliotaka na wasiotaka.

Sasa hali imerudi kama zamani na hivyo imerudi kwa kutafakari ili kupanga mikakati mipya ya kutoka hapo walipo na hivyo ni muhimu wakajipanga vilivyo.

Habari kutoka Paris, Ufaransa, ambako ulifanyika mkutano, imekubalika kuwa wanachama wafanye juhudi za pamoja  kujipanga kuhusu mwenendo wa soko, ikizingatiwa urari wa mahitaji na upatikanaji na kuzuia mdororo wa soko kwa kuzalisha zaidi na wote wafanye kinachotakiwa bila kujali itikadi za nchi zao, ila kwa maslahi ya biashara hiyo.

Kizingiti cha kwanza ni kuwafanya wale ambao si wanachama wa OPEC kutekeleza agenda zinazofanana na zile za chama, ikiwamo nchi za Urusi na Marekani na Norway zikubali ushawishi wa kupunguza uzalishaji.

 

Matumaini ya bei kupanda

Ofisa Mtendaji Mkuu wa British Oil Petroleum (BOP), Bob Dudley, ana matumaini makubwa ya kupanda bei, ingawa si sana, lakini si kuwa chini ya dola 30.

“Inategemewa bei itafikia na kukaa kwenye dola 50 kwa pipa hadi katikati ya mwaka huu,” alisema.

 

Hii ni miujiza, kwani wiki iliyopita mafuta yaliuzwa dola 27 kwa pipa kutokana na soko kuzidiwa na mafuta.

Alitoa dhihaka kuwa matanki yote na mabwawa ya kuogelea yatajaa mafuta, akionyesha ukubwa wa tatizo la kuzidiwa upatikanaji mafuta.

Alisema yeye anatarajia bei kuongezeka katika kipindi cha tatu na nne cha mwaka, lakini haitafikia dola 100 kwa pipa.

 

OPEC iko tayari kufungua majadiliano ya kupunguza uzalishaji, alisema

Patrick Pouyanne, Mtendaji Mkuu wa Kampuni kubwa ya mafuta na gesi ya Ufaransa, Total, kuwa bei itakuwa nzuri mwishoni mwa mwaka huu.  

 

Ni tatizo kubwa

 

Mdororo wa bei ni hatari, kwani faida yote iliyopatikana awali imeliwa na kuanguka bei kwa silimia 70 na hivyo kutishia kupoteza ajira na hivyo kukwama uwekezaji mpya katika miradi mipya kama ile ya gesi ya Tanzania, kwani mradi umekuwa ghali sana.

 

Ingawa haipendezi kwa wengi kusikia ni kuwa miradi mingi iko kwenye kusubiri na huenda hali ikawa bora baada ya miaka mitatu ndio soko litachanganya tena na mwenendo wa Marekani utatabirika kwa ufasaha zaidi.

 

 Urusi yapewa ujiko

 

Baada ya kutathmini hali, OPEC inaona lazima kuweko na mpango mkakati ambao utaishirikisha Urusi katika mipango yake, kwani inaamini ni juhudi za pamoja tu ndizo zinaweza kufanya soko liende wanavyotaka wao, kwani Marekani ujaji wake unatishia hali ya kila mmoja wao.

Katika ripoti yake ya kila mwezi, imekubali kuwa sera zinazofanana ni muhimu kwa kuweko soko inara.

 

Wakati akiba ndogo ya mafuta na uchumi unaoelekea kukua unaashiria kukua kwa mahitaji ya mafuta, lakini zinahitajika juhudi za wazi kufanya  mashauriano ya mara kwa mara juu ili kuimarisha mahitaji na umahiri wa soko la mafuta duniani, ili kupata bei nzuri.

Imani hiyo inatokana na ukweli kuwa ni kwa muda mchache sana mwaka huu toka washirikiane na Urusi, soko limeweza kuwa chini kidogo ya dola 50, kwani naye alipunguza uzalishaji na hivyo kufanya Marekani iingie sokoni, kwani mafuta ya makinikia ya mafuta (shale) gharama za utengenezaji ni za juu ya dola 45 na hivyo ikiuzwa bei chini Marekani hujitoa kwenye soko kwa ajili ya kupata hasara.

Wanachama wa OPEC walikubaliana mwaka  jana Novemeba kuwa uzalishaji upunguzwe kwa kiasi cha mapipa milioni  1.2 kwa miezi sita, ili kupunguza mdororo (glut) ya mahitaji ya mafuta. Wale ambao sio wanachama nao walipunguza kiasi kinacholinganishwa na hicho na hivyo kuleta matokeo chanya ya bei kupanda au kuimarika.

