NAIROBI, KENYA
MATOKEO ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Kibra yaliyompa ushindi mgombea wa Orange Democratic Movement (ODM), Imran Bernard Okoth ni kama yamezidi kupandisha homa ya uchaguzi wa 2022 nchini Kenya hasa kwa upande wa Makamu wa Rais, William Ruto anayetizamwa kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo ambao ulikuwa umetajwa kama kinyang’anyiro kati ya mwanasiasa wa upinzani Raila Odinga na Ruto kuonyesha ubabe wa kisiasa.
Pamoja na kwamba Kibra ni ngome ya ODM ya kigogo wa siasa za upinzani, Raila Odinga ambaye ‘shaking hand’ yake na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta amekuwa akiitumia kumtisha Ruto, matokeo yake yalikuwa yakiaminika kutoa mwelekeo wa uchaguzi ujao.
Okoth wa ODM akibebwa kwenye kampeni na Raila alitangazwa mshindi kwa kura 24, 636 akifuatiwa na mgombea wa Jubilee McDonald Mariga aliyeshikwa mkono na Ruto akipata kura 11, 230 huku yule wa Amani Nation Congress (ANC) akichukua nafasi ya tatu kwa kura 5, 275.
Jana gazeti la Daily Nation la nchini Kenya liliandika kuwa; Ruto amewashutumu kimya kimya ‘maluteni’ (timu yake ya mkakati) wake wa karibu baada ya kupoteza jimbo la Kibra.
‘Maluteni’ hao walimuahidi ushindi katika jimbo hilo au kama wakishindwa basi kwa kura chache mno.
Kutokana na kukatishwa tamaa na askari wake wa miguu, chanzo kilicho karibu na makamu huyo wa Rais kililidokeza gazeti hilo kuwa Ruto alifuta mkutano uliopangwa kufanyika Alhamis jioni katika makazi yake ya Karen.
Kikosi hicho kinachoongoza kampeni ambacho kilikuwa ardhini kilikuwa njiani kwenda kukutana na Ruto wakati alipofuta mkutano huo.
Mtu wa karibu na Ruto ambaye alizungumza na Daily Nation alisema makamu huyo wa rais alikasirishwa baada ya kutumia muda mwingi, nguvu na rasilimali nyingi katika kampeni ambazo mgombea wa Jubilee McDonald Mariga ameambulia kura 11,280 dhidi ya zile za Okoth 24,636.
“Bosi alibadilsha uamuzi, alipiga simu na kusema hatapokea mgeni yeyote …alikuwa katika hali ya hasira,” kilisema chanzo hicho.
“Alikuwa mkarimu mno, wakati tulipokuwa tunakwenda kwake, alikuwa anatupa chakula na fedha,”alisema James Onkundi, ambaye ni mwendesha boda-boda katika jimbo la Kibra.
Licha ya jumbe kali alizotuma kupitia mtandao wa Twitter
akidai kuwa kushindwa huko kulionekana kama ushindi kwake, Ruto pia alionekana kukerwa na baadhi ya maofisa wa Jubilee ambao walishindwa kusapoti kampeni za Mariga.
Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju na maofisa wengine walioungana na Rais Uhuru Kenyatta walishindwa kuingia kwenye kampeni wakati viongozi wa upande wa pili kama wao waliingia kumuunga mkono Okoth.
Wakati hayo yakiendelea kimyakimya Ruto alimpongeza Okoth lakini ameitangazia ODM kivumbi cha siasa katika siku zijazo.
Makamu huyo wa rais anayejipanga kumrithi Kenyatta alisema kuwa chama cha Jubilee kimepata umaarufu katika eneo la Kibra na kujitengenezea barabara ya kisiasa kwa kupata uungwaji mkono na wakazi.
Alisema kuwa chama cha Jubilee kimepenyeza katika ‘chumba chao cha kulala’ na kupata uungwaji mkono kutoka kwa wakazi.
Kikosi cha Jubilee kinasema kimejipenyeza katika chumba cha kulala, kutokana na kujinyakulia asilimia 26 kutoka ya awali ya 12 katika uchaguzi wa 2017.
“Wapinzani wetu walishuka kutoka asilimia 78 (2047) hadi 52. Walipata kiti lakini tumewapa notisi,” alionya.
Awali kabla ya ushindi huo wa ODM, Ruto alikuwa mwingi wa ujasiri na kusema kuwa Mariga atapata ushindi mkubwa katika eneo hilo.
Alipuuzilia mbali usemi kwamba Kibra ni kama chumba cha kulala cha Raila na kudokeza kuwa ataingia huko na kumfurusha mwenyeji.
Hata hivyo, ndoto yake ya kupata ushindi ilididimia baada ya mgombea wa ODM kuanza kuashiria kupata ushindi pindi tu kura zilipanza kuhesabiwa.
Baada ya matokeo hayo wapambe wa Raila walionekana kusambaza vichwa vya habari kwenye mitandao ya kijamii vinavyosomeka; ‘William Ruto apokea kichapo kwa kuingia chumba cha Raila cha kulala’
SIRI YA ODM
Wakati huo huo, viongozi wa ODM, wamefichua kuwa walitumia mbinu ili kuhakikisha kuwa mgombea wake ameibuka mshindi.
Ijumaa, maafisa wa chama hicho walikiri kwamba walikuwa na kituo cha kujumlisha matokeo baada ya kuhesabiwa vituoni ili kuzima wizi wa kura.
Wakizungumza baada ya Okoth kutangazwa mbunge mteule wa eneo hilo, viongozi hao walisema hawakutaka kumuaibisha kiongozi wa chama chao Odinga ambaye alitangaza eneo hilo kuwa chumba chake cha kulala kisiasa.
“Mara hii tulijipanga na kulinda kura zetu kwa njia zote. Lakini kando na hilo, mpinzani wa Jubilee hakuwa chochote akilinganishwa na Imran Okoth. Huwezi kuchokoza Odinga Kibra na utarajie kwamba utashinda huku wafuasi wake wakiwa wamenyamaza tu,”alisema Mwenyekiti wa chama hicho, John Mbadi na kuongeza;
“Sisi hatukutumia ghasia dhidi yao jinsi wanavyodai bali mara hii raia ndio walijitokeza kukomesha ufidhuli wao wa kumtusi Odinga kila walipofanya mikutano maeneo mengine ya nchi.”
Mbadi alisema walikuwa na kituo chao cha kujumuisha matokeo katika ofisi za wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga na matokeo waliyopata yalitofautiana kidogo tu na yale yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi (IEBC).
Mkurugenzi wa uchaguzi wa ODM aliye kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa na mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, alisema hawangeruhusu Ruto na wabunge wa Jubilee kuteka eneobunge hilo kisiasa.
“Huwezi kuja Kibra na upimane nguvu na baba. Sasa tuna ufunguo wa chumba cha kulala na tumewaonyesha kivumbi kwa kupata ushindi mkubwa. Wao ni waoga na sasa wametawanyika wote,” alisema Mohamed katika kituo cha kujumuisha kura cha Chuo cha Mafunzo cha Nairobi City Inspectorate.
Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na wagombea 24, Okoth sasa atarithi kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha nduguye, marehemu Ken Okoth aliyeaga dunia kutokana na ugonjwa wa saratani mnamo Julai 2019.
“Ninawashukuru sana wapigakura wa Kibra kwa kunipigia kura na kuonyesha kwamba fedha haziwezi kununua uongozi. Namshukuru sana kiongozi wa chama chetu Raila Odinga na viongozi wote wa ‘handshake’ walionifanyia kampeni. Naomba wapinzani wangu tushirikiane kujenga Kibra,” alisema.