Elizabeth Kilindi – Njombe.
TAKRIBANI wananchi 250 wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe, wanatarajia kupata ajira itakayotolewa na kiwanda kipya cha kusindika matunda ya parachichi cha Olivado kinachotarajia kuanza kazi rasmi Februari,mwakani.
Hatua hiyo inakuja baada ya Wilaya ya Wanging’ombe kutoa eneo la ukubwa wa ekari 30 katika Kijiji cha Itulahumba ili kuongeza thamani ya zao la parachichi.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Ally Kassinge alisema ujio wa kiwanda hicho ni manufaa kwa wananchi ambapo wakulima zaidi 1,000 kutoka sehemu mbalimbali wamepata mafunzo ya zao hilo.
“Wakulima wetu walikua wanauza zaidi kwa utaratibu wa usafirishaji wa nje kulikua na awamu kwa maana kupaki kwake kwa kuchagua parachichi za kiwango cha kati na juu zaidi,lakini wenye kiwanda hiki wametuambia kuwa hakutakua na kuchagua kwa hiyo zile parachichi ndogo sana,parachichi za kati na kubwa zote zitakua zinatumika”alisema.
Kassinge aliongeza “Lakini jengine kiwanda hiki kitatumika eneo kwa ajili ya kupaki parachichi ambazo zitakua zinasafirishwa nje kwa ajili ya matumizi ya walaji kwa namna nyingine, badala ya Watanzania kutafuta soko la parachichi nje ya nchi hususani nchi za Ulaya hata matumizi ya parachichi za kawaida soko lake litakuwepo hapa hapa ndani”alisema.
Kuhusu utendaji kazi wa Serikali alitoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kwenda kuwekeza ndani ya wilaya hiyo kwa kuwa inayo ardhi ya kutosha ili kukidhi sekta za kilimo, viwanda, utalii na elimu.
Meneja wa kiwanda hicho, Bosco Richard alisema mipango ya kiwanda hicho ni kuwawezesha wakulima kulima kilimo hai chenye tija ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
“Lengo kubwa ni kuwasaidia wananchi waweze kulima kilimo hai na chenye tija ambacho kitamsaidia mkulima kupata soko la ndani na la nje kwa sababu tunawafundisha kulima kulingana na kiwango cha kimataifa kwa namna gani kutunza mashamba yao kwa sababu soko la parachichi ni kubwa kwa sasa,” alisema.
Mkazi wa Kijiji cha Itulahumba, Deo Msemwa alisema wamekuwa wakipata hasara kutokana na kukosa hela ya usafirishaji kwenda viwanda vya mikoa ya jirani na kuamua kuwauzia madalali ambao uwenda kuyauza kwa bei ya juu viwandani lakini ujio wa kiwanda hicho utasaidia kuondoa changamoto hiyo.