Urafiki wa mashaka

Matatizo ya OPEC unaweza kusema ya kujitakia kwa kulana kisogo kwa taasisi ambayo ilishakuwa na sera ya kupunguza uzalishaji ili ulingane na mahitaji ya soko, lakini kufika mwaka 2014 hadi 2016 waliacha sera hiyo na kufanya uzalishaji holela ili  uwe mwingi na bei ipungue ili kuzuia Marekani asiuze mafuta yake katika soko la dunia. Lakini mchimba shimo hujichimbia mwenyewe; na ndicho kilichotokea.

Matokeo ni kuwa, hiyo vunjabei kutoka dola 100 iliishia pabaya, kwani ilianguka vibaya sana hadi chini ya dola 30 na kuwaathiri waliokuwamo na wasiokuwamo na juhudi za kurudia bei kubwa zimeshindikana, kwani wazalishaji wengine wameingia sokoni na kuleta timbwili kubwa kwa wazalishaji kwani mahitaji yamedoda.

Urusi, ambayo ilitengwa awali kwa misingi ya kisiasa, sasa inakumbatiwa na OPEC kwa vile yeye ni mzalishaji mkubwa wa mafuta na gesi na matendo yake huathiri hali ya soko.

Tanzania na nchi zisizo na mafuta yake zilifaidika kwa bei ndogo, kwani bajeti iliweza kumudu, lakini imepata hasara ya kukosa uwekezaji katika mradi wake wa gesi na hasa ujenzi wa Mtambo wa LNG  kule Lindi, ambao umekwama hadi mwaka 2025.

Uzalishaji wa Marekani unaonekana kuanguka mwaka jana, OPEC inauona kuwa inazinduka na kupanuka zaidi mwaka huu 2017 na hasa kwenye masuala ya gesi.

Wazalishaji wengine nje ya soko wameonekana kuzidisha uzalishaji kwa mapipa milioni 0.95 na kati ya hizo,  Marekani kukua kwa kiasi cha milioni  0.82 kwa siku.

Biashara ya mafuta ina mambo mengi sana na mwenendo wake si rahisi kuujua na kuubashiri, kwani kuna vitu vingi vya kuzingatiwa na mara nyingi hubadilika badilika.

Wataalamu wanasema vyovyote itakavyokuwa, ujaji wa Marekani kwenye soko ni maendeleo ambayo yatasababisha mabadiliko mengi katika biashara ya mafuta na kuleta migogoro mingi ya maslahi ya mafuta.

Wachunguzi wa mambo wanadai kuwa hata safari ya Rais Donald Trump kwenda Saudi Arabia alifanya hivyo kwenda kuweka mikakati ya namna ya kubadili mwenendo ili Marekani iwe na sauti kubwa kwenye biashara hiyo, ikiungwa mkono na Saudi Arabia.  Aramco ndiyo kampuni kubwa ya mafuta Saudi Arabia na uzalishaji wake ni mkubwa kuliko kampuni yoyote duniani na Marekani ana hisa kwenye kampuni hiyo.

Wale wataalamu wa siasa na uchumi wote niliozungumza nao wamekubali kuwa dunia itegemee mabadiliko makubwa  kwenye masuala ya mafuta na mwenendo wake, haswa pale Rais Trump alipoweka wazi kuinanga Jamhuri ya Iran, nchi inayofuata demokrasia na kuikumbatia Saudi Arabia, nchi ya kimwinyi na inayoendeshwa  kwa misingi ya kidikteta.

Awali kwenye OPEC Iran ilikuwa inakwaruzana na Saudi Arabia, lakini sasa upele huo umepata mkunaji kwa maana ya Trump na hivyo tutegemee makubwa toka OPEC, kwani Rais huyo ataivunja kama haitafuata matakwa yake, kwani ataitumia Saudi Arabia kutekeleza ajenda zake kuvuruga taasisi hiyo amabayo ilionekana kufaulu na nchi wanachama kuneemeka. Trump sera yake ni Amerika Kwanza.

Ulimwengu inabidi wajue kuwa bei ya mafuta inapopanda mfaidikaji wa kiwango cha juu ni Marekani, kwani nchi zalishaji hupata chini ya asilimia 15 ya mauzo, kinachobakia ni mali ya Marekani kwa mfumo alioujenga  yeye!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here