Kiwango uchangiaji damu chaongezeka

0
556

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM 

MKURUGENZI wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dk. Magdelena Lyimo, amesema kiwango cha uchangiaji damu kimeongezeka kutoka asilimia 40 hadi 60.

Licha ya kuongezeka kwa kiwango hicho, alisema wako katika mpango wa kujenga kituo kikubwa cha damu Kanda ya Dodoma na tayari Sh bilioni 1.3 zimeshatengwa ili kufikia asilimia 100 za ukusanyaji damu. 

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa kampeni ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ iliyoandaliwa na maofisa habari walioko chini ya wizara hiyo, Dk. Lyimo alisema hatua hiyo ya ongezeko ni baada ya jamii kuwa na hamasa zaidi ya kuchangia damu.

“Kazi zetu ni kuhakikisha uwepo damu salama na ya kutosha na yenye ubora wa juu na ipatikane kwa wakati unaohitajika, tunahamasisha uchangiaji damu, tunatoa elimu, tunakusanya, tunapima, tunahifadhi na pia tunasambaza, tuna mwongozo wa uhamasishaji, ukusanyaji, usambazaji matumizi sahihi ya damu.

“Tuna vituo vya kanda saba, kuna Kanda ya Mashariki iko Mkoa Dar es Salaam, Kaskazini iko Kilimanjaro, Kanda ya Ziwa iko Mwanza, Kanda ya Magharibi iko Tabora, Kusini iko Mtwara na Kanda za Nyanda za Juu Kusini iko Mbeya.

“Kila kanda ina mikoa yake ambayo inahudumia. Pia kuna kanda za jeshi, hizi hazina mpaka wa kuhudumia,” alisema Dk. Lyimo.

Alisema mpango huo wa damu salama unafanya kazi na hospitali za kibingwa ili kuweza kurahisisha upatikanaji wa damu kwa wagonjwa.

Akizungumza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mine, Dk. Lyimo alisema ununuzi wa mashine 24 za maabara umerahisisha shughuli za upimaji wa maambukizi katika damu na makundi ya damu.

“Tumepata mashine mpya 24, kila kituo cha kanda kimepata mashine na gharama za mashine hizi ni Sh bilioni 13.2, kila kanda ina mashine nne ambapo mashine mbili ni za kupima maambukizi ya damu na mashine mbili za kupima makundi ya damu.

“Hizi za damu zina uwezo wa kupima sampuli 156 ndani ya saa mbili na ile ya kupima maambukizi inapima aina nne kama Ukimwi, homa ya ini B na C na kaswende. Hii ina uwezo wa kupima sampuli 100 ndani ya saa mbili, kwa sampuli 100 tunapata majibu 400 kutokana na kupima ugonjwa zaidi ya mmoja,” alisema Dk. Lyimo. 

Hata hivyo alisema kuna mashine ya kisasa zaidi ambayo inapokea sampuli 600 na inatoa majibu ndani ya saa moja.

“Kwa mfumo wa nyuma, sampuli zilikuwa zinapimwa 88 ndani ya saa tatu au nne na unapata jibu moja, kwahiyo ililazimu wawepo watumishi wanne tofauti na sasa hata uwezekano wa kufanya makosa umepungua.

“Tumeweza kuhakiki ubora wa huduma zinazotolewa, ‘tuna-deal’ na watu wote wa kutoa damu wanaweza kufanikisha zoezi, tumekuwa na viwango vya juu zaidi.

“Mpango wetu ni kuhakikisha tumeimarisha huduma na kanda zote saba zitafikia vigezo vya kitaifa na kimataifa,” alieleza Dk. Lyimo.

Kutokana na uhitaji wa mazao yatokanayo na damu, alisema uhitaji wake utakuwa mkubwa hivyo uimarishwaji unaendelea wa upatikanaji wake.

“Tutaongeza matumizi ya mazao ya damu kama plate late, plasma na hizi zinahitajika kwa wagonjwa mfano kama saratani, figo na hata moyo, hivyo tunataka mgonjwa apate kitu anachokihitaji kwa wakati,” alisema Dk. Lyimo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here