26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kivuko MV Ilemela chaingizwa Ziwa

Benjamin Masese-Mwanza

SERIKALI imepokea kivuko cha MV Ilemela ambacho ni kati ya vivuko vitatu vinavyojengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport na kukiingiza katika Ziwa Victoria kwa majaribio kabla ya kuanza kutoa huduma kati ya Kisiwa cha Bezi na Kayenza vilivyopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kivuko hicho kilichojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 2.7 kilipokewa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye ambaye aliagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na Wakala wa Huduma za Meli Tanzania (Tasac) kuhakikisha wanasimamia ukaguzi na kutoa leseni mara moja.

Nditiye alisema kukamilika kwa kivuko hicho kutasaidia wananchi wa Bezi- Kayenze ambao walikuwa wanatumia mitumbwi na boti za watu binafsi kuwa na usafiri wa uhakika.

Alisisitiza kuwa Serikali imekusudia kuboresha huduma za majini katika bahari, maziwa na mito ili wananchi wote waweze kuwa na mawasiliano yatakayowezesha kukuza uchumi wao.

 “Kivuko hiki kina urefu wa mita 37, upana mita 10 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0.75 hadi 1.4 ambapo kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100, yaani abiria 200, magari 10 na mizigo ambapo kimegharimu Sh bilioni 2.7 ambazo zimetolewa na Serikali.

“Hadi sasa mkandarasi ambaye ni Songoro Marine amekwishalipwa asilimia 90 ya fedha zote na baada ya ukaguzi wa Temesa na Tasac tunamalizia fedha zote, kama mnavyoona hapa kuna vivuko vingine viwili vinaendelea kujengwa, ambavyo ni MV Chato na MV Bugorola ambavyo navyo tutavipokea Februari mwaka huu,” alisema Nditiye.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema wakati anagombea ubunge ndani ya jimbo, aliwahidi wananchi kuwapo na kivuko ingawa hakikuwapo katika ilani ya CCM na baada ya kushinda aliamua kumwomba Rais Dk. John Magufuli kumsaidia.

Naye Mtendaji Mkuu wa Temesa, Japhet Masele alisema hadi sasa Rais Magufuli ametoa Sh bilioni 9.9 katika bajeti iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ujenzi wa vivuko nchini kikiwamo cha MV Ilemela ambacho mkataba wake ulisainiwa Agosti 29, mwaka juzi na ujenzi kuanza Septemba mwaka huo.

Katika hatua nyingine, Nditiye alimwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo kufanya utafiti wa haraka na kubaini ni mnara gani unafaa kujengwa katika eneo la Bezi-Kayenze ili kuwa na mawasiliano kwa wananchi wanaoishi huko na maeneo jirani ya Ukerewe.

Agizo hilo alilitoa baada ya Mbunge wa Ilemela, Mabula kumweleza kuwa wananchi wa Bezi-Kayenze hawana mawasiliano na amekuwa wakipata shida, hususan pale inapotokea dharura katika Kituo cha Afya Sangabuye kinachohudumia wakazi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles