24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Kiwanda cha kuchakata nyama kuanza uzalishaji

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

KIWANDA cha kisasa cha nyama cha TanChoice kilichopo Soga, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kinatarajia kuanza uzalishaji mwezi huu kwa lengo la kutumia fursa ya uhitaji wa nyama katika nchi za Asia ambazo zimeathiriwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hiyo imekuja baada ya maambukizi ya virusi hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi katika nchi mbalimbali duniani ikiwamo uchakataji wa nyama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uwezeshaji, Uwekezaji wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), James Maziku, uwekezaji katika kiwanda hicho utaongeza fursa zaidi ya 500 kwa Watanzania.

Aidha, alisema uwekezaji katika mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh bilioni 35, ni moja ya mafanikio ya miradi ya viwanda vilivyoanzishwa katika maeneo maalumu ya uwekezaji baada ya kupata leseni kutoka EPZA.

 “TanChoice kilitakiwa kuanza uzalishaji baadae mwaka huu, lakini kutokana na uhitaji wa nyama katika nchi za Asia, kitaanza uzalishaji mwezi huu ili kutimiza hitaji hilo.

 “Kiwanda hiki chenye kutumia teknolojia ya kisasa, kitakuwa na uwezo wa kuchakata ng’ombe 1,000 na mbuzi na kondoo 4,500 kwa siku, tayari kimezingatia viwango vya kitaifa na kimataifa ambavyo husimamiwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) ikiwa ni pamoja na mfumo wa usimamiaji wa usalama wa chakula ISO 22000 na usimamizi wa mfumo wa ubora ISO 9001,” alisema Maziku.

Alisema kiwango cha nyama kitakachosafirishwa nje ya nchi kitatokana na mahitaji ya soko huria ambalo lipo Falme za Kiarabu, Oman, Qatar, Saudi Arabia, China, Indonesia, Vietnam na Malaysia.

 “Usafirishaji wa nyama na bidhaa zake kutoka kiwanda cha TanChoice zitasafirishwa kwa magari maalumu au container hadi uwanja wa ndege au bandarini.

“Bidhaa hizi za nyama zitasafirishwa kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere wakati nyama na bidhaa za nyama zilizogandishwa zitasafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Maziku.

Alisema mradi wa kuchakata nyama utawahakikishia wafugaji wadogo wadogo soko la uhakika la mifugo yao hivyo kuongeza kipato.

“Kwa vile masoko makubwa ya nyama itakayochakatwa na kiwanda cha TanChoice ni ya Ulaya na Umoja wa Falme za Kiarabu, ni muhimu kuweka mkazo katika kuhakikisha bidhaa za nyama zinakuwa na viwango vya kimataifa,” alisema Maziku.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles