Safina Sarwatt, Kilimanjaro
Kiwanda cha kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi cha Kilimanjaro International Leather kilichopo Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kinakusudia kupanua masoko ya bidhaa zake ikiwemo viatu vya Jeshi.
Kiwanda hicho kinakusudia kupanua masoko ya ndani hapa nchini na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Nchi za COMESA.
Meneja Masoko na Mauzo wa Kiwanda cha Kilimanjaro International Leather, Donald Nkomavantu, ameyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea kiwanda hicho.
Amesena kiwanda hicho tayari kimefungua maduka ya kuuza bidhaa zake katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Moshi lengo likiwa ni kuhakikisha wanafungua maduka ya kuuza bidhaa zake nchi nzima.
Amesema tayari wameanza kupata oda ya kuuza na kusambaza bidhaa zake Kimataifa katika nchi mbalimbali barani Afrika .
Aidha, amaongeza kuwa, wanakusudia kuuza bidhaa zake katika nchi zote za ndani na nje ya Bara la Afrika.
Nkomavantu amesema kiwanda hicho ni mali ya Watanzani ambapo kinamilikiwa na uliokuwa mfuko wa PSPF kwa ubia na jeshi la Magereza na wamefanikiwa kufunga mitambo mipya ya kisasa kutoka nchini Itali yenye ubora wa hali ya juu.
Meneja huyo amesema kwa sasa kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi zaidi ya 200 wanaendelea na shughuli za uzalishaji wa viatu vya raia wa kawaida ikiwemo viatu vya kijeshi na bidhaa mbalimbali zitokanazo na ngozi.
Amesema kiwanda hicho kitakapomaliza mchakato wa kufunga mitambo yote kitakuwa na uwezo wa kuzalisha jozi 400 kwa siku na kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira zaidi ya 3,000 na kutoa wito kwa Watanzani kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
“Kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto kutoka kwa wafugaji na wachinjaji wa mifugo kushindwa kuandaa ngozi zenye ubora unaotakiwa kwani ngozi nyingi zinazofika kiwandani zinakuwa na matundu matundu.
“Uongozi wa kiwanda tayari umejiandaa kutoa elimu kwa wafugaji na wachinjaji wa mifugo namna bora ya kuchinja na kutunza ngozi ili kupata ngozi bora isiyokuwa na matundu,” Meneja Nkomavantu